![](https://blogger.googleusercontent.com/img/b/R29vZ2xl/AVvXsEjK-Cy-MABAGjqC4qE5AjVHaBLCger7KYfYbzeLYlvBFbfpGSzSppk1yfodRvkPU2WJwsh7Lk9BQYeNwc5dCldtKLrb4e-3L416J0wuOatHiOFiJ5jhn1LM2_kOiDltmt7ycEicMxgWjbc/s640/Sefue.jpg)
Baada ya kudumu Ikulu kwa takribani siku 127zikiwamo 67
tangu aongezewe muda wa mwaka moja akiwa na Serikali ya Awamu ya Tano, Balozi
Ombeni Sefue ameshukuru heshima aliyopewa na Rais John Magufuli kwa muda wote
aliomsaidia kutekeleza majukumu yake ya ukatibu mkuu kiongozi na kueleza kuwa
Serikali ya sasa ni ya mabadiliko.
Wakati Sefue akiondoka, mhandisi John Kijazi amepokea kijiti
cha ukuu wa utumishi serikalini na kuahidi kuwa atafuatilia mazingira ya
watumishi wote pamoja na mazingira yao, ili kurekebisha panapohitajika kwa
lengo la kuongeza uwajibikaji na tija kwa wananchi.
Akizungumza muda mfupi baada ya kuapishwa kwa mrithi wake,
licha ya kumshukuru Rais, Balozi Sefue aliwataka watendaji wote serikalini
kumpa ushirikiano wa kutosha Balozi Kijazi ili kuleta ufanisi kwenye huduma za
umma.
“Namshukuru Rais kwa kuniamini kwa kipindi chote nilichodumu
naye. Ni heshima kubwa kuwatumikia Watanzania pamoja naye. Nitampa ushirikiano
wowote atakaouhitaji katibu mkuu kiongozi mpya kwenye utekelezaji wa majukumu
yake,” alisema Sefue.
Rais Magufuli, ameahidi na mara zote amekuwa akisisitiza
adhma yake ya kutumbua majipu kwa watumishi wote ambao hawaendani na kasi yake.
Tangu taarifa za mabadilio hayo zilipotangazwa jana, kumekuwepo na tetesi
nyingi kuwa huenda Sefue naye ni jipu lilikuwepo ikulu, suala ambalo halikupata
maelezo ya kutosha kutoka kwa balozi huyo.
Alipoulizwa juu ya tetesi hizo alijibu kwa ufupi: “Hii ni
Serikali ya mabadiliko.”
Kwa upande wake Kijazi, alisema atafanya kazi kwa kuzingatia
vipaumbele vya Rais huku akimshauri namna sahihi za kuboresha mazingira ya
utumishi serikalini.
Akieleza juu ya majukumu yake mapya, alionyesha kuyatambua
ipasavyo na kubainisha kuwa atashirikiana na Baraza la Mawaziri kwenye vikao
vyao, bila kusahau kuzifuatilia wizara husika na kuona endapo kila kitu
kinaenda kama inavyotakiwa.
“Nitakutana na mawaziri kwenye vikao vyao nitakavyoviandaa.
Nitawasiliana na kuwafuatilia watendaji wa wizara husika juu ya masuala
yatakayokuwa yamejitokeza ndani ya maeneo yao ya uwajibikaji. Kila mmoja
atimize wajibu wake ili Taifa lisonge mbele,” alisema Kijazi.
Ili kuitendea haki hadhi ya utumishi wa umma, Kijazi
ameahidi kuhakikisha kila kitu kinasimamiwa kwa ukaribu huku akitoa msisitizo
kwenye vipaumbele vya Rais. “Kwenye suala la mapato na rushwa, nitafuatilia kwa
nguvu ili kuongeza uwajibikaji kwa watumishi wa Serikali,” alisisitiza Kijazi.
Balozi Kijazi aliteuliwa juzi kushika nafasi inayoachwa na
Balozi Sefue. Kabla ya uteuzi huo, Kijazi alikuwa mwakilishi wa Tanzania kwa
nchi za India, Singapore, Sri Lanka, Bangladesh na Nepal huku makazi yake yakiwa
jijini New Delhi, India kuanzia mwaka 2007.
Katika wadhifa huo, alikuwa mkuu wa mabalozi wote
wanaowakilisha Tanzania nje ya nchi pamoja na mkuu wa mabalozi wa Afrika nchini
India. Kabla hajateuliwa kuwa mwakilishi wa nchi, Kijazi amekuwa mtumishi serikalini
kwa nafasi mbalimbali ikiwamo Katibu Mkuu Wizara ya Ujenzi kuanzia mwaka 2002
mpaka 2006.
Kabla ya hapo alikuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Maendeleo ya
Miundombinu kati ya mwaka 1996 hadi 2002.
