Mkuu wa Kambi ya Wakimbizi Nyarugusu iliyopo wilayani Kasulu, mkoani Kigoma, Sospeter Christopher Boyo (aliyesimama mwenye shati la kitenge) akisoma taarifa fupi ya Kambi ya Nyarugusu kwa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mh. Mathias Chikawe (aliyeketi mwenye suti ya kijivu) aliyeambatana na Mratibu Mkazi wa Mashirika ya Umoja wa Mataifa na Mwakilishi wa Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP), Alvaro Rodriguez mara baada ya kuwasili kwenye kambi hiyo kujionea hali halisi ya mazingira na changamoto zinazowakabili Waomba hifadhi wa Burundi na Kongo. (Picha zote na Zainul Mzige wa modewjiblog)
WAKATI dunia kupitia Mashirika ya Umoja wa Mataifa yanahangika kutanzua changamoto za wakimbizi Nyarugusu, mkoani Kigoma imeelezwa kuwa idadi kubwa ya Wakimbizi waliorejeshwa nchini Burundi kutoka kambi ya Mtabila iliyoko Kigoma iliyofungwa rasmi Desemba, 2012 wameingia tena nchini na kujazana katika makazi ya muda ya Nyarugusu wakiomba hifadhi.
Kauli hiyo imetolewa na Mkuu wa Kambi ya Nyarugusu Sospter Christopher wakati akizungumza na Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi aliyekwenda kuangalia hali halisi ya kambi ya Nyarugusu na Wakimbizi akiambatana na Maofisa wa Umoja wa Mataifa akiwemo Mratibu wa Mashirika hayo nchini Alvaro Rodriguez.
Kurejea kwa wingi kwa Wakimbizi hao ni pigo kisaikolojia kwa watu ambao walirejeshwa nyumbani kwa kuonekana kwamba hali ni shwari na walikuwa wameanza kuishi maisha ya kawaida.
Mkuu huyo wa kambi alisema idadi hiyo ikichanganyika na wengine imafanya kambi kuhemewa na kuonekana haja ya kutafuta eneo jingine la kupiga kambi kwa ajili ya Wakimbizi hao ambao mpaka mwishoni mwa wiki iliyopita walikuwa zaidi ya elfu 51.
“ Kwa sababu tunapokea idadi kubwa ya waomba hifadhi toka Burundi, tumekuwa tukiongeza idadi ya vituo vya mapokezi ili kukidhi mahitaji ya kuwapokea wakati tukisubiri maelekezo toka ngazi za juu za kuwahamishia Migunga Hills eneo linalopendekezwa kufunguliwa kambi ya Nyarugusu B” alisema Christopher mbele ya Waziri Chikawe.
Alisema walianza kupokea waomba hifadhi hapo kambini kuanzia Aprili 29, 2015 kwa idadi ndogo kabisa ya watu 36, lakini idadi hiyo ilianza kuongezeka siku hadi siku na kufikia Mei 27 mwaka huu idadi yao ilifikia 48,333, idadi kubwa ikiwa wanawake na watoto.
Wakimbizi hao walikuwa wakipitia vituo vya Kigoma (27,638), Manyovu (4,439), Kilelema (1,603) na Kigadye (1,291).
Kambi hiyo yenye uwezo wa kubeba watu 50,000 imeelemewa kwa sababu ya ujio mpya uliosababisha kuwepo kwa Wakimbizi zaidi ya 106,410.
Kuna matatizo zaidi ya milipuko ya wagonjwa kambi hii imechanganywa na Wakimbizi wa Kongo watu ambao hawana utamaduni wa pamoja na kuonekana hatari ya kukabiliana kwa kutosikilizana.
Aidha kambi hiyo pamoja na kuwahifadhi waburundi wapo pia Wakimbizi kutoka Kongo wapatao 54,706; Burundi,3261 ; Rwanda 72; Uganda 17; Sudan Kusini wanane; Kenya 7; Somalia 3; Ethiopia 1; Zimbabwe 1; na Ivory coast 1.
