Uwanja wa Azam ambao ndiyo wa kisasa baada ya ule wa Taifa,
Dar es Salaam ulijengwa kwa Sh 2 bilioni za Kitanzania hadi kuanza kutumika kwa
mechi za Ligi Kuu Bara.
Lakini katika hali ya kushangaza Straika wa Taifa Stars,
Mbwana Samatta amegomea kiasi kama hicho cha fedha kujiunga na Zamalek ya
Misri.
Katika kuonyesha jeuri zaidi, Samatta amesema pia hataongeza
mkataba na klabu yake ya TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, hata
kama bosi wa timu hiyo Moise Katumbi atampa dau la maana kwa kuwa ndoto zake si
kuendelea kucheza Afrika.
Samatta alisema ndoto zake kwa sasa ni kucheza soka la
kulipwa Barani Ulaya na hawezi kuongeza mkataba wa kuichezea Mazembe, huku pia
akikiri kuligomea dili la Zamalek ambalo lingempa Sh 2 bilioni.
Nyota huyo wa zamani wa Simba alikiri kuwa jitihada zake za
kutimkia Ulaya mwaka huu tayari zimegonga mwamba, lakini hajakata tamaa na
hataongeza mkataba Mazembe ili kujiongezea nafasi ya kujiunga na klabu za
Ulaya.
“Dirisha limefungwa tayari kwa sasa, ila sijakata tamaa,
nasubiri tena dirisha lijalo, mkataba wangu pia utakuwa unamalizika hivyo
nitakuwa na nafasi kubwa zaidi,” alisema Samatta
“Kuhusu kuongeza mkataba Mazembe hapana, sina mpango huo,
sina ndoto za kucheza tena Afrika na ndiyo sababu nilikataa dili la Zamalek
hivi majuzi, sikupenda kujiunga nayo maana siyo ndoto yangu,” aliongeza.
Chanzo:Mwanaspoti
No comments:
Post a Comment