VIJEMBE vya kisiasa jana vilichukua sehemu kubwa ya mjadala wa Bajeti ya
Ofisi ya Waziri Mkuu unaoendelea, ambapo mvutano mkubwa ulikuwa kati ya
Serikali na vyama vya upinzani nani amechoka.
Akizungumza bungeni kwa vijembe, Mbunge wa Mtera, Livingstone Lusinde
(CCM), alisema hoja ya kambi rasmi ya upinzani kuwa Serikali imechoka,
inawezekana ni kweli ila haikuwekwa vizuri.
Alifafanua kuwa Serikali imefanya kazi kubwa ya kukopesha wanafunzi,
kutoa huduma ya afya, kujenga barabara kusambaza umeme bila kusahau hata
majanga yakitokea, inayofanya kazi ni Serikali na hivyo katika miaka
mitano inastahili kuchoka.
Alisema kwa upande wa kambi ya rasmi ya upinzani, hawawezi kuchoka kwa
kuwa kazi yao kila mara ni kusema neno lenye tarakimu sita la ‘Hapana’,
hata katika masuala ya maendeleo.
Alitoa mfano wa suala la ujenzi wa barabara ya kwenda Jimbo la Hai,
ambalo mbunge wake ni Kiongozi wa Kambi ya Upinzani Bungeni, Freeman
Mbowe (Chadema), kuwa badala ya kusaidia ujenzi, kazi yao ilikuwa kusema
‘Hapana’.
Alifananisha uchovu wa Serikali na gari la Mbowe alilosema kuwa
likitembea kilometa nyingi, siku zote atalipeleka kwa mafundi lipate
huduma ya marekebisho na kuendelea na safari, na hivyo hivyo baada ya
miaka mitano, kutafanyika uchaguzi na CCM itaendelea kuongoza.
Lusinde aliitaka Kambi Rasmi ya Upinzani, kuzungumzia suala la uchovu
kwa nidhamu kwa kuwa ikitafsiriwa vingine itawahusu baadhi ya viongozi
wao wanaoendesha vyama hivyo wakati wamechoka.
“Mzee Mtei (Edwin, ambaye ni muasisi wa Chadema) kachoka lakini ndiye
anayeongoza chama… Dk Slaa (Willibrod, Katibu Mkuu wa Chadema) naye
kachoka mbona mnamtegemea kwa urais huku mkimkataa Profesa (Ibrahim
Lipumba)…? Ikulu si wodi ya wagonjwa,” alisema Lusinde.
Lusinde alifananisha Serikali na timu ya mpira iliyoshinda, ambayo
alisema lazima ichoke kwa kazi kubwa, tofauti na timu iliyopata sifuri.
Kuhusu madai ya Kambi Rasmi ya Upinzani kuwa Uchaguzi Mkuu ukisogezwa
mbele moto utalipuka, Lusinde alisema Serikali itaweka tarehe yake ya
uchaguzi lakini na Mungu pia anayo tarehe yake.
“Hamkumbuki 2005 uchaguzi ulisogezwa mbele baada ya mgombea mwenza wa
Chadema kufariki? Ipo tarehe yetu na ya Mungu pia ipo msitishe
wananchi,” alisema Lusinde.
Kisa cha Mfalme
Akizungumzia msuguano wa maneno kati ya Kambi Rasmi ya Upinzani na
wabunge wa CCM, Lusinde alitoa mfano wa nchi moja ya kifalme, ambayo
Mfalme alimuita Waziri Mkuu na Kiongozi wa Upinzani, baada ya kuona
wanalumbana sana.
Katika mazungumzo yao, Lusinde alisema Mfalme alimwambia Kiongozi wa Upinzani aombe suala moja apewe na mwenzako atapewa viwili.
Kwa mujibu wa Lusinde, Kiongozi wa Upinzani aliomba wiki nzima ya
kutafakari na muda wote badala ya kutafakari anachotaka kupewa na
Mfalme, alitafakari kwa nini mwenzake apewe viwili na yeye kimoja.
