Pages

Saturday, September 28, 2013

AZAM TV KUONYESHA MECHI ZOTE ZA YANGA TV


tv 

KITUO cha Televisheni cha Azam kimeahidi kuonyesha mechi za Yanga zitakazochezwa katika Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam na zile za ugenini kwa sababu mkataba unawaruhusu.
 
Katibu Mkuu wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Angetile Osiah amethibitisha kuwa Azam TV wapo huru kuonyesha mechi yoyote ya Ligi Kuu Bara.

Habari nzuri ni kuwa ving’amuzi vya Azam TV vitaanza kuuzwa mwanzoni mwa wiki ya kwanza ya mwezi ujao kabla ya mechi kuanza kuonyeshwa ama Oktoba 5 au Oktoba 9, mwaka huu.

Habari kutoka Azam TV zinasema kuwa wataonyesha pia mechi zinazoihusu Yanga kwa sababu mkataba unawataka kuonyesha mechi za Ligi Kuu Bara.

Yanga waligoma kusaini mkataba wa Azam TV kwa madai kuwa Sh 100 milioni ambazo kila klabu inapewa ni ndogo sana kwao.

“Mkataba wetu unasema kuwa tunatakiwa kuonyesha mechi za Ligi Kuu Bara, kwa hiyo tutaonyesha pia mechi za nyumbani na ugenini za Yanga, kwa sababu mkataba wetu tumesaini na Kamati ya Ligi,” alisema mmoja ya viongozi wa Azam TV.

Akizungumzia hilo, Katibu Mkuu wa TFF, Osiah alisema Azam TV wapo huru kuonyesha mechi yoyote kwa sababu mkataba unawaruhusu.

“Hata kama ni mechi za Yanga iwe Dar es Salaam au mikoani, Azam TV wanaruhusiwa kuonyesha,” alisema Osiah.

Katika hatua nyingine, wataalamu kutoka Afrika Kusini wanatoa mafunzo kwa wafanyakazi wa Azam TV mpaka Oktoba 15, mwaka huu.

“Hawa wataalamu wameomba kabla hawajaondoka warushe mechi mbili laivu kuona kama kuna upungufu wowote. Na ndiyo maana nadhani mechi za raundi ya saba za Oktoba 5 au mechi za raundi ya nane za Oktoba 9, zitaanza kuonyeshwa moja kwa moja,” alisema mmoja wa mabosi wa Azam TV.

Alisema wataanza kuonyesha mechi za Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam na mechi za mikoani zitaanza kuonekana baada ya kuwasili kwa gari la OB Van ambalo litashughulika na mechi za mikoani tu.

Kama Azam TV itaanza kuonyesha mechi Oktoba 5, ina maana kwamba wataanza na mechi ya Simba dhidi ya Ruvu Shooting au siku inayofuata wanaweza kuonyesha pia Yanga dhidi ya Mtibwa. Iwapo mechi hizo hazitaonyeshwa maana yake mechi za raundi ya nane zinazoweza kuonyeshwa ni Azam dhidi ya Mgambo Oktoba 9, au Simba dhidi ya Prisons Oktoba 12 na Ashanti dhidi ya Coastal Union Oktoba 13.
Habari za ndani zinasema ving’amuzi vya Azam TV vitaanza kuuzwa wiki ya kwanza ya mwezi ujao.
CHANZO: GAZETI LA MWANASPOTI

No comments:

Post a Comment