Kutokana
na hatua ya Samson Mwigamba, aliyesimamishwa uenyekiti wa CHADEMA Mkoa wa
Arusha, kukiri mbele ya waandishi wa habari kuwa amevunja katiba, kanuni,
maadili, miongozo, taratibu na itifaki za chama kwamba yeye ndiye aliyeandika
(kwa kutumia jina bandia);
Kwenye
mitandao ya kijamii, waraka uliojaa uongo, upotoshaji na uchonganishi kwa
wanachama na viongozi, Idara ya Habari ya CHADEMA (kupitia Ofisa Habari, ambaye
alikuwepo kwenye kikao hicho) imechukua hatua ya kuanza kutoa na kuandaa
utolewaji wa taarifa rasmi zinazojibu uongo, upotoshaji na uchonganishi
ulioandikwa na Mwigamba, ili kuweka kumbumbu sawa, wanachama na Watanzania wote
waelewe.
Kwa
kuanzia, leo tunatoa ufafanuzi juu ya suala la kikatiba la ukomo wa uongozi
ndani ya chama.
Kupitia
taarifa hii ya Idara ya Habari, kwanza tunapenda kushangazwa na hatua ya
Mwigamba kuendelea kuvunja katiba, kanuni, maadili, miongozo, taratibu na
itifaki ya chama, ambapo kupitia vyombo vya habari ameendelea kutunga mambo
yasiyokuwepo badala ya kuwasilisha hoja zake (kama anazo) kupitia vikao halali
vya chama ambavyo yeye anao uwezo wa kuitisha au kuhudhuria.
Tungependa
umma ufahamu masuala kadhaa, kwamba katika kikao cha Baraza la Uongozi wa Kanda
ya Kaskazini (Tanga, Manyara, Kilimnajaro a Arusha), muda mfupi kabla Mwigamba
hajatuhumiwa kwa usaliti na hujuma, alikuwa ametoka kuwasilisha taarifa ya hali
ya chama katika mkoa wa