Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA) kama msimamizi na mratibu
wa sekta ya Sanaa nchini linapenda kutoa pongezi za dhati kwa Wasanii Single
Mtambalike (Rich Rich) na Elizabeth Michael (Lulu) kwa kushinda tuzo za African
Magic Viewers’ Choice Awards (AMVCA2016) zilizotolewa mwishoni mwa wiki nchini
Nigeria na kushuhudiwa na Dunia kupitia luninga na mitandao ya kijamii.
Katika tuzo hizo Msanii Singo Mtambalike ameshinda tuzo ya Filamu
Bora ya Lugha ya Asili (Best Local Language – Swahili) kupitia filamu ya
‘Kitendawali’ huku Msanii Elizabeth Michael (Lulu) akishinda tuzo ya Filamu
Bora ya Afrika Mashariki (Best Movie -Eastern Africa) kupitia filamu yake ya
‘Mapenzi’
Kuteuliwa na kushinda kwa Wasanii wa Tanzania katika tuzo
hizi zilizoshirikisha wasanii na filamu nyingi za Afrika ni ishara kwamba
wasanii wetu wanakubalika, kutambuliwa na kuthaminiwa ndani na nje ya Tanzania.
Aidha, ushindi huu unazidi kulipa heshima na kulitangaza
taifa letu katika nyanja mbalimbali hivyo kuzidi kulifanya ling’ae na kuwa
kinara katika ukanda huu wa Afrika Mashariki na Kati.
Baraza linatoa wito kwa wasanii na wadau wote kuzidisha
ubunifu, bidii na weledi katika kazi wanazozifanya ili wasanii wengi zaidi
waweze kuchomoza katika tuzo na majukwaa mbalimbali ya kimataifa kwa lengo la
kulitangaza taifa na kukuza soko la kazi zao kimataifa.
Ni matumaini ya Baraza kwamba wasanii wataendelea kutambua
umuhimu wa kufuata sheria, kanuni na taratibu za kutambuliwa na Serikali.
No comments:
Post a Comment