Licha ya Bodi ya Sukari Tanzania kutangaza bei elekezi ya
bidhaa hiyo kuwa ni Sh1,800 kwa Dar es Salaam, maeneo mbalimbali jijini inauzwa
kwa Sh2,200.
Juzi, Mkurugenzi Mkuu wa bodi hiyo, Henry Semwanza alisema
bei hiyo itatumika kwa maduka yote ya rejareja na wafanyabiashara wanatakiwa
kuizingatia pamoja na kuendelea kusambaza sukari kwa wingi.
Waandishi wetu waliotembelea maeneo mbalimbali yakiwamo
Manzese, Magomeni, Kariakoo, Kisutu na Gongo la Mboto walibaini kuwa mfuko wa
sukari wa kilo 50 ulikuwa unauzwa Sh97,000 hadi Sh100,000 huku wa kilo 25
ukiuzwa kuanzia Sh48,000 hadi Sh50,000.
Mfanyabiashara wa duka la jumla eneo la Manzese, Alex
Brayton alisema alikuwa akiuza sukari kwa bei ya rejareja Sh2,200 na kwamba
sababu kubwa ni kwamba sukari inayozalishwa viwandani haionekani wala
haitoshelezi hivyo wafanyabiashara wakubwa wamekuwa wanawauzia kwa bei ya juu.
“Suala la kushusha sukari hadi kufikia Sh1,800 kwa bei
elekezi halitawezekana kwa kuwa bei ya jumla ya kilo moja tunauziwa Sh2,000
hivyo tunalazimika kuuza Sh2,200 ili kilo moja tupate faida ya Sh200,” alisema
Brayton. Mfanyabiashara mwingine wa duka la jumla Magomeni, Idrisa Abraham
aliyekuwa akiuza mfuko wa sukari wa kilo 50 kwa Sh98,000 na wa kilo 25 kwa
Sh48,000, alisema kabla ya kutoa bei elekezi, Serikali ilitakiwa kufanya
utafiti ili kubaini sababu ya kutoonekana kwa bidhaa hiyo na kukutana na
wafanyabiashara wanaosambaza na wa maduka ya jumla ili kujua kwa nini sukari ya
Tanzania haionekani na kinachoifanya kupanda “...nina imani wangebaini kitu,
kinachonishangaza sukari iliyokuwa inatoka Malawi na Brazil ilikuwa inauzwa kwa
bei nafuu sana na ilikuwa inalipiwa kodi kwa nini ya Tanzania iwe bei juu?”
Mfanyabiashara wa duka la rejareja eneo la Gongo la Mboto,
Issa Salmin alisema wanauziwa kwa bei ya jumla Sh2,000 hivyo wanalazimika kuuza
kwa Sh2,200.
Mfanyabiashara wa rejareja Ubungo – Msewe, Joseph Masawe
alisema siyo rahisi kushusha bei ghafla wakati wafanyabiashara wakubwa
waliwauzia kwa bei ya juu.
Alisema wataweza kufanya hivyo ikiwa wafanyabiashara wakubwa
watashusha bei na ile waliyokwishanunua na kuihifadhi kwenye maghala itakuwa
imemalizika.
Masawe alisema Serikali inatakiwa kutengeneza mfumo
utakaowabana wafanyabiashara wakubwa ambao ndiyo chanzo cha kupanda kwa bei ya
sukari.
“Huwezi kutwambia tushushe bei ya bidhaa zilizo sokoni
wakati tulinunua kwa bei kubwa, cha msingi Serikali iwadhibiti wafanyabiashara
wakubwa ili washushe bei, vinginevyo itaendelea kuwa kama maigizo,” alisema.
Mfanyabiashara mwingine wa Mabibo, Henry Mwinuka alisema
anauza sukari kwa Sh2,200 baada ya kununua mfuko mmoja kwa Sh90,000 bei ambayo
ilikuwa juu.
“Nilinunua mifuko 15, kila mmoja Sh90,000. Ikiwa nitashusha
bei itakuwa hasara kubwa kwangu, lazima iishe kwanza ndipo tushushe na
tutafanikiwa ikiwa bei iliyo sokoni itakuwa chini ya Sh80,000,” alisema.
Alisema iwapo Serikali inataka kudhibiti bei ya bidhaa hiyo,
lazima iwabane wafanyabiashara wakubwa ambao wamekuwa wakijinufaisha kwa
kuingiza sukari ya magendo na kukwepa kodi.
“Kuna sukari inayoitwa KK ‘Grade four’ inasambazwa kama
kawaida wakati haitakiwi hata kidogo kutokana na kiwango chake.
Serikali haijaweza kabisa kuidhibiti. Hili ni tatizo,”
alisema.
Pia, alisema kuna janja imeanza kutumika kwa kuhifadhi
sukari hiyo kwenye mifuko ya kampuni za viwanda vya ndani, jambo ambalo ni
hatari zaidi.
No comments:
Post a Comment