Mkurugenzi wa Idara ya huduma za Wakimbizi wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Harrison Mseke (wa pili kushoto) akizungumza jambo na Mratibu Mkazi wa Mashirika ya Umoja wa Mataifa na Mwakilishi wa Shirika la Maendeleo (UNDP), Alvaro Rodriguez (kushoto) huku Mkuu wa kambi mpya inayotarajiwa kuanzishwa ya Nyarugusu B, Fredrick Nisajile (wa nne kulia) akitoa maelezo kwa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mh. Mathias Chikawe (wa tatu kushoto) mara tu baada ya kuwasili na kusomewa taarifa kwenye kambi ya Nyarugusu wilayani Kasulu mkoani Kigoma. Wengine pichani ni baadhi ya viongozi wa ulinzi na usalama wa wilaya ya Kasulu mkoani Kigoma.
Akijibu maswali ya waandishi wa habari walioambatana naye katika ziara hiyo kuhusu hali ya baadae ya Wakimbizi wa Kongo ambao wapo nchini kwa takribani miaka 19 sasa, Waziri Chikawe alisema kwamba serikali haina mpango wa kuwapa uraia kwa sasa ingawa Marekani imesema itawachukua Wakimbizi elfu 30 kuwapeleka kwao na kwingine duniani.
“hatuna mpango wa kuwapa uraia kwa sasa…” alisema Chikawe na kusema kwamba kwa kuondolewa kwa hao wengine kutasaidia kupunguza idadi yao katika kambi hiyo.
Alisema kwamba ni lengo la serikali kuhakikisha kwamba kambi hiyo inapunguzwa ili kuweza kuchangia ipasavyo kwa hali bora ya Wakimbizi na kwamba mchakato wa kuwaangalia waomba hifadhi kama wanafaa kuwa Wakimbizi unaendelea.
Akizungumzia malalamiko ya upatikanaji wa chakula, Waziri Chikawe alisema kwamba si kweli kuwa kuna watu hawajapata chakula kwa siku saba la sivyo wangelikufa.
Alisema wengi wa Wakimbizi ni watoto na kwamba wanapoingia nchini wanapewa vyakula vikavu (kama biskuti) lakini wakishafika kambini wanapewa chakula kilichopikwa na resheni ya siku 14 .
Alisisitiza kuwa kama kungelikuwa hakuna chakula watoto hao wasingeishi, labda kama wanataka kuongezewa chakula zaidi.
Kuhusu ujenzi wa kambi mpya Migunga alisema kwamba wataalamu wanaangalia barabara mbadala kwani iliyopo sasa pamoja na kuhitajika milioni 300 kuitengeneza lakini bado kila mvua itakapokuwa inanyesha itahitaji kutengenezwa.
Naye Mwakilishi wa Shirika la Umoja wa Mtaifa la Kuhudumia Wakimbizi (UNHCR), Joyce Mends-Cole katika mahojiano na waandishi wa habari aliishukuru serikali ya Tanzania kwa kufungua mipaka ili Wakimbizi waweze kuingia na kutoa eneo kwa ajili ya kambi mpya kutokana na ya sasa kujaa sana.
Aidha aliishukuru serikali ya Uingereza kwa kuwa ya kwanza kutoa misaada kwa ajili ya Wakimbizi hao na kutarajia nchi nyingine kama Marekani itafanya hivyo mapema ili kuisaidia serikali ya Tanzania katika kuhudumia waomba hifadhi.
Naye Mratibu wa Mashirika ya Umoja wa Mataifa nchini, Alvaro Rodriguez amesema wanafanya kila linalowezekana ili kupunguza idadi ya Wakimbizi katika kambi ya Nyarugusu kwa kuwapatia eneo jingine la kujihifadhi.
Alisema kwa kuwatoa hapo watasaidia shule zilizofungwa ambazo zinasomesha watoto kutoka kwa Wakimbizi wa Kongo kurejea madarasani kukamilisha mtaala wao.
Mkuu wa kambi mpya inayotarajiwa kuanzishwa ya Nyarugusu B, Fredrick Nisajile akifafanua jambo kwa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mh. Mathias Chikawe wakati akitembelea na kukagua maeneo mbalimbali ya Kambi ya Nyarugusu iliyopo wilayani Kasulu, mkoani Kigoma.
Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mh. Mathias Chikawe na Mratibu Mkazi wa Mashirika ya Umoja wa Mataifa, Mwakilishi wa Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP), Alvaro Rodriguez pamoja na Mwakilishi wa Shirika la Umoja wa Mtaifa la Kuhudumia Wakimbizi (UNHCR), Joyce Mends-Cole wakikagua sehemu wanayolala Waomba hifadhi wanaoendelea kuwasili katika kambi ya Nyarugusu ambayo inaelemewa kutokana na wingi wa Waomba hifadhi hao wanaoendelea kumiminika mjini Kigoma.
