Pages

Friday, May 15, 2015

Vijembe Vya Kisiasa Vyatawala Bungeni......Lusinde Asema Dr Slaa Hafai Kuwa Rais Maana Ikulu Sio Wodi Ya Wagonjwa

VIJEMBE vya kisiasa jana vilichukua sehemu kubwa ya mjadala wa Bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu unaoendelea, ambapo mvutano mkubwa ulikuwa kati ya Serikali na vyama vya upinzani nani amechoka.

Akizungumza bungeni kwa vijembe, Mbunge wa Mtera, Livingstone Lusinde (CCM), alisema hoja ya kambi rasmi ya upinzani kuwa Serikali imechoka, inawezekana ni kweli ila haikuwekwa vizuri.



Alifafanua kuwa Serikali imefanya kazi kubwa ya kukopesha wanafunzi, kutoa huduma ya afya, kujenga barabara kusambaza umeme bila kusahau hata majanga yakitokea, inayofanya kazi ni Serikali na hivyo katika miaka mitano inastahili kuchoka.

Alisema kwa upande wa kambi ya rasmi ya upinzani, hawawezi kuchoka kwa kuwa kazi yao kila mara ni kusema neno lenye tarakimu sita la ‘Hapana’, hata katika masuala ya maendeleo.

Alitoa mfano wa suala la ujenzi wa barabara ya kwenda Jimbo la Hai, ambalo mbunge wake ni Kiongozi wa Kambi ya Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe (Chadema), kuwa badala ya kusaidia ujenzi, kazi yao ilikuwa kusema ‘Hapana’.

Alifananisha uchovu wa Serikali na gari la Mbowe alilosema kuwa likitembea kilometa nyingi, siku zote atalipeleka kwa mafundi lipate huduma ya marekebisho na kuendelea na safari, na hivyo hivyo baada ya miaka mitano, kutafanyika uchaguzi na CCM itaendelea kuongoza.

Lusinde aliitaka Kambi Rasmi ya Upinzani, kuzungumzia suala la uchovu kwa nidhamu kwa kuwa ikitafsiriwa vingine itawahusu baadhi ya viongozi wao wanaoendesha vyama hivyo wakati wamechoka.

“Mzee Mtei (Edwin, ambaye ni muasisi wa Chadema) kachoka lakini ndiye anayeongoza chama… Dk Slaa (Willibrod, Katibu Mkuu wa Chadema) naye kachoka mbona mnamtegemea kwa urais huku mkimkataa Profesa (Ibrahim Lipumba)…? Ikulu si wodi ya wagonjwa,” alisema Lusinde.

Lusinde alifananisha Serikali na timu ya mpira iliyoshinda, ambayo alisema lazima ichoke kwa kazi kubwa, tofauti na timu iliyopata sifuri.

Kuhusu madai ya Kambi Rasmi ya Upinzani kuwa Uchaguzi Mkuu ukisogezwa mbele moto utalipuka, Lusinde alisema Serikali itaweka tarehe yake ya uchaguzi lakini na Mungu pia anayo tarehe yake.

“Hamkumbuki 2005 uchaguzi ulisogezwa mbele baada ya mgombea mwenza wa Chadema kufariki? Ipo tarehe yetu na ya Mungu pia ipo msitishe wananchi,” alisema Lusinde.

Kisa cha Mfalme
Akizungumzia msuguano wa maneno kati ya Kambi Rasmi ya Upinzani na wabunge wa CCM, Lusinde alitoa mfano wa nchi moja ya kifalme, ambayo Mfalme alimuita Waziri Mkuu na Kiongozi wa Upinzani, baada ya kuona wanalumbana sana.

Katika mazungumzo yao, Lusinde alisema Mfalme alimwambia Kiongozi wa Upinzani aombe suala moja apewe na mwenzako atapewa viwili.

Kwa mujibu wa Lusinde, Kiongozi wa Upinzani aliomba wiki nzima ya kutafakari na muda wote badala ya kutafakari anachotaka kupewa na Mfalme, alitafakari kwa nini mwenzake apewe viwili na yeye kimoja.

Baada ya kumalizika kwa wiki hiyo, Kiongozi huyo wa Upinzani kwa mujibu wa Lusinde, alikwenda kwa Mfalme na kumuomba amng’oe jicho ili Waziri Mkuu, ang’olewe macho yote mawili, kwa jinsi mpinzani huyo alivyokuwa na roho mbaya.

Kutokana na kisa hicho, Lusinde aliwasihi Watanzania wasijaribu kuonja sumu katika Uchaguzi Mkuu ujao na kufafanua kuwa mara zote CCM imekuwa ikishindana na wagombea wa vyama Chadema na vingine, lakini leo kuna chama hata hakijasajiliwa kinaitwa ‘ukawa’ (Ukawa, Umoja wa Katiba ya Wananchi).

Naye Mbunge wa Sikonge, Said Mkumba (CCM), alisema ukiona watu wanaungana katika vita, ujue ni dhaifu na hilo ndilo linaloonekana katika Kambi Rasmi ya Upinzani, ambayo inajaribu kuunganisha nguvu ili kushindana na CCM.

Alisema Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) hauwezi kwenda Ikulu wakati viongozi wake hawajui mafanikio yaliyopatikana tangu Uhuru.

“Huwezi kushinda kwenda Ikulu, bila kushinda katika serikali za mitaa,” alisema na kuongeza kuwa wanasiasa wa upinzani wanatoa kejeli lakini wakikua wataacha hayo maneno.

Mbio za makatibu wakuu: “Mchukue Katibu Mkuu wa Chadema, CUF na CCM wape wakimbie kilometa tano, nani atakuwa amechoka, mnazungumza huku mkijitukana wenyewe,” alisema.

Baada ya tamko hilo, Spika wa Bunge, Anne Makinda, aliongeza “Kama mngeendelea kuwepo, tungeanzisha mbio za vigogo tuone nani mchovu.”

Wakijibu hoja hizo, Mbunge wa Iringa Mjini, Mchungaji Peter Msigwa, alisema uchovu unaozungumzwa si wa mwili bali wa akili na wa kufikiri.

Alisema dalili za kuchoka ni hatua ya Taifa katika mwaka mmoja kufanya mambo makubwa kuliko uwezo wake, vikiwemo Uchaguzi Mkuu, Katiba Mpya na utoaji wa Vitambulisho vya Taifa.

Naye Mbunge wa Viti Maalumu, Conchesta Rwamlaza (Chadema) alisema wakati mwaka uliopita Serikali ilitenga bajeti ya maendeleo Sh bilioni 660, mpaka leo ni bilioni 160 tu zilizotolewa.

“Tukisema Serikali imechoka, usikate tama badala yake ipelekeni ikafanyiwe ‘massage’ ili uchovu utoke,” alisema Rwamlaza.

Naye Mbunge wa Viti Maalumu, Pauline Gekul, alifafanua kuwa uchovu wa Serikali si sawa na wa afya, kwa kuwa mtu anaweza kukosa afya lakini akawa na busara nzuri au akawa mlemavu lakini ana upeo mzuri.

“Uchovu wa Serikali ni namna inavyokosa vipaumbele na namna mnavyoshindwa kutekeleza mipango. Kwa hiyo wanaosema tufanye riadha hawaelewi kwa nini tunasema Serikali imechoka,” alisema.

Aliwataka wabunge wa CCM wasibeze Ukawa, kwa kuwa Watanzania wanahitaji mabadiliko ya kweli na wanajua Ukawa ndio suluhisho la matatizo yao.

No comments:

Post a Comment