Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (Nec), Jaji Damian
Lubuva amewataka wanasiasa walioshindwa kwenye Uchaguzi Mkuu waache kujitangaza
kuwa walishinda, akisema wanapotosha wananchi.
Kauli hiyo ya Jaji Lubuva imekuja siku chache baada ya
aliyekuwa mgombea urais kwa tiketi ya Chadema, Edward Lowassa kudai kuwa kama
si matokeo kuchakachuliwa, alikuwa na nafasi kubwa ya kushinda kwa sababu wananchi
walishaichoka CCM na wakawa wanataka mabadiliko.
Lowassa alisema hayo katika mahojiano maalum na waandishi wa
habari ofisini kwake, akisema yeye na Ukawa walishinda kwa kishindo isipokuwa
matokeo yalivurugwa makusudi ili CCM iendelee kubaki madarakani.
Jana, akiwa kwenye mkutano wa tathmini kati ya NEC na asasi
za kiraia kuhusu utoaji elimu kwa mpigakura uliofanyika Dodoma, Jaji Lubuva
alisema uchaguzi umeshapita na kilichobaki sasa ni kufanya kazi tu.
Bila ya kutaja jina la mwanasiasa huyo, Jaji Lubuva alisema
kama kuna mtu alishindwa katika uchaguzi uliopita, ajipange kwa ajili ya
uchaguzi mkuu ujao mwaka 2020.
“Hata wananchi wanawashangaa kwa kuwa wao ndio walioamua ni
nani anafaa kuwaongoza,” alisema Jaji Lubuva.
Alisema kuwa NEC ilikuwa inapokea matokeo ya uchaguzi kutoka
majimboni na kuyasoma kama yalivyotumwa na katika hilo hakuna wakala hata mmoja
wa chama ambaye aliyapinga matokeo hayo.
“Sasa nashangaa kuna baadhi ya wagombea wanaotaka Tume
ifukuzwe kazi eti tu kwa sababu wao hawakushinda. Naomba ifahamike kwamba
katika kila uchaguzi duniani kuna kushinda na kushindwa.
"Sasa kama kila atakayeshindwa atataka tume ifukuzwe
kazi hapatakuwa na tume ya uchaguzi kwa sababu kila atakayekuwa anashindwa
atakuwa anataka tume ifukuzwe kazi,” alisema Jaji Lubuva.
Chadema, ambayo iliungana na vyama vitatu kuunda Ukawa,
iliitaka NEC kusitisha utangazaji matokeo ikidai kuwa kilichokuwa kikitangazwa
ni tofauti na takwimu walizokusanya kutoka majimboni. Lakini NEC ikaendelea
kutangaza.
Baadaye, Chadema ililalamika ikidai kituo chao cha kukusanya
na kujumlisha matokeo kilivamiwa na polisi na kompyuta kuchukuliwa na hivyo
kuvuruga ufuatiliaji wao wa matokeo.
Kwa upande wake mkurugenzi wa huduma kutoka NEC, Emmanuel
Kavishe alisema kuwa Tume inafanya kazi kwa mujibu wa sheria na Katiba na
kwamba hata siku moja haijawahi kumpendelea au kumuonea mtu yeyote.
Katika uchaguzi wa urais, John Magufuli alipata kura milioni
8.8 huku Lowassa akipata milioni 6.07.
<
No comments:
Post a Comment