Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, (Utawala Bora), George Mkuchika
Watumishi 25 kati yao sita wakiwa wafanyakazi wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) waliburuzwa mahakamani kwa tuhuma za rushwa kati ya Julai mwaka jana hadi Januari mwaka huu.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, (Utawala Bora), George Mkuchika (pichani), alisema hayo jijini hapa jana katika semina kuhusu Utawala Bora na Mikakati ya Kupambana na Rushwa katika ofisi za umma.
Washiriki wa semina hiyo wanatoka taasisi za umma, sekta binafsi, viongozi wa dini na washirika wa maendeleo pamoja na wawakilishi kutoka taasisi za kupambana na rushwa kutoka Kenya, Rwanda, Uganda na Burundi.
“Kama serikali, tunajitahidi kupambana na rushwa katika sekta ya umma kama mnavyojua, rushwa inatengeneza umaskini, kuongeza pengo kati ya maskini na tajiri na kufanya jamii isiweze kuwa na utulivu na kupunguza uwezo wa nchi kufikia maendeleo katika ngazi zote,” alisema.
Alisema rushwa kwa upande wa TRA inaweza kusababisha hasara kubwa kwa mapato ya serikali, kupoteza uaminifu na kuchafua sura ya mamlaka hiyo.
Hata hivyo, alisema pamoja na juhudi zote ambazo zimekwishafanywa, bado rushwa imekuwa ni changamoto ndani ya TRA na kama haitavaliwa njuga, itaendelea kubomoa mapato ya serikali.
Alisema wafanyabiashara wanaoagiza bidhaa toka nje ambao siyo waaminifu, wanawarubuni baadhi ya maafisa wa TRA ili kuweka alama za uwongo kwenye bidhaa hizo na mfano mzuri zaidi ni pale bidhaa za viwandani zinapowekewa alama kama ni bidhaa ghafi.
“Kutokana na mtandao wa rushwa, hata uchunguzi wa bidhaa haufanywi ipasavyo. Rushwa inapofua wafanyakazi wa TRA wakati wakifanya ukaguzi katika makontena ya bidhaa kiasi hata kudanganya kwamba bidhaa iliyomo yaani kama vifaa vya ujenzi au nguo kuelezwa kuwa ni mzigo wa chandarua,” alisema.
No comments:
Post a Comment