Na Boniface Wambura,
IMEWEKWA MEI 19, 2013 SAA 6:20 MCHANA
MECHI
ya watani wa jadi Simba na Yanga la Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara,
iliyochezwa jana (Mei 18 mwaka huu) kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es
Salaam na kumalizika kwa mabingwa wapya Yanga kushinda mabao 2-0
imeingiza sh. 500,390,000.
Mechi hiyo namba 180 ambayo ilikuwa kati ya saba la kuhitimisha ligi
hiyo msimu wa 2012/2013 ilishuhudiwa na watazamaji 57,406 waliokata
tiketi kwa viingilio vya sh. 5,000, sh. 7,000, sh. 10,000, sh. 15,000,
sh. 20,000 na sh. 30,000.
Kila klabu imepata mgawo wa sh. 123,970,927.45 wakati Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) iliyolipwa ni sh. 76,330,677.97.
Kiingilio cha sh. 5,000 ndicho kilichovutia watazamaji wengi ambapo
waliokata tiketi hizo walikuwa 19,039 na kuingiza sh. 95,195,000 wakati
kile cha sh. 7,000 kiliingiza watazamaji 17,647 na kupatikana sh.
123,515,000.
Mgawo mwingine wa mapato hayo ni asilimia 15 ya uwanja sh.
63,036,064.81, tiketi sh. 3,818,890, gharama za mechi sh. 37,821,638.88,
Kamati ya Ligi sh. 37,821,638.88, Mfuko wa Maendeleo ya Mpira wa Miguu
(FDF) sh. 18,910,819.44 na Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Dar es
Salaam (DRFA) sh. 14,708,415.12.
Ushindi huo leo, umenogesha sherehe za taji la 24 la ubingwa wa Ligi
Kuu ya Vodacom Tanzania Bara kwa Yanga, kwani mashabiki wa timu hiyo
waliangusha bonge la shangwe kuanzia kushangilia mabao hadi taji.
Kwa matokeo hayo, Yanga inamaliza msimu wa Ligi Kuu ikiwa na pointi
60, ikifuatiwa na Azam FC iliyomaliza na pointi 55 na Simba 45.
Katika mchezo huo, ambao Saanya alisaidiwa na Samuel Mpenzu wa Arusha
na Jesse Erasmo kutoka Morogoro, hadi mapumziko Yanga walikuwa mbele
kwa bao 1-0 lililotiwa kimiani na Didier Kavumbangu dakika ya tano tu.
Kavumbangu alifunga kwa kichwa akiuwahi mpira wa juu uliopanguliwa na
kipa na Nahodha wa Simba, Juma Kaseja kufuatia kona iliyochongwa na
Haruna Niyonzima kutoka wingi ya kushoto. Mpira uliozaa kona hiyo
ulitokana na Simon Msuva ambaye alikuwa anachanja mbuga, lakini beki
Haruna Shamte akatoa nje.
Simba ilipata nafasi ya kusawazisha dakika ya 27 baada ya Mrisho
Ngassa kuangushwa kwenye eneo la hatari na Nadir Cannavaro na refa
Saanya kuamuru penalti, lakini mkwaju wa Mussa Mudde ulipanguliwa na
Ally Mustafa ‘Barthez’ kabla ya kipa huyo kuuchupia na kuudaka.
Kwa ujumla, Yanga ilitawala kipindi cha kwanza karibu chote ingawa
mwishoni mwa kipindi hicho, kidogo Haruna Chanongo aliitia majaribioni
ngome ya Yanga kama mara mbili hivi na kusababisha kona mbili mfululizo.
Kipindi cha pili, Simba SC walikianza vizuri dakika 10 za mwanzo
wakipeleka mashambulizi langoni mwa Yanga kutokea pembeni, lakini safu
ya ulinzi ya mabingwa hao wa Bara ilisimama imara kukabiliana na hatari
zote.
Krosi maridadi ya Simon Msuva dakika ya 62 iliunganishwa vyema
kimiani na Hamisi Kiiza ‘Diego’ kuipatia Yanga bao la pili. Baada ya bao
hilo, Yanga sasa walianza kucheza kwa kujiamini zaidi na Simba
wakionekana kucheza ili kutoruhusu mabao zaidi.
Dakika ya 87, refa Saanya alijeruhiwa wakati anakwenda kuamua ugomvi
kati ya Didier Kavumbangu na Nassor Masoud ‘Chollo’ akaanguka na
kutibiwa kwa dakika hadi kuinuka dakika ya 90 na kumaliza mpira baada ya
sekunde kadhaa.
Baada ya mchezo huo, kiungo Athumani Iddi ‘Chuji’ wa Yanga alitajwa
kuwa mchezaji bora wa mechi na kupewa zawadi ya Sh. 100,000 na wadhamini
wa
No comments:
Post a Comment