WAKATI
vuguvugu la kusaka mgombea urais ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM)
likishika kasi, Katibu Mkuu wa Chadema, Dk. Willibrod Slaa, ameondoka
kwenda barani Ulaya kusaka ubani wa urais kwa muda wa siku nane.
Dk.
Slaa ambaye amekuwa akitajwa kuwa anaweza kuteuliwa na Umoja wa Katiba
ya Wananchi (Ukawa) kugombea urais Oktoba mwaka huu kutokana na rekodi
yake, anafanya ziara hii ikiwa ni ya pili baada ya ziara ndefu
aliyoifanya hivi karibu nchini Marekani.
Taarifa
iliyotolewa kwa vyombo vya habari jijini Dar es Salaam jana na Mkuu wa
Idara ya Mambo ya Nje na Uhusiano wa Kimataifa,Deogratias Munishi,
ilisema Dk. Slaa ataanzia nchini Uholanzi ambako atakutana na viongozi
wa Jumuiya ya Ulaya (EU) ambapo watazungumzia mambo mbalimbali yakiwamo
ya kisiasa.
“Akiwa
Uholanzi anatarajiwa kukutana na kufanya mazungumzo na viongozi
mbalimbali wa nchi za Jumuiya ya Ulaya (EU), atakutana na jopo la
wataalamu wa masuala ya uchumi kwa lengo la kubadilishana uzoefu katika
kupata mifumo sahihi na kujenga taasisi za kusaidia uwajibikaji.
“Pia
tunaamini mazungumzo haya yatajikita zaidi kutoa mwelekeo wa kusukuma
maendeleo ya watu katika nchi za Afrika, hususan zenye rasilimali nyingi
kama Tanzania ili kuziepusha na kile ambacho kimezikumba nchi nyingi
duniani,” ilisema taarifa hiyo.
Taarifa hiyo, ilisema Dk. Slaa pia atajadiliana kuhusu hali ya demokrasia, utawala bora na ukuzaji wa haki za binadamu.
Ilisema
Dk. Slaa ameambatana na Mkurugenzi wa Bunge na Halmashauri, John Mrema
na Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano, Tumaini Makene.
Kabla
ya ziara hiyo, Dk. Slaa ametoka kufanya ziara ya kikazi katika mikoa ya
Kagera, Mbeya, Rukwa na Katavi akikagua uandikishaji wapigakura kwenye
Daftari la Kudumu la Wapigakura kwa mfumo wa BVR huku pia akiwahamasisha
Watanzania wote wenye sifa za kupiga kura kuhakikisha wamejiandikisha.
No comments:
Post a Comment