Dar
es Salaam. Mshambuliaji wa nyota wa zamani wa timu ya soka ya Simba na
Taifa, Joseph Kaniki ‘Golota’ na bondia Mkwanda Matumla wanashikiliwa
huku Addis Ababa, Ethiopia wakituhumiwa kusafirisha dawa za kulevya.
Kukamatwa
kwao kumezidi kuongeza idadi ya Watanzania maarufu waliotiwa mbaroni
nje ya nchi katika siku za karibuni wakituhimiwa kwa makosa hayo.
Tukio
hilo limetokea miezi miwili baada ya Watanzania wawili, wasanii Agnes
Gerald Masogange na Melisa Edward kukamatwa kwenye Uwanja wa Oliver
Tambo, Afrika Kusini wakituhumiwa kusafirisha dawa za kulevya zenye
uzito wa kilo 150 na thamani ya Sh6bilioni.
Aidha,
hilo limetokea baada ya meli ya mizigo ya Gold Star iliyosajiliwa
nchini kukamatwa na maofisa Forodha na askari wa doria wa Italia katika
Pwani ya Sicily, Bahari ya Mediterranean ikiwa na tani 30 ya dawa za
kulevya aina ya bangi zenye thamani ya Pauni za Uingereza 50milioni
(Sh125 bilioni).
Kaniki
na Matumla walikamatwa Agosti 31, mwaka huu kwenye Uwanja wa Ndege wa
Bole, Addis Ababa wakati wakijiandaa kupanda ndege ya Shirika la Ndege
la Ethiopia tayari kwa safari ya kuelekea Paris, Ufaransa.
Kaimu
Balozi wa Tanzania nchini Ethiopia, Samuel Shelukindo alithibitisha
jana kwamba wanamichezo hao wanashikiliwa nchini humo na Polisi wa
Kitengo cha Uchunguzi wa Makosa ya Jinai.
Wanamichezo
hao wamepandishwa kizimbani katika Mahakamu Kuu ya Ethiopia iliyoko
kwenye eneo la Arada, Addis Ababa kujibu tuhuma za kubeba kilo saba za
dawa hizo haramu. Mkwanda anadaiwa kubeba kilo nne wakati Kaniki
akidaiwa kubeba kilo tatu. Kama watapatikana na hatia, wanaweza kufungwa
kifungo cha miaka tisa hadi 15.
Alisema
uwezekano wa kesi ya Kaniki na Matumla kurudishwa Tanzania haupo kwa
kuwa nchi hizi mbili hazina utaratibu wa kubadilishana wafungwa.
“Wameshikiliwa
hapa Ethiopia kwa zaidi ya siku 10 sasa, sisi tulipigiwa simu na polisi
wa hapa Alhamisi iliyopita kujulishwa kwamba kuna Watanzania wawili
wameshikiliwa kwa tuhuma za kukutwa na dawa za kulevya, tulipokwenda
tukamkuta ni Kaniki na Matumla,” alisema Shelukindo.
“Wao
wenyewe wanaeleza kwamba walipitia Mombasa na huo mzigo walipewa na mtu
mmoja. Lakini Kaniki yeye anajitetea kwamba huyo aliyewapa huo mzigo
pale Mombasa anajuana vizuri na Mkwanda. “Kwa hiyo alichofanya yeye ni
kuubeba tu. Walikuwa wapitie hapa Addis wakashuke Paris, Ufaransa ndipo
warudi Sweden kwa njia zao wanazojua wenyewe. Walipofika hapa Mkwanda
alifanikiwa kupenya akapanda ndege lakini Kaniki akanaswa na mbwa ndipo
akajitetea kwa polisi kwamba lile begi lilikuwa lake lakini mizigo
mingine ilikuwa ya Mkwanda.
“Ndipo
hapo sasa Mkwanda akashushwa kwenye ndege wakashikiliwa na Jumatatu ya
wiki iliyopita wakapandishwa kwenye Mahakama ya hapa kutajiwa kesi yao
lakini hawakupewa nafasi ya kujitetea. Kesi itatajwa tena Jumanne (leo)
na Jumatano (kesho) na uchunguzi wa polisi bado unaendelea.”
Wanamichezo
hao walidai kwamba walikabidhiwa mizigo hiyo kwenye Uwanja wa Ndege wa
Mombasa walipokuwa wakikabidhiwa pasi za kupandia ndege baada ya kupita
sehemu zote za ukaguzi.
“Kilichotokea
ni jambo la aibu kwa nchi na hata wachezaji wenyewe wanajuta. Kwa
mfano, Kaniki anasema alikuwa aende England kucheza mpira Desemba lakini
sisi tukamwambia hatuwezi kumsaidia inabidi akabiliane na kesi iliyoko
mbele yake. Mkwanda yeye ametuambia kwamba anaishi Sweden hatuna maelezo
yake zaidi,” alisema Shelukindo na kuongeza kuwa wamewapelekea
wanamichezo hao msaada wa mablanketi kwa vile bado wako mahabusu na
Ethiopia kwa sasa kuna baridi kali.
Shelukindo
alisema wachezaji hao wapo mahabusu kwenye Kituo cha Polisi cha
Uchunguzi wa Makosa ya Jinai (Federal Police Crime Investigation) na
hawana chochote zaidi ya nguo walizokuwa wamevaa.
Watanzania wengine kuachiwa leo
Shelukindo
alisema kuna Watanzania wanne wanaotazamiwa kuachia leo baada ya
kumaliza vifungo vyao baada ya kupatikana na hatia ya kusafirisha dawa
za kulevya.
“Kuna
Watanzania wengine walinaswa hapa miaka ya nyuma wao walikuwa wamemeza
wakapasuliwa dawa zikatolewa na baadhi yao walifariki. Hata hivyo, wanne
ambao wamemaliza vifungo vyao vya miaka minne wanaweza kurudishwa
Tanzania,” alisema Shelukindo.
No comments:
Post a Comment