Kutokana na Wasichana wengi walio
Mashuleni kulazimika kukosa Masomo yao katika Kipindi cha hedhi, Mwanaharakati
wa Kutetea haki za Wanawake na Wasichana nchini Khadija Liganga, amelazimika
kuanzisha kampeni ya kukusanya pedi 3,000 ndani ya mwezi huu ili kuwasaidia
wahitaji.
Akizungumza jana
katika Kipindi cha Passion Break Fast kinachorushwa na Radio Passion Fm ya
Jijini Mwanza, Liganga alibainisha kwamba ameamua kukusanya pedi hizo kutoka
kwa wadau mbalimbali ili kuziwasilisha katika Shule 10 za Msingi na Sekondari zilizo katika Mikoa ya
Mwanza na Mara hii ikiwa ni maalumu kwa ajili ya wasichana wanafunzi ambao
hawana uwezo wa kumudu kununua pedi hizo.
“Tarehe Moja
mwezi wa Kwanza mwaka huu, wanawake tulikutana Jijini Mwanza chini ya mpango
tuliouita Women Round Table kwa ajili ya kupanga mikakati mbalimbali ya
kimaendeleo kwa mwaka huu 2016. Moja ya mikakati niliyoipanga ni pamoja kuanzisha
mradi uitwao Binti Box ambao umelenga kusaidia uchangiaji na upatikanaji wa
pedi kwa ajili ya wanafunzi wenye uhitaji mashuleni pamoja na kuwapa elimu ya
namna ya kujiweka katika hali ya usafi wawapo katika kipindi cha hedhi”.
Alisema Liganga na kuongeza kuwa mpango huo utakuwa endelevu.
Kumekuwepo
na tatizo la wanafunzi wasichana katika maeneo mbalimbali nchini kukosa masomo
yao katika kipindi cha hedhi huku baadhi yao wakilazimika kuacha shule kutokana
na aibu wanayokumbana nayo wawapo shuleni hii ikiwa ni kutokana na kukosa elimu
ya kutosha pindi waingiapo katika kipindi cha hedhi.
Unaweza kuungana
na mwanaharaki huyo kwa kuchangia pedi ambapo anapatikana kwa nambari 0713 093 801
hiyo ikiwa ni kwa wale walio mbali na Jijini Mwanza ama waweza kutembelea ofisi
za Dida Vitenge Wear zilizopo Nganza Sekondari barabara ya kwenda Chuo Kikuu
cha SAUT jirani na ghorofa upande wa kushoto hapo.
Imeandaliwa na George Binagi-GB Pazzo wa Binagi Media Group
No comments:
Post a Comment