Social Icons

IMETOSHA

IMETOSHA

Saturday, October 8, 2011

wizara ya habari wafukuzwa kwnye ofisi zao kwa kudaiwa kodi ya mda mrefu

OPERESHENI ya Shirika la Nyumba la Taifa (NHC), ya kuwafukuza katika nyumba zake wapangaji sugu jana ilibisha hodi katika Wizara ya Habari, Vijana,  Utamaduni na Michezo baada ya Idara zake za Habari (Maelezo) na Utamaduni kutupiwa nje virago zikidaiwa jumla ya Sh391 milioni. Deni hilo linaelezwa kuwa ni malimbikizo ya kodi ya pango kwa muda wa miaka mitatu mfulululizo.

Mchakato wa idara hizo kufukuzwa katika majengo ya NHC ulianza saa 3.00 asubuhi ukiongozwa na kampuni za udalali ya Mzizima Action Mart and Bedt Collect Ltd. Baada ya kufika katika ofisi hizo walikwenda moja kwa moja katika ofisi za uongozi na kueleza kusudio lao.
Bila kuchelewa wafanyakazi hao ambao walionekana dhahiri kujua walichokifuata, walianza kutoa kifaa kimoja baada ya kingine nje zikiwamo meza, viti, kompyuta, seti za televisheni na makabrasha mengine.

Kwa Maelezo, tukio hilo lilifanyika mbele ya macho ya waandishi wa habari ambao walikuwa katika ofisi hizo wakisubiri kuingia katika mikutano iliyokuwa imepangwa kufanyika. Kutokana na hali hiyo mikutano hiyo ilikwama.
Idara ya Maelezo ina ukumbi ambao hutumika kuendeshea mikutano ya habari ambayo wahusika hulipa kiasi kidogo cha fedha na kupata fursa ya kuzungumza na waandishi wa habari wa vyombo mbalimbali nchini.

Akizungumza wakati operesheni hiyo ikiendelea katika idara hizo, Meneja wa Kitengo cha Kukusanya Madeni NHC,  Japhet Mwanasenga alisema Idara ya Utamaduni inadaiwa Sh87milioni, Maelezo inadaiwa Sh47 milioni ikiwa ni kodi ya miezi saba na Idara ya Filamu inadaiwa Sh30 milioni ikiwa ni kodi ya miezi minane.

Alisema shirika lake limefikia uamuzi huo baada ya kutenda haki kwa kila mdaiwa. Alisema kwanza lilitoa notisi ya siku 14 ya kumtaka kila mdeni awe ameshalipa deni lake.

Alisema licha ya wizara hiyo kupelekewa notisi hiyo ilishindwa kulipa deni hilo kitendo kilichosababisha wachukue hatua zaidi. “Baada ya kuona wizara inadaiwa, NHC kupitia kitengo chake cha kukusanya madeni ilitoa taarifa katika kuhusiana na deni hilo lakini walijibu kuwa watalipa baada ya Serikali kupitisha Bajeti ya wizara,” alisema Mwanasenga.

Mwanasenga alisema hata hivyo, baada ya Bunge la Bajeti kumalizika, wizara hiyo ilipitishiwa bajeti yake lakini deni hilo halikulipwa ndipo NHC ilipoamua kuwasilisha nakala ya kukumbushia deni hilo.

Huu ni mwendelezo wa shirika hilo kuwatolea vifaa nje wadaiwa wake sugu. Juzi tukio kama hilo lilifanyika katika Wizara ya Kilimo, Chakula na Ushirika ikidaiwa Sh30 milioni.

 Akizungumzia kuhusu wizara hiyo, Mwanasenga alisema hadi jana wizara hiyo ilikuwa imeshalipa kiasi cha Sh25 milioni hivyo NHC kurudisha vifaa vyake kwa kuwa imeahidi kumalizia deni lililobaki baada  ya wiki moja.
















Wafanyakazi wa Kampuni binafsi ya udalalia wakitoa samani na vifaa vingine vya ofisi kutoka katika jengo ambalo walipanga Idara ya Habari (MAELEZO), Mtaa wa Samora, jijini Dar es Salaam, jana kutokana na kushindwa kulipa malimbikizo ya deni la pango wanalodaiwa na Shirika la Nyumba la Taifa (NHC


No comments:

Post a Comment