Ndani ya Wizara ya Ujenzi, kabla hajawa katibu mkuu, alikuwa
mhandisi mwandamizi wa ujenzi wa barabara kisha kupandishwa cheo na kuwa
mkurugenzi wa barabara za mikoa.
Kumbukumbu za taaluma yake zinaonyesha kuwa alipata Shahada
yake ya kwanza ya Sayansi ya Uhandisi wa Umma mwaka 1982 kutoka Chuo Kikuu cha
Dar es Salaam, na baadaye Shahada ya Uzamili katika Uhandisi wa Barabara kutoka
Chuo Kikuu cha Birmingham, Uingereza mwaka 1992.
Jana wakati anaapishwa, saa 4:15 asubuhi, Kijazi alikuwa
sambamba na mke wake, Fransiscar Kijazi na kwa pamoja wamejaliwa watoto watatu,
David, Emmanuel na Richard. Kwa heshima ya familia hiyo, baada ya kukamilisha
protokali, Rais Magufuli alipiga picha ya pamoja na familia ya mteule huyo mpya
atakayehudumu ikulu kuanzia sasa.
Hata hivyo kwa mara ya mwisho, Sefue aliendelea na kazi yake
mpaka jana asubuhi na ndiye aliyemkabidhi Kijazi kitabu kitakatifu cha Biblia,
Katiba na kiapo cha uongozi ambacho alisaini.
Wadau wazungumza
Balozi Abdul Faraji alisema mabadiliko yaliyofanyika ya
katibu mkuu kiongozi ni ya kawaida katika nchi mbalimbali ulimwenguni, hasa
pale Serikali mpya inavyoingia madarakani. Alisema kila Rais mpya mara nyingi
hupenda kuingia ofisini akiwa na timu ya watu wake, ambao anaona watafanikisha
utelekelezaji wa malengo aliyojiwekea katika Serikali yake.
Faraji ambaye aliwahi kuwa Balozi wa Tanzania katika nchi
mbalimbali duniani ikiwamo Ufaransa (1972-1973), alisema balozi Sefue emeondoka
Ikulu akiwa amefanya kazi kubwa ambayo anatakiwa kupongezwa na kila Mtanzania.
“Tunamsifu kwa kazi yake hasa kwa kipindi hiki cha miezi mitatu ya utawala wa
Rais Magufuli. Alijitahidi kwenda na kasi ya mabadiliko kwa uwezo wake
ukizingatia alikuwa kwenye awamu ya Serikali ya awamu ya nne ambayo siasa yake
haikuwa na kasi kama ya sasa,” alisema.
Wakati mijadala katika mitandao ya kijamii ikiendelea juu ya
muda mfupi aliokaa balozi Sefue, Mhadhiri wa Idara ya Sayansi ya Siasa na
Utawala wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Shumbusho Damian alisema muda
huo huenda ulikuwa ni maalumu kumpatia uzoefu Rais Magufuli katika masuala
mbalimbali yaliyokuwa yakiendelea Serikalini.
“Jambo ambalo sikutegemea ni kumteua Kijazi kuwa Katibu Mkuu
Kiongozi kwa sababu nadharia iliyokuwepo ni kwamba Rais Magufuli anataka
kufanya kazi na watu wapya ambao hajawahi kufanya nao kazi”, alisema.
Katibu Mkuu wa chama cha CCK, Renatus Muabhi alimpongeza
Rais Magufuli kwa uteuzi huo na kueleza kuwa ni wakati mwafaka kwa Serikali
yake kuwachukulia hatua za kisheria wale wote wenye kashfa.
“Kila utawala ni lazima uwe na safu yake ya uongozi ili
kuondoa viraka vitakavyokwamisha utekelezaji wa baadhi ya mambo yanayoletwa na
mfumo mpya. Rais alitwambia kuwa ameikuta nchi katika hali mbaya, hivyo ni
wakati muafaka wa kuwaondoa wote wenye tuhuma,” alisema Muabhi.
Akizungumzia ahadi ya balozi Sefue kupangiwa kazi nyingine,
Mhadhiri wa Chuo cha Diplomasia, Dk Ahmed Kiwanuka alisema kauli hiyo ni ya
kawaida na humaanisha dhamira ya kweli ya Rais kutafuta nafasi mpya ya
kumpeleka mhusika hata kama itachukua muda mrefu. “Kuna kazi nyingine kama za
ubalozi ni lazima zipitie mchakato mrefu siyo rahisi kama watu wanavyofikiri.
Hivyo Rais hawezi ghafla akasema ‘namteua fulani kuwa balozi wa nchi fulani’
kama jina la huyo mtu halijakubaliwa upande wa pili,” alisema Dk Kiwanuka.
No comments:
Post a Comment