Mbeya/Dar. Wakazi wa jijini hapa juzi walizua
tafrani baada ya kufunga ofisi za Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco)
kwa muda wakidai kupewa majibu kuhusu tatizo la upatikanaji wa umeme
lililodumu kwa zaidi ya siku tano.
Tukio hilo lilitokea jana saa 4:00 asubuhi baada
ya wateja hao kusubiri majibu kutoka kwa wahusika, ambao awali
walitangaziwa kuwa huduma hiyo
ingeanza kupatikana juzi, lakini mpaka jana tatizo hilo lilikuwa likiendelea.
ingeanza kupatikana juzi, lakini mpaka jana tatizo hilo lilikuwa likiendelea.
Wakazi hao waliwafungia wafanyakazi wa Tanesco wa
kitengo cha malipo, wakisema kuwa hawafanyi kazi yoyote na hivyo
hawatakiwi kutoka nje. Hali hiyo ilidumu hadi askari wa walipowasili na
kuwashauri waondoke.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti ofisini hapo,
wateja hao walisema baada ya kukosekana kwa huduma ya luku kwa siku
tatu, jana kupitia simu zao za mkononi walipokea ujumbe uliowataarifu
kuwa huduma hiyo ingeanza kutolewa jana kwa mawakala na katika ofisi za
Tanesco, hata hivyo hali haikuwa hivyo.
Mkazi wa Mwanjelwa, Dickson Mwangunga alisema watendaji wa shirika hilo wanatoa taarifa zisizo sahihi na kusababisha usumbufu.
“Ni vema kama wangetoa taarifa sahihi, watu
tumefika hapa kwa ajili ya kununua umeme, lakini huduma hiyo haipo.
Baadhi yao wanatuambia eti hali bado haijatengemaa, wengine wanasema
tusubiri na muda unazidi kwenda, sasa nani mkweli? ndiyo maana tumeamua
kuzifunga ofisi zao watupe jibu sahihi lini huduma hii itatengemaa,”
alisema Mwangunga.
Hata hivyo, sakata hilo liliokolewa na mkuu wa
upelelezi wa Wilaya ya Mbeya, Kitinkwi Mtatiro ambaye alifika katika
ofisi hizo na kuwaomba wateja hao warejee nyumbani hadi watakapopewa
taarifa ya kurejeshwa kwa huduma na uongozi wa Tanesco.
“Nawaomba mfungue milango ya ofisi, waacheni
wafanye kazi hili ni tatizo limetokea. Hata wao hawapendi karaha hii
itokee ni vema mkawa watulivu msipende kujichukulia sheria mkononi.
Jambo hili linaweza kuvuruga amani,” alisena Mtatiro.
Akizungumzia hali hiyo, meneja wa Tanesco wa
Mbeya, Amos Maganga aliwaomba wananchi kuwa watulivu kwa kuwa tatizo
hilo ni la kitaifa na mara mitambo itakaporekebishwa watajulishwa
kupitia simu zao za mkononi.
Dar es Salaam
Jijini Dar es Salaam, wananchi waliendelea kulia na tatizo hilo lililodumu kwa siku tatu mfululizo.
Baadhi yao wamelalamikia hasara wanayoipata kwa
sababu ya kukosa umeme na kushindwa kufanya kazi za uzalishaji
zinazotegemea uwapo wa umeme.
No comments:
Post a Comment