Muonekano wa moja ya chumba cha kulala familia za waomba hifadhi katika kambi ya Nyarugusu ambapo kifika muda wa kulala wanatandika mkeka chini katika vumbi hilo jekundu na kupata usingizi.
Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mh. Mathias Chikawe (mwenye suti ya kijivu), Mratibu Mkazi wa Mashirika ya Umoja wa Mataifa na Mwakilishi wa Shirika la Maendeleo (UNDP), Alvaro Rodriguez (wa pili kushoto) pamoja na Mwakilishi wa Shirika la Umoja wa Mtaifa la Kuhudumia Wakimbizi (UNHCR), Joyce Mends-Cole (kushoto) wakisikiliza hoja mbalimbali kutoka kwa Waomba hifadhi wanaohifadhiwa kwenye kambi ya Wakimbizi Nyarugusu iliyopo wilaya ya Kasulu mkoani Kigoma walipotembelea kambi hiyo kukagua kambi hiyo na kuangalia changamoto mbalimbali zinazowakabili na namna ya kuzitatua.
Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mh. Mathias Chikawe (mwenye suti ya kijivu) akiteta jambo na Mratibu Mkazi wa Mashirika ya Umoja wa Mataifa na Mwakilishi wa Shirika la Maendeleo (UNDP), Alvaro Rodriguez wakati walipotembelea kambi ya Wakimbizi ya Nyarugusu iliyopo wilaya ya Kasulu mkoani Kigoma mwishoni mwa juma lililopita.
Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mh. Mathias Chikawe akigawa vifaa vya matumizi ya nyumbani ambavyo ni Blangeti, Mkeka, Kontena la kuhifadhi chakula na dumu la maji la lita 10 kwa mmoja wa Waomba hifadhi waliowasili siku ya ziara ya kutembelea kambi ya Nyarugusu mwishoni mwa juma wilayani Kasulu mkoani Kigoma. Anayeshuhudia tukio hilo ni Mratibu Mkazi wa Mashirika ya Umoja wa Mataifa na Mwakilishi wa Shirika la Maendeleo (UNDP), Alvaro Rodriguez (mwenye shati jeupe).Kulia ni Mkuu wa kambi mpya inayotarajiwa kuanzishwa ya Nyarugusu B, Fredrick Nisajile.
Waomba hifadhi na familia zoa wakiwa katika foleni ya kupokea vifaa hivyo.
Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mh. Mathias Chikawe akizungumza na Waomba hifadhi katika kambi ya Nyarugusu wakati alipofanya ziara ya kutembelea eneo hilo akiwa ameambatana na Mkuu wa Mashirika ya Umoja wa Mataifa pamoja na Mwakilishi wa shirika la kuhudumia Wakimbizi nchini (UNHCR).
Mtaalam wa Mahusiano na Mawasiliano wa Shirika la Umoja wa Mataifa (UN) Tanzania, Hoyce Temu akizungumza na mmoja wa wakinamama anayeishi kwenye kambi ya Wakimbizi Nyarugusu wakati wa ziara maalum ya kutembelea maeneo hayo iliyohusisha Serikali ya Tanzania na Umoja wa Mataifa.
Mratibu Mkazi wa Mashirika ya Umoja wa Mataifa na Mwakilishi wa Shirika la Maendeleo (UNDP), Alvaro Rodriguez na Mtaalam wa Mahusiano na Mawasiliano wa Shirika la Umoja wa Mataifa (UN) Tanzania, Hoyce Temu wakibadilishana mawazo na mmoja wa wafanyakazi wa Shirika la Kimataifa Ia Uhamiaji (I.O.M) (katikati) ambaye jina lake halikuweza kupatikana kiurahisi katika kambi ya Wakimbizi ya Nyarugusu iliyopo wilayani Kasulu mkoani Kigoma.
Mkurugenzi wa Idara ya huduma za Wakimbizi wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Harrison Mseke (mwenye suti ya kijivu) akifafanua jambo kwa Mh. Mathias Chikawe alipotembela katika chumba maalum kichotumika kufanya usajili kwa Waomba hifadhi na familia zao kwa ajili ya kupewa hati ya kuwa Wakimbizi kamili kama watatimiza vigezo vinavyohitajika. Aliyeketi kulia ni Msajili wa Waomba hifadhi, Ndalo Charles Bogohe.