Baada ya kumalizika kwa wiki hiyo, Kiongozi huyo wa Upinzani kwa mujibu
wa Lusinde, alikwenda kwa Mfalme na kumuomba amng’oe jicho ili Waziri
Mkuu, ang’olewe macho yote mawili, kwa jinsi mpinzani huyo alivyokuwa na
roho mbaya.
Kutokana na kisa hicho, Lusinde aliwasihi Watanzania wasijaribu kuonja
sumu katika Uchaguzi Mkuu ujao na kufafanua kuwa mara zote CCM imekuwa
ikishindana na wagombea wa vyama Chadema na vingine, lakini leo kuna
chama hata hakijasajiliwa kinaitwa ‘ukawa’ (Ukawa, Umoja wa Katiba ya
Wananchi).
Naye Mbunge wa Sikonge, Said Mkumba (CCM), alisema ukiona watu
wanaungana katika vita, ujue ni dhaifu na hilo ndilo linaloonekana
katika Kambi Rasmi ya Upinzani, ambayo inajaribu kuunganisha nguvu ili
kushindana na CCM.
Alisema Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) hauwezi kwenda Ikulu wakati
viongozi wake hawajui mafanikio yaliyopatikana tangu Uhuru.
“Huwezi kushinda kwenda Ikulu, bila kushinda katika serikali za mitaa,”
alisema na kuongeza kuwa wanasiasa wa upinzani wanatoa kejeli lakini
wakikua wataacha hayo maneno.
Mbio za makatibu wakuu: “Mchukue Katibu Mkuu wa Chadema, CUF na CCM wape
wakimbie kilometa tano, nani atakuwa amechoka, mnazungumza huku
mkijitukana wenyewe,” alisema.
Baada ya tamko hilo, Spika wa Bunge, Anne Makinda, aliongeza “Kama
mngeendelea kuwepo, tungeanzisha mbio za vigogo tuone nani mchovu.”
Wakijibu hoja hizo, Mbunge wa Iringa Mjini, Mchungaji Peter Msigwa,
alisema uchovu unaozungumzwa si wa mwili bali wa akili na wa kufikiri.
Alisema dalili za kuchoka ni hatua ya Taifa katika mwaka mmoja kufanya
mambo makubwa kuliko uwezo wake, vikiwemo Uchaguzi Mkuu, Katiba Mpya na
utoaji wa Vitambulisho vya Taifa.
Naye Mbunge wa Viti Maalumu, Conchesta Rwamlaza (Chadema) alisema wakati
mwaka uliopita Serikali ilitenga bajeti ya maendeleo Sh bilioni 660,
mpaka leo ni bilioni 160 tu zilizotolewa.
“Tukisema Serikali imechoka, usikate tama badala yake ipelekeni ikafanyiwe ‘massage’ ili uchovu utoke,” alisema Rwamlaza.
Naye Mbunge wa Viti Maalumu, Pauline Gekul, alifafanua kuwa uchovu wa
Serikali si sawa na wa afya, kwa kuwa mtu anaweza kukosa afya lakini
akawa na busara nzuri au akawa mlemavu lakini ana upeo mzuri.
“Uchovu wa Serikali ni namna inavyokosa vipaumbele na namna
mnavyoshindwa kutekeleza mipango. Kwa hiyo wanaosema tufanye riadha
hawaelewi kwa nini tunasema Serikali imechoka,” alisema.
Aliwataka wabunge wa CCM wasibeze Ukawa, kwa kuwa Watanzania wanahitaji
mabadiliko ya kweli na wanajua Ukawa ndio suluhisho la matatizo yao.
RC SERUKAMBA AIUNGA MKONO REA UGAWAJI MITUNGI YA GESI 9800 IRINGA
-
REA yahamasisha ujenzi wa vituo vidogo vya mafuta maeneo ya vijijini
Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Mhe. Peter Serukamba ameunga mkono juhudi za Wakala
wa Nish...
25 minutes ago
No comments:
Post a Comment