Pages

Monday, April 15, 2013

KAULI YA MJENGWA BAADA YA KUKAMATWA NA POLISI MAKAO MAKUU KUHUSU KUTEKWA KWA KIBANDA




Ndugu zangu,
Kama alivyowataarifu kaka yangu Nyaroonyo Kichehere, ni kuwa, jana Jumamosi nilikuwa Makao Makuu ya Jeshi la Polisi kuanzia saa tano asubuhi ya jana mpaka saa tatu usiku. Ilihusu mahojiano ya Polisi na mimi kuhusiana na sakata la ndugu yetu Absalom Kibanda.


Ukweli sikukamatwa mahali popote, bali niliitwa na Kamishna ( Upelelezi) Advocate Nyombi. Alhamisi nikiwa Iringa, tukakubaliana na kiungwana na Kamishna Nyombi kuwa nifike Makao Makuu hayo ya polisi Jumamosi saa tano. Ikawa hivyo.


Hapo nilipokelewa na Kamishna Nyombi. Baada ya mazungumzo mafupi ndipo akawaita maofisa wengine watano wa Upepelezi kufanya mahojiano nami.


Niliomba niwe na Mwanasheria, nikakubaliwa. Nilimpigia simu kaka yangu Nyaroonyo, naye, kwa vile ni Wakili pia wa Kibanda akanisaidia kuhakikisha napata wakili mwingine. Pamoja na kuwa ilikuwa ni Jumamosi, ndugu yangu Nyaroonyo Kichehere alifanya alivyoweza.





Ndani ya dakika 40 hivi alifika chumba nr 704 ghorofa ya saba akiwa na Wakili Jacquiline Rweyongeza na Legal Officer Dickson Mbonde. Nilimshukuru Kaka Nyaroonyo Kichehere. Na nilimuaga kwa kumwambia; “ Nenda ukaifahamishe jamii juu ya hiki kilichonitokea”.


Nachukua fursa hii pia kuwashukuru kwa dhati kabisa dada yangu Wakili Jacquiline Rweyongeza na kaka Dickson Mbonde kwa kuacha yote ya Jumamosi na kuwa tayari kuwa msaada kwangu. 


Jacquiline alimuacha nyumbani mtoto wake wa miezi minne kwa ajili ya suala langu. Sina namna nyingine ya kumshukuru. Na hakika, msaada wao niliuhitaji sana.

Nawashukuru pia kwa dhati kabisa, ndugu zangu Saed Kubenea, Mbaraka Islam na wengine wote waliokuwa na utayari wa kunisaidia pale msaada wao ulipohitajika. 



Kwa ufupi, nimetoa maelezo yangu bila shuruti wala kutishwa.



Na nimeweka wazi kuwa yanaweza kutumika Mahakamani kama yatahitajika au hata kama mimi nitahitajika, kwa namna yeyote ile.

Kesho saa mbili asubuhi nitaripoti Makao Makuu ya Polisi kupewa maelezo ya kitakachofuatia.Kwa mara nyingine tena, nawashukuru sana kwa kuwa nami katika muda wote huu.
Maggid,
Dar es Salaam.

No comments:

Post a Comment