HOFU YATANDA NYUMBANI KWAKE, MILANGO YATIWA KUFULI
JESHI
la Polisi limesema liko tayari kumlinda kiongozi wa Jumuiya ya
Madaktari Tanzania, Dk Steven Ulimboka iwapo atahitaji ulinzi huo.Kauli
hiyo imekuja siku mbili tangu daktari huyo wa magonjwa ya binadamu
arejee nchini, huku usiri ukiwa umetawala taarifa zake kutokana na
kutokuwapo kwa ndugu, jamaa au rafiki aliyekuwa tayari kusema chochote
kumhusu.
“Nitachoweza
kusema ni kwamba nashukuru mwanangu amerejea salama, lakini siwezi
kusema chochote kuhusu mambo yanayomuhusu yeye,” alisema baba mzazi wa
Dk Ulimboka, Mzee Mwaitenda.
Tofauti
na juzi ambapo nyumbani kwake kulikuwa na watu kadhaa akiwamo
Mweitenda, jana mageti yote ya nyumba hiyo iliyoko eneo la Kibangu,
Manispaa ya Kinondoni, Dar es Salaam, yalifungwa na hapakuwa na mtu
yeyote ndani.
Katikati
ya hofu hiyo ya usalama, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni, Charles
Kenyela alisema Jeshi lake haliwezi kutoa ulinzi kwa Dk Ulimboka bila
yeye mwenyewe kuomba.
"Kwanza
walishaamua (madaktari) kuchagua ulinzi, sisi tufanyeje? Atakapoona
kuna ulazima atatujulisha," alisema Kenyela na kuongeza;
"Hatuwezi
kupeleka askari bila kuombwa. Ukipeleka halafu akasema hawahitaji,
itakuwa embarrasing (fedheha) sana. Sisi tunajua amerudi na tunamtakia
heri aendelee vizuri, apone na aungane na wenzake,"
Kamanda
Kenyela alifafanua kuwa nyumbani kwa mtu ni eneo la faragha ambalo
polisi hawawezi kwenda bila kuombwa na kufanya hivyo, ni kitu
kisichokubalika.
"Mimi
kama kamanda sijapokea ombi lolote kutoka kwa Ulimboka wala kusikia
tishio lolote dhidi ya usalama wake. Akiona kuna haja ya kulindwa, aseme
tutakwenda," alisema.
Awali
Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Suleman Kova alisema
hawezi kuzungumzia ulinzi wa Dk Ulimboka kwa sababu tayari madaktari
waliomba ulinzi UN.
UN wagoma kuongea
Msemaji
wa Mwakilishi Mkazi wa UN nchini, Hoyce Temu hakutaka kueleza endapo
taasisi hiyo ya kimataifa ilikubali ombi hilo au la akisema, suala la
ulinzi halipaswi kuwekwa hadharani.
Alifafanua kuwa iwapo suala hilo litawekwa hadharani ni sawa na kuwapa nafasi maadui kujua namna mipango ya ulinzi ilivyopangwa.
"Suala la security (usalama) kama lilivyo si suala la kuwekwa wazi kwa public (umma)," alisema Temu.
Mwanzoni
mwa Julai mwaka huu, Chama cha Madaktari Tanzania (MAT) kiliomba ulinzi
kutoka ofisi za Umoja wa Mataifa (UN) jijini Dar es Salaam kikieleza
kuwa hakina imani na polisi.
Chama
hicho kiliomba ulinzi huo baada ya kuwapo na madai kwamba kuna kikundi
cha watu kimekusudia kumuua Dk Ulimboka wakati akiwa kwenye matibabu
nchini Afrika Kusini.
Katibu
Mkuu wa MAT, Dk Rodrick Kabangila alipoulizwa endapo UN ilikubali kutoa
ulinzi kwa Dk Ulimboka alijibu "haikuwa lazima kwa UN kutujibu."
Aliongeza,
"Sisi tuliwasilisha barua, tukitoa malalamiko yetu, namna gani
watafanya kazi ya ulinzi siyo lazima watujibu, wao wanataratibu zao za
kufanya kazi."
Daktari wake anena
Profesa
Joseph Kahamba alisema hajaonana na Dk Ulimboka tangu arejee nchini
Jumapili ila anaamini anaendelea vizuri.Alipoulizwa imekuaje hajaonana
na mgonjwa wake wakati yeye ndiye aliyemwandikia rufaa ya kutibiwa nje
ya nchi alisema, "Siyo ajabu".
Alisema
siyo lazima daktari aliyemwandikia mgonjwa rufaa ya kwenda kutibiwa nje
ya nchi kuwasiliana naye anaporudi kwa kuwa hili linategemea hali
aliyonayo mgonjwa husika.
"Hapa
kuna mambo mawili; kuna kurudi akitakiwa tena kulazwa na kurudi kwa
maana ya kupona," alieleza Profesa Kahamba baada ya kuulizwa kama ni
lazima daktari aliyetoa rufaa awasiliane na mgonjwa baada ya kurudi
kwenye matibabu.
Aliendelea
"Angerudi (Dk Ulimboka) kwa state (hali) ya kulazwa, lazima angefikia
kwangu nimwone, lakini kama amepona, anaweza kwenda kusalimia ndugu na
kunywa bia kwanza halafu baada ya siku, wiki au mwezi akaja nikaonana
naye."
Profesa
Kahamba alieleza "Tangu Ulimboka arudi sijaonana naye zaidi ya kufanya
mawasiliano na wenzake kwenye simu ila amepona kwa kuwa hajarudi
kwangu."
MAT: Mwacheni apumzike
MAT
kimewataka waandishi wa habari kutoendelea kumfuatilia Dk Ulimboka
ambaye ni kiongozi wa jumuiya hiyo kwa kile walichoeeleza anatakiwa
kupata fursa ya kupumzika.Makamu wa Rais wa MAT, Dk Prinus Saidia
alipotakiwa kueleza ni lini atajitokeza hadharani kufuta kiu ya
Watanzania kuhusu kilichomsibu, alisema:“Yeye mwenyewe ametuomba
tumwache apumuzike kwa muda na sisi tumeona hili ni sahihi. Tumemwacha
kwanza hadi hapo atakapotuambia kuwa yuko tayari kuungana nasi.”
Dk
Saidia alisema madaktari kwa umoja wao wamefurahi kuona Dk Ulimboka
amerejea akiwa mzima na kwamba hilo ndilo jambo bora zaidi kuliko kitu
kingine chochote kwa sasa.
“Tunamshukuru
Mungu Dk Ulimboka amerudi akiwa mzima, hili ndilo lilikuwa la msingi.
Hata hivyo, suala liko wazi mgogoro baina yetu (madaktari) na Serikali
haujafikia mwafaka. Inatakiwa pande zote zikae na kukubaliana na si
upande mmoja kutumia nguvu,” alisema Dk Saidia.
Katika
hatua nyingine habari kutoka ndani ya MAT zinasema viongozi wake
wamekuwa wakifanya vikao vya ndani tangu juzi kujadili mambo mbalimbali
likiwamo la kuandaa mazingira yatakayomwezesha Dk Ulimboka kuzungumza
hadharani.
“Kuna
vikao vinaendelea tangu jana (juzi), viongozi wanakutana kujadili mambo
mbalimbali likiwamo namna Dk Ulimboka atakavyopata fursa ya
kuzungumza,” kilisema chanzo hicho.
Dk
Ulimboka alitekwa, kuteswa na kutupwa kwenye Msitu wa Pande nje kidogo
ya Jiji la Dar es Salaam usiku wa kuamkia Juni 26 mwaka huu.
Chanzo: http://www.mwananchi.co.tz
No comments:
Post a Comment