Pages

Wednesday, February 17, 2016

AMERI GROUP YA DUBAI KUZALISHA MEGAWATI 600 ZA UMEME

Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo( kulia) akipata maelezo kutoka kwa Makamu wa Rais Mwandamizi wa kampuni ya PW Power Systems Charles Levey,( kushoto) ambayo ni wakandarasi wa ujenzi wa mradi wa kuzalisha megawati mia 600 za umeme wa gesi asilia iliyogundulika nchini ambao Kampuni ya Ameri Group ya nchini Dubai imeyonesha nia ya kuwekeza.( wa pili kulia ni Mkurugenzi Mkuu wa kampuni ya Ameri Group ya Dubai.
Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo,akiwa kwenye mkutano na watendani wa Wizara ya Nishati na Madini pamoja na ujumbe wa kampuni ya Ameri Group kutoka Dubai walionesha nia ya kuzalisha megawati 600 za umeme wa gesi asilia iliyogunduliwa nchini, katika ukumbi wa mikutano wa Wizara ya Nishati na Madini jijini DSM



 Na Zuena Msuya, Dar Es Salaam.

Kampuni ya Ameri Group yenye makazi yake nchini Dubai imeonyesha nia ya kuwekeza katika sekta ndogo ya gesi asilia kwa kuzalisha umeme wa megawati  600 za umeme unaotokana na nishati hiyo iliyogundulika nchini.

Hayo yalibainishwa  jijini Dar Es Salaam wakati wa Mkutano kati ya Waziri wa Nishati na Madini Profesa Sospeter Muhongo na  ujumbe wa Kampuni hiyo ukiongozwa na Mkurugenzi Mkuu wa Ameri Group, Ziad Barakat aliyeambatana na Mkandarasi atakayetekeleza mradi huo na kampuni itakayofunga mashine za kufua umeme.

Barakat alisema Kampuni hiyo inatarajia kuzalisha umeme wa megawati 600 unaotokana na gesi asilia ambapo katika awamu ya kwanza wataanza na megawati 300.

Kwa upande wake Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo aliitaka kampuni hiyo kukaa pamoja na Shirika la Umeme nchini (TANESCO), Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania ( TPDC) pamoja na Mamlaka ya Udhibiti wa Nishati na Maji( EWURA) ili kuona namna ambavyo kampuni hiyo itatekeleza mradi huo.

 Aidha, Prof. Muhongo alizitaka Taasisi hizo kujadiliana kwa kina kuhusu masuala ya bei ya umeme ambayo kampuni hiyo itaiuzia TANESCO pamoja na masuala mengine ili wafikie muafaka kabla ya kuanza kwa utekelezaji wa mradi.


Pamoja na mambo mengine, Prof. Muhongo alisema mara baada ya kampuni hiyo kujadiliana na TANESCO, EWURA pamoja na TPDC na kufikia makubalino; Serikali itaelekeza eneo ambalo kampuni hiyo itafua umeme wa gesi katika maeneo ambayo gesi asilia imegunduliwa kama ni Mtwara, Lindi, au Somangafungu.

No comments:

Post a Comment