Maofisa polisi wa Jiji la Mwanza wakijadiliana jambo katika Kituo cha Mabasi cha Nyegezi wakati wa mgomo huo.
Abiria wakiwa wamesimama ndani ya eneo la Kituo cha Mabasi cha Nyegezi baada ya kukoswa usafiri kufuatia mgomo huo, huku askari polisi akihakikisha ulinzi na usalama katika eneo hilo.
Abiria na wakazi wengine wa Jiji la Mwanza wakitaharuki mgomo wa madereva hapo Nyegezi.
Baadhi ya wasafiri wakizungumza na maofisa polisi wa Mkoa wa
Mwanza katika Kituo cha Mabasi cha Nyegezi.
Baadhi ya abiria waliokwama kusafiri wakiwa kwenye makundi wakijadili hatima yao.
Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana Baraka Konisaga (kushoto)
akiongozana na Ofisa wa polisi mkoani Mwanza kukagua kituo cha Mabasi cha
Nyegezi.
Mkuu wa Wilaya akiwatangazazia abiria waliokwama kuondoka waingie kwenye magari ili waanze safari zao, lakini abiria walipoingia hakuna gari lililoondoka kituoni hapo.
Na Johnson James, GPL- Mwanza
MADEREVA wanaoendesha mabasi ya abiria waendao mikoani
wamegoma kuendesha magari yote yanayofanya safari zake kutoka jijini hapa
kuelekea maeneo mbalimbali hapa nchini kutokana na baadhi ya viongozi wao ambao
wako jijini Dar es Salaam kukamatwa na polisi.
Akizungumza na waandishi wa habari, Makamu Mwenyekiti wa
Umoja wa Madereva Mkoa wa Mwanza, Shaban Wandiba amesema kuwa “sisi kama Umoja
wa Madereva wa Mabasi yaendayo mikoani, tumepokea taarifa kuwa kuna baadhi ya
viongozi wetu walioko huko Dar es Salaam wamekamatwa wakati wao ndio watetezi
wetu hivyo baada ya madereva kusikia hivyo wakasema kuwa hawataondoa magari
mpaka viongozi hao waachiwe huru na Jeshi la Polisi Mkoa wa Dar es Salaam.”
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana jijini hapa,
Baraka Konisaga amesema kuwa hakuna haja ya wananchi kuendelea kuteseka katika
maeneo ya kituo cha mabasi yaendayo mikoani cha Nyegezi bila sababu za msingi
kama kuna baadhi ya magari yameamua kugoma yapishe njia ili wanaotaka
kuwasafirisha abiria waendelee na safari zao.
Hata hivyo licha ya mkuu huyo wa wilaya kutoa tamko kwa
wamililiki wa mabasi ya Bunda, Happy Nation, Zuberi na mengine kuwa waondoe
magari yao mgomo huo umeendelea na hakuna dereva hata mmoja aliyejitokeza
kuwasha gari kuashiria kuanza safari ya kusafirisha watu.
Aidha nao baadhi ya abiria waliofika mapema katika Kituo cha
Mabasi cha Nyegezi kwa ajili ya kusafiri na kukumbana na adha hiyo wamesema
kuwa “Sisi hatukuwa na taarifa za mgomo huu na kama tungekuwa na taarifa yake
tusinge kata tiketi kwa ajili ya safari hivyo wengine hapa tunaenda Dar
kuangalia wagonjwa hivyo tunaiomba serikali iingilie kati mgomo huu, wazungumze
na hawa madereva wajue nini tatizo na wajue jinsi gani ya kutatua matatizo haya
yaliyopo".
Nao wamiliki wa magari hayo yaendayo mikoani wamesema kuwa
hawautambui mgomo huo na watawaambia madereva wao kuwasafirisha abiria hao
waliokata tiketi kwa jana ili wafike kwa wakati licha ya kuchelewa kuanza
safari hata hivyo licha ya wamiliki wa magari kutoa kauli nzito kwa madereva wa
magari yao madereva hao wamegoma kuondoa magari hali iliyofanya abiria
waliofika katika kituo cha Nyegezi kuwa katika hali ya sintofahamu baada ya
madereva hao kutoonekana katika maeneo hayo.
Mpaka mwandishi wa habari hii anatoka eneo la tukio hakuna
gari hata moja ambalo lilikuwa limeondoka maeneo hayo.
No comments:
Post a Comment