ISHARA YA VIDOLE VIWILI, PEOPLES POWER VYATAWALA
RAIS Jakaya Kikwete jana alipata wakati mgumu, baada ya kukutana na
nguvu ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) jijini Mwanza
katika ziara yake, huku Waziri wake wa Ujenzi, Dk. John Magufuli, naye
akijikuta akizomewa mbele yake. Mbunge
wa Nyamagana, Ezekia Wenje, alivunja mwiko baada ya kujiunga katika
msafara huo wa raia akiwa na gari lenye alama za Movement for Change
(M4C) lililokuwa limefungwa bendera mbili za CHADEMA. Hata
hivyo maofisa usalama walipata wakati mgumu kulizuia gari hilo lisiwepo
katika msafara huo, jambo lililozua tafrani kidogo katika uwanja wa
Furahisha ambapo Kikwete alikuwa akihutubia mkutano wa hadhara. Awali
wakati wa uzinduzi wa wodi ya wazazi iliyoko eneo la Butimba, Rais
alilazimika kumpa Wenje nafasi ya kuwasalimia wananchi baada ya Mkuu wa
Mkoa, Evarist Ndikilo, kutaka kufanya hila ya kumnyima haki hiyo kama
mbunge wa jimbo husika.
Baada ya viongozi wote kutambulishwa bila Wenje kutajwa, wananchi
walianza kupaza sauti wakitaka mbunge wao naye atambulishwe. Wenje
baada ya kusimama alimshukuru Rais Kikwete kwa kumpa nafasi hiyo lakini
akamwomba amvumilie kidogo atoe salamu maalumu ya wana Mwanza. Kama
kawaida ya CHADEMA kwenye salamu yao, Wenje aliwaomba wananchi wakunje
ngumi kisha akawasalimu kwa kibwagizo cha peoples… nao wakamwitikia
power! Akiwa
katika viwanja vya Furahisha ambapo Rais Kikwete alichelewa kuanza
mkutano wake, Wenje alifika hapo na kushangiliwa kwa nguvu na wananchi
huku polisi wakiwazuia bila mafanikio. Ilipofika
saa 12 jioni kabla Rais hajaingia uwanjani, wananchi hao walimtaka
Wenje awahutubie huku wakidai bendera ya taifa ishushwe kwani muda wake
ulikuwa umefika.
Kikwete aliingia uwanjani hapo saa 12:10 akiongozana na viongozi
mbalimbali wa chama na serikali lakini wananchi hawakuonyesha
kumshangilia badala yake walikuwa wakimwonyesha alama ya vidole viwili
inayotumiwa na CHADEMA wakiimba ‘peoples…power’. Katika
hatua ya kushangaza wananchi hao walimshangilia kwa nguvu mbunge wa
Ilemela, Highness Kiwia, aliyekuwa ameongozana na Rais huku wakiwazomea
Meya wa Manispaa ya Ilemela, Henry Matata, ambaye hakufika kabisa
mkutanoni hapo. Matata
alionekana mapema wakati Rais Kikwete akisomewa taarifa ya maendeleo
makao makuu ya wilaya hiyo lakini hakufika uwanjani kabisa katika viti
vya mbele alionekana naibu wake, Swila Dede.
Baadhi ya wananchi hao walisikika wakisema chini kwa chini kuwa
Matata ni mwizi hawataki kumsikia lakini shangwe na nderemo zikajiri
pale walipotambulishwa Wenje na Kiwia. Rais
Kikwete akiwa wilaya ya Ilemela, wananchi wengi waliokuwa wamesimama
njiani walimwonyesha vidole viwili ikiwa ni alama CHADEMA. Hata
hivyo, hali hiyo ilionekana kumkera kiongozi huyo wa nchi pamoja na
maofisa wa usalama, ambapo wana usalama wakiwemo polisi walionekana
wakiwatisha na kuwazuia wananchi kunyoosha vidole viwili.
Magufuli azomewa
Waziri wa Ujenzi, Dk. Magufuli, alikumbana na jinamizi la
kuzomewa mbele ya Rais baada ya kusimama jukwaani na kutaja jina la
Matata, ambapo wananchi wengi walimzomea kwa miluzi huku wakimnyooshea
vidole viwili. Adha
Magufuli alizomewa pia aliposema wabunge wa Ilemela na Nyamagana jijini
hapa ni wana CHADEMA lakini ndani ya roho zao ni wana CCM. Pia aliendelea kuzomewa aliposema kuwa iwapo Rais angehitaji kupokea kadi za CHADEMA zilizorudishwa angepokea nyingi. “Mheshimiwa
Rais, nampongeza Meya Matata (akazomewa), lakini pia wabunge wa Ilemela
na Nyamagana wanachapa kazi vizuri, nje CHADEMA lakini ndani wao CCM
(akazomewa).” Akizungumza
katika mkutano huo, Rais Kikwete alimpongeza mbunge wa Nyamagana kwa
uchapakazi mzuri hasa kusimamia sekta ya elimu na kwamba wabunge wa
namna hiyo wanastahili kuigwa.
Hata hivyo, alisema serikali yake imejipanga vizuri kuhakikisha
usafiri wa reli, ndege, majini na barabara za lami vinaboreshwa maradufu
kwa ajili ya maendeleo ya wananchi. “Serikali
yangu imeweka nguvu kubwa katika kuboresha sekta ya uchukuzi, ujenzi na
nyinginezo. Hii ni kutaka kuwaletea wananchi wetu maendeleo ya
kisekta,” alisema. Baadhi
ya mawaziri walioongozana na Rais mbali na Magufuli ni Naibu Waziri,
Ofisi ya Makamu wa Rais, Charles Kitwanga, Waziri wa Kilimo, Chakula na
Ushirika, Christopher Chiza, Waziri wa Maji, Prof. Jumanne Maghembe,
Naibu Waziri wa Ujenzi na Dk. Charles Tizeba.
from Tanzania Daima
No comments:
Post a Comment