MWANASHERIA maarufu nchini, Damas Ndumbaro, amemkingia kifua rais mpya wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Jamal Malinzi, kwa kitendo chake cha kuvunja kamati za shirikisho hilo akisema bosi huyo hajavunja Katiba.
Ndumbaro aliliambia Mwanaspoti jana Jumatano kuwa
kamati za kisheria za shirikisho hilo zinaweza kuvunjwa na Mkutano Mkuu
wa TFF na Malinzi aliomba ridhaa ya mkutano mkuu kabla ya kufanya hivyo.
“Malinzi aligundua kuwa mwenye mamlaka ya kuvunja
kamati za TFF ni Mkutano Mkuu tu. Kumbuka kuwa Mkutano Mkuu hukutana
mara moja tu kwa mwaka, kwa hiyo asingefanya hivyo maana yake kamati
hizo zingeendelea kuwapo mpaka mwakani,” alisema Ndumbaro.
“Ndio maana Malinzi aliomba ridhaa ya mkutano mkuu ili avunje kamati hizo na akakubaliwa. Kwa hiyo alifuata katiba inavyotaka.”
Alipoulizwa Malinzi aliombaje hivyo wakati suala
hilo halikuwamo katika ajenda, Ndumbaro alisema ilimradi ilikubaliwa na
wajumbe basi hakuna tatizo.
Ndumbaro ambaye ni wakala wa wachezaji
anayetambuliwa na Fifa, alisema Malinzi pia hakukosea alipovunja kamati
ndogondogo za shirikisho hilo kwa sababu kamati hizo huvunjwa na kamati
ya utendaji ya TFF.
“Kamati ya Utendaji ndio yenye mamlaka ya kuvunja
kamati ndogondogo za TFF, lakini kumbuka kuwa Mkutano Mkuu una mamlaka
zaidi ya Kamati ya Utendaji. Kwa sababu Malinzi alikuwa tayari amepewa
ridhaa ya mkutano mkuu kwa hiyo alichokifanya ni sawa.” Akifafanua
kuhusu madai kuwa wakati Malinzi anaomba ridhaa kwa Mkutano Mkuu, watu
wengine kama waandishi walikuwapo ukumbini, Ndumbaro alisema hilo halina
tatizo kwa sababu mkutano mkuu hauwezi kukosa uhalali kwa sababu ya
kuwapo kwa waandishi wa habari ukumbini.
“Kuwepo kwa waandishi wa habari au kutokuwapo ukumbini hakutengui mkutano mkuu,” alisema.
Kuhusu uamuzi wa Malinzi kufuta adhabu za watu
mbalimbali, Ndumbaro alisema hapo kunaweza kuwa na maswali ya kujiuliza
kwa sababu Katiba ya TFF haisemi lolote.
“Kuhusu kusamehe watu waliopewa adhabu na kamati
za TFF, Katiba haisemi kama anaweza kusamehe au kutosamehe. Hapo kidogo
panaacha maswali,” alisema Ndumbaro.
Lakini kundi jingine la wadau wa soka limedai Malinzi alikosea kwa sababu amevunja Katiba ya TFF.
Mmoja ya wadau wa soka nchini alidai kuwa hakuna
mtu mwenye mamlaka ya kutengua adhabu yoyote ambayo imetolewa na kamati
za kisheria kwani zipo huru.CHANZO MWANASPOTI
No comments:
Post a Comment