Zoezi la usajili likiendelea kwa familia za waomba hifadhi katika kambi ya Nyarugusu iliyopo wilayani Kasulu mkoani Kigoma.
Wakinamama wakiandaa chakula cha mchana kwa familia zao kama walivyokutwa na kamera ya modewjiblog.
Sehemu ya familia za Waomba hifadhi katika kambi ya Wakimbizi Nyarugusu, wilayani Kasulu, mkoani Geita wakiendelea kujipanga baada ya kuwasili kwenye eneo hilo.
Moja ya familia za waomba hifadhi ikiwa imejipumzisha mara baada ya chakula cha mchana huku nyuso zao zikionekana kuwa na furaha na matumaini mapya.
Hili ni eneo ambalo Waomba hifadhi kutoka nchini Burundi wa kambi ya Nyarugusu wakiteka maji safi kwa matumizi yao.
Mkurugenzi wa Idara ya huduma za Wakimbizi wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Harrison Mseke (kushoto) akizungumza jambo na Mratibu Mkazi wa Mashirika ya Umoja wa Mataifa na Mwakilishi wa Shirika la Maendeleo (UNDP), Alvaro Rodriguez (wa pili kushoto) wakati wakielekea kukagua vyumba vya madarasa katika shule ya msingi Mapendo ambayo yamegeuzwa kuwa nyumba za kulala Waomba hifadhi, kutokana na uhaba wa makazi ya kuishi kwenye maeneo ya kambi ya Nyarugusu, wilayani Kasulu mkoani Kigoma. Wengine pichani ni baadhi ya viongozi wa ulinzi na usalama wa wilaya ya Kasulu mkoani Kigoma katika msafara huo.
Baadhi ya Waomba hifadhi katika kambi ya Wakimbizi Nyarugusu wakiwa wamempumzika huku wengine wakipata chakula cha mchana kama walivyokutwa na kamera ya modewjiblog.
Kinababa nao hushiriki kuandaa chakula cha mchana kwa familia zao kama huyu aliyekutwa na kamera ya modewjiblog.
Eneo la shule ya msingi Mapendo katika kambi ya Wakimbizi Nyarugusu ambalo kwa sasa linatumika kuhifadhi Waomba hifadhi wanaoendelea kuwasili nchini wakitokea Burundi kupitia mji wa Kigoma.
Madawati ya wanafunzi katika shule ya msingi Mapendo yakiwa nje ya madarasa yakitumika kuanikiwa nguo na huku wakati wa msimu wa mvua yakinyeshewa.
Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mh. Mathias Chikawe na Mratibu Mkazi wa Mashirika ya Umoja wa Mataifa na Mwakilishi wa Shirika la Maendeleo (UNDP), Alvaro Rodriguez wakibadilishana mawazo na wasimizi wa kambi hizo za Nyarugusu wakati wa ziara ya siku moja wilayani Kasulu, mkoani Kigoma.
Mratibu Mkazi wa Mashirika ya Umoja wa Mataifa na Mwakilishi wa Shirika la Maendeleo (UNDP), Alvaro Rodriguez (kushoto) akiwa ameambatana na Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mh. Mathias Chikawe wakikagua eneo jipya litakaloitwa Nyarugusu B lililotolewa na serikali kwa ajili ya Waomba hifadhi wanaoendelea kumiminika mjini Kigoma ambalo liko mbioni kutengenezwa na kukamilika ndani ya miezi 3 ijayo.
Eneo jipya la kambi ya Nyarugusu B ambalo limetengwa na serikali ya Jamhuri ya Tanzania kwa ajili ya makazi ya Waomba hifadhi wanataotenganishwa Burundi na Congo mara tu baada ya kukamilika.
Muonekano wa eneo jingine la makazi ya Waombahifadhi ndani ya kambi ya Wakimbizi Nyarugusu iliyopo wilayani Kasulu, mkoani Kigoma.
Amani na upendo itawale kati yetu......ndivyo wanavyosema kwa pamoja baadhi ya watoto waomba hifadhi wakifurahia picha pamoja na Mratibu Mkazi wa Mashirika ya Umoja wa Mataifa na Mwakilishi wa Shirika la Maendeleo (UNDP), Alvaro Rodriguez.
No comments:
Post a Comment