Guus
Hiddink amekatishiwa mkataba wa kuifundisha timu ya taifa ya Uturuki
baada ya nchi hiyo kushindwa kufuzu kwa fainali za Kombe la Euro mwaka
2012. Uturuki ilipoteza kwa jumla ya mabao 3-0 dhidi ya Croatia baada ya
kwenda sare ya kutofungana mechi ya pili siku ya Jumanne.Shirikisho la
Kandanda la Uturuki - TFF - limesema wamefikia makubaliano kumaliza
mkataba wa mwalimu huyo wa zamani wa Chelsea, ambao ulikuwa umalizike
mwakani. Hiddink, mwenye umri wa miaka 65, alichukua kazi ya kuifundisha
timu ya taifa ya Uturuki mwezi wa Agosti mwaka 2010 na nchi hiyo
ilishika nafasi ya pili katika kundi A. Hiddink alishawahi kuwa mwalimu
wa timu za taifa za Uholanzi, Korea Kusini, Australia na Urusi, pamoja
na vilabu vya PSV Eindhoven, Real Madrid na Chelsea. Taarifa rasmi
iliyotolewa na TFF katika mtandao imesema: "Tungependa kumshukuru Bw
Guus Hiddink kwa kazi yake wakati akiifundisha timu yetu ya taifa, na
tunamtakia kila la kheri katika kazi yake siku za usoni."Katika
mahojiano kabla ya mechi siku ya Jumanne alisema alitazamia kumaliza
kufanya kazi na Uturuki na akaongeza: "Nilifanya kazi kwa ajili ya
kuijenga timu kwa siku za mbele lakini nadhani hii itakuwa mechi yangu
ya mwisho na timu hii - ukweli ndio huo."Hiddink, anayeaminika ni mmoja
wa mameneja hodari wa kandanda, inasemekana bado anahitajika sana na
vilabu kama Paris Saint-Germain ya Ufaransa na Anzhi Makhachkala
zimeonesha tamaa ya kutaka kumchukua.
No comments:
Post a Comment