JESHI la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), limevitaka vyombo vya habari kuacha kuandika taarifa za mgogoro wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), badala yake taarifa rasmi zitakuwa zikitolewa na jeshi hilo kila baada ya wiki mbili.
Katazo
hilo limetolewa jana jijini Dar es Salaam na Meja Erick Komba wakati
akizungumza na waandishi wa habari kuhusu maendeleo ya mgogoro huo.
Alisema
hali hiyo inatokana na jeshi hilo kubaini kuwa baadhi ya vyombo vya
habari nchini vinaandika habari za uchochezi zinazotaka kuziingiza
vitani nchi ya Tanzania na Rwanda.
Meja
Komba alisema hategemei kama kutakuwa na chombo chochote cha habari
kitakachotoa habari kuhusu maendeleo ya mgogoro huo bila kupata taarifa
rasmi kutoka jeshi hilo.
Alionya kuwa chombo chochote kitakachokwenda kinyume kitakuwa kina tatizo.
Meja Komba alisema wananchi wanapaswa
kuelezwa kuwa kikosi cha Tanzania kilichoko DRC ni sehemu ya Brigedia
ya SADC, iliyotoa mchango wake katika Jeshi la Umoja wa Mataifa
(Monusco).
Alitaja majukumu ya kikosi hicho kuwa
ni kuzuia waasi wa M23 na wengine kujitanua, kuvunja nguvu zao na
kuyapokonya silaha makundi yote ya waasi.
“Kwa kuzingatia kuwa kikosi chetu
kiko chini ya majeshi ya Monusco, inamaanisha kuwa operesheni hiyo ni ya
Umoja wa Mataifa,” alisema.
Aliongeza
kuwa Tanzania haikupeleka kikosi chake DRC kwa ajili ya kupigana na
M23, pia ieleweke kuwa haina tatizo na Rwanda kuhusiana na operesheni
hiyo ambapo Rwanda ilitoa ridhaa kikosi cha Tanzania kwenda DRC.
Meja
Komba alisema Rwanda ni miongoni mwa wanachama wa nchi za Maziwa Makuu,
ambayo imesaidia kwa kuruhusu kikosi cha Tanzania kupitisha vifaa na
zana katika nchi yake kupeleka DRC.
“Tanzania inashiriki katika
operesheni hiyo ya ulinzi wa amani nchini DRC kutokana na mgogoro kati
ya serikali na waasi hususan kikundi cha M23,” alisema.
Mgogoro huo ulianza Aprili mwaka
jana, ambapo kikundi cha M23 kilijitoa katika jeshi la serikali na
kuanzisha mapigano yaliyosababisha hali ya usalama nchini DRC kuwa
mbaya.
Katika hatua nyingine, Waziri wa
Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe Benard, amesema
kuwa marais Jakaya Kikwete na Paul Kagame wa Rwanda wamemaliza tofauti
zilizokuwa zimejitokeza kati yao hivi karibuni.
Marais hao walikutana na kufanya
kikao cha faragha jijini Kampala nchini Uganda juzi baada ya mkutano wa
viongozi wa nchi za Maziwa Makuu na baadaye kutoa taarifa kwa waandishi
wa habari.
Kuzorota
kwa mahusiano kati ya viongozi hao kulikuja kufuatia kauli ya Rais
Kikwete ya kumtaka Rais Kagame kukaa meza moja na vikundi vya waasi wa
nchi yake vilivyo nchini Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo, ushauri
ulioonekana kumkera Rais Kagame.
Akizungumza na waandishi wa habari
jana jijini Dar es Salaam, Membe alisema marais hao walitumia mazungumzo
yao yaliyochukua muda wa saa moja kujadiliana na kueleweshana mambo
mbalimbali yaliyosababisha kutoelewana.
“Baada ya mkutano huo ambao uliwapa
fursa za kuchambua, kujadili na kurejesha mahusiano ya kihistoria kati
ya nchi hizi mbili, marais wetu walitoka na nyuso za furaha,” alisema.
Moja ya maazimio ya kikao chao ni kuwa na vikao vingine kati ya Rwanda na Tanzania katika siku zijazo.
“Kwa
kweli kikao kati ya Rais Kikwete na Rais Kagame kimeondoa majungu yote,
kimekata fitina, uongo na maneno ya kuchombeza yaliyokuwa yakitawanywa
na watu mbalimbali hapa nchini na hata kule Kigali,” alisema.
Mbali
ya kikao hicho pia Rais Kikwete alifanya kikao kingine cha faragha na
Rais wa Uganda Yoweri Museveni ambapo walipata muda wa kujadiliana kwa
kina kuhusu mambo mbalimbali kuhusu nchi zao na mambo ya migogoro katika
nchi za Maziwa Makuu.
Akizungumzia
yale yaliyokubaliwa katika mkutano wa viongozi wa nchi za Maziwa Makuu,
Membe alisema kuwa mkutano huo kwanza ulimruhusu Rais Museveni aendelee
kusuluhisha vita ya serikali ya DRC na waasi.
Alisema
kuwa viongozi hao walilaani mashambulizi ya M23 yaliyojeruhi na kumuua
Meja Mshindo wa Tanzania aliyekuwa miongoni mwa askari walioko nchini
Congo katika kusimamia amani chini ya Umoja wa Mataifa.
No comments:
Post a Comment