MICHUANO YA KOMBE LA UHAI (UHAI CUP)
Michuano ya
kuwania Kombe la Uhai (Uhai Cup 2011) inayoshirikisha timu za pili
(U20) za klabu zote 14 za Ligi Kuu ya Vodacom inatarajia kuanza Novemba
12 mwaka huu katika Uwanja wa Azam ulioko Chamazi, Dar es Salaam.
Timu ya Taifa ya
vijana wenye umri chini ya miaka 17 (Serengeti Boyz) itashiriki
michuano hiyo inayodhaminiwa na kampuni ya Said Salim Bakhresa ikiwa
timu mwalikwa.
Bingwa wa michuano
hiyo atapata sh. milioni 1.5, mshindi wa pili sh. milioni moja wakati
wa tatu atapata sh. 500,000. Mbali ya fedha hizo, bingwa atapata medali
za dhahabu, makamu bingwa medali za fedha na mshindi wa tatu medali za
shaba.
Mchezaji bora atapata
sh. 400,000, mfungaji bora (sh. 300,000), kipa bora (sh. 300,000) na
timu yenye nidhamu itapata sh. 300,000. Kila timu inayoshiriki
itapatiwa sh. milioni moja kwa ajili ya maandalizi.
Mdhamini pia
atagharamia nauli za kuja Dar es Salaam na kurudi kwa timu ambazo
zinatoka mikoani. Michuano hiyo itachezeshwa na waamuzi vijana kama
ilivyokuwa msimu uliopita.
Pia mradi wa Campaign
Against Malaria nao utasaidia kwa kutoa jezi kwa timu zote zinazoshiriki
michuano hiyo.
Kesho (Novemba 5 mwaka huu) saa 4 asubuhi kutakuwa na mkutano
kati ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) na klabu zenye timu
shiriki na baadaye kufanyika upangaji ratiba.
No comments:
Post a Comment