SERIKALI
imetaja manufaa na faida ambazo wanatarajia kuzipata wananchi wa Mtwara
pamoja na Lindi endapo gesi itasafirishwa kwenda Jijini Dar es Salaam.
Imesema Mkoa wa Mtwara ndipo utakapo jengwa mtambo mkubwa wa kusafishia
gesi hiyo kabla ya kusafirishwa kwenda jijini Dar es Salaam kwa
matumizi ya uzalishaji umeme na matumizi ya moja kwa moja viwandani.
Kauli
hiyo imetolewa jana na Naibu Waziri wa Nishati na Madini, George
Simbachawene alipokuwa akizungumza katika Kipindi cha Dakika 45
kinachorushwa na Kituo cha Radio One jijini Dar es Salaam.
Naibu
waziri huyo ameweka wazi kuwa mkoani Mtwara licha ya Serikali kupanga
kujenga viwanda vingine kadhaa, inajenga mtambo wa megawati 250 ambao
utakuwa ukizalisha umeme na mwingine kujengwa mkoani Lindi eneo la
Somanga Funga utakao kuwa ukizalisha megawati 520.
Akifafanua
zaidi Simbachawene alisema eneo la Mikindani katika Kijiji cha Msijute
mkoani Mtwara kinatarajiwa kujengwa kiwanda kikubwa cha saruji Afrika
Mashariki na Kati chenye uwezo wa kutoaji ajira kwa watu 6000 jambo
ambalo ni manufaa ya Wanamtwara.
Alisema
pia tayari kuna wawekezaji wa viwanda vya mbolea wamejitokeza kujenga
viwanda mkoani Mtwara na Serikali itaviacha vinu vya kuchimba na
kusindika gesi eneo hilo jambo ambalo bado ni manufaa makubwa kwa
wananchi.
“Viwanda
vya kusindika gesi hii vimepangwa kujengwa maeneo ya Lubasi, Kishere,
Mchinga Bay, Lindi, Sudi Bay, Airport pamoja na Mikindani…viwanda vyote
hivi vitatoa ajira kubwa sana,” alisema Naibu Waziri.
Alisema
licha ya manufaa hayo, gesi itakapopelekwa Dar es Salaam itazalisha
umeme wa uhakika pamoja na kutumika moja kwa moja viwandani jambo ambalo
litailetea taifa tija kubwa ikiwa ni pamoja kupunguza ukali wa maisha.
“Ni
kweli gesi imepatikana Mtwara lakini ni lazima uipeleke sokoni ili
iweze kupata soko (wateja)…Dar es Salaam ndio kwenye soko, huwezi
ukaiacha Mtwara ambako hakuna soko; mbali na kuzalisha umeme kuna
viwanda 37 na hoteli kadhaa zinataka ziitumie moja kwa moja ni lazima
iletwe huku, Mtwara pale hakuna soko,” alisema.
Aidha
alitolea mfano kuwa zipo nchi mbalimbali ambazo zimegundua gesi lakini
zimelazimika kuisafirisha kwa mabomba kwenda eneo la soko. Alibainisha
kuwa nchi ya Urusi inasafirisha gesi yake hadi nchini Ujerumani huku
Iran ikisafirisha hadi India gesi yake kutafuta soko lilipo.
Alisema
miundombinu mikubwa ya umeme ipo jijini Dar es Salaam hivyo kuna kila
sababu ya gesi hiyo kuletwa jijini humo ili iweze kuzalisha umeme na
matumizi ya viwandani moja kwa moja pamoja na matumizi mengine, ambapo
tayari wateja wamepatikana.
Aidha
aliongeza kuwa uzalishaji umeme wa kutosha kwa kutumia gesi utapunguza
bei ya umeme na kuuzwa kati ya senti 6 na 8 za Marekani jambo ambalo
litapunguza ugumu wa maisha na pia bei ya bidhaa nchini.
Pamoja
na hayo amevitaka baadhi ya vyama vya siasa na taasisi zisizo za
Serikali (NGO’s) zinazowapotosha Wanamtwara juu ya mradi huo kuacha
kitendo hicho kwani hakuna asiyejua umuhimu wa gesi hiyo kuja Dar es
Salaam.
“Hivi
ni nani asiyejua kuwa tatizo la kutokua na umeme wa uhakika nchini
ndilo linalokwamisha uchumi wa nchi…Tanzania inapoteza bilioni 4.5 kwa
ajili ya kununua mafuta ya kuzalisha umeme kwenye mitambo yake, sasa
gesi itaokoa fedha hizi,” alisema Simbachawene.
Hata
hivyo amesema Serikali haiwezi utekeleza mradi huo kwa nguvu bali
itaendelea kuwaelimisha Wanamtwara umuhimu na manufaa ya gesi hiyo
kuletwa Dar es Salaam na inaimani wataelewa na malumbano kumalizika.
No comments:
Post a Comment