Prosper Niyoyankana (picha), mwanasheria wa Hussein Radjabu.
Na RFI
Kiongozi wa zamani wa chama tawala Cndd-Fdd nchini Burundi,
Hussein Radjabu anasadikiwa kuwa ametoroka jela usiku wa Jumapili kuamkia
Jumatatu Machi 2 mwaka 2015. Hussein Radjabu alikua akizuiliwa jela kwa kipindi
cha zaidi ya miaka 7, tangu mwaka 2007.
Hussein Radjabu alifungwa jela kwa tuhuma za kupanga njama
za mapinduzi dhidi ya utawala wa Pierre Nkurunziza. Alihukumiwa kifungo cha
miaka 13 jela.
Wadadisi wanasema kutoroka kwa Hussein Radjabu ni pigo kubwa
kwa utawala wa Pierre Nkurunziza.(P.T)
Hata hivyo wafuasi wengi wa kinara huyo wa zamani wa chama
tawala Cndd-Fdd, wanahisi kwamba huenda ameondolewa jela na kuuawa.
Kiongozi wa jela kuu la Mpimba, mjini Bujumbura, ambako
amekua akizuiliwa Hussein Radjabu, amethibitisha taarifa ya kutoroka kwa kinara
huyo wa zamani wa chama tawala.
Lakini mwanasheria wake, Prosper Niyoyankana ameiomba
serikali ya Burundi kufanya kilio chini ya uwezo wake ili kifahamishe wapi
amepelekwa mteja wake. Prosper Niyoyankana anahisi kwamba mteja wake ameuawa.
Hayo yanatokea wakati kunaripotiowa mpasuko katika chama
tawala, baada ya baadhi ya wafuasi vigogo wa chama hicho kutoa misimamo yao
kuhusu kugombea kwa rais Pierre Nkurunziza kwa muhula wa tatu.
Rais Pierre Nkurunziza anakabiliwa na upinzani ndani na nje ya
chama chake hususan vyama vya upinzani, mashirika ya kiraia pamoja na Kanisa
Katoliki nchini Burundi.
Hayo yanajiri wakati serikali ya Burundi iliandaa mwishoni
mwa juma lililopita maandamano ya amani ambayo yaliitikiwa na halaiki ya watu,
wengi wao wakiwa wanafunzi na wafanyakazi wa serikali.
Upinzani ulidai kwamba maandamano hayo yaliandaliwa na chama
tawala ili kuonesha kuwa kina wafuasi wengi, huku baadhi ya mashirika ya kiraia
yakikosoa maneno yaliyokua yakitumiwa na waandamanaji kama vitisho kwa baadhi
ya viongozi wa mashirika hayo ya kiraia
No comments:
Post a Comment