Na Mwandishi Wetu
SHIRIKA la Ndege la Air Tanzania (ATCL) limepata ndege
nyingine aina ya Boeing 737-500 ambayo inatarajia kuwasili leo hii Mchana
(Alhamisi) kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere Jijini Dar es
Salaam, taarifa iliyotolewa na Kampuni hiyo jana ilieleza.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, ndege hiyo yenye uwezo wa kubeba
abiria 108 imekodiwa kutoka katika kampuni ya Aero Vista iliyopo nchini Dubai
na tayari imeshafanyiwa uchunguzi na timu ya wataalam kutoka katika Mamlaka ya
Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA) nchini Misri ilikoperekwa kwa ajili ya
uchunguzi huo.
“Wataalam kutoka
Mamlaka ya Usafiri wa Anga (TCCA) wamekamilisha uchunguzi wa ndege ambayo kwa
sasa ipo jijini Cairo, Misri na ndege itarejea nchini kwetu leo hii mchana.
“Ndege hiyo imeshawekwa chata ya Kampuni ya ATCL na baada ya
kuwasili tunetegemea itaanza kufanya safari mara moja,” Taarifa hiyo ilisema.
Taarifa hiyo imeeleza kuwa ndege hiyo itakuwa na uwezo wa
kuchukua abiria 12 kwenye daraja la kwanza (business class) pamoja na abiria 96
kwenye daraja la kawaida (economy class).
Kaimu Mkurugenzi Mtendaji
wa ATCL, Bw. Paul Chizi akizungumza na waandishi wa Habari jijini Dar es
Salaam wiki chache zilizopita alitoa maelezo kwa uchache juu ya ujio wa ndege
hiyo lakini hakuweza kufafanua zaidi kuhusiana na ndege hiyo.
Chizi alisema kuwa mipango ya ujio wa ndege hiyo ilikuwa ni
mipango ya muda mfupi iliyowekwa ili kuboresha huduma za ndege alisisitiza kuwa
kampuni tayari ina mpango wa muda mrefu ambao utafanyiwa kazi kikamilifu.
ATCL hivikaribuni imezindua tovuti ikiwa katika jitihada za
kuboresha huduma kwa wateja pamoja na kuongeza ubora wa ndege hiyo ya kitaifa.
Tovuti hiyo itawawezesha wateja kupata taarifa ya safari za
ndege bila ya kufika katika ofisi za kampuni hiyo au mawakala na kuwawezesha
wateja kutoa maoni yao kupitia mitandao ya kijamii.
No comments:
Post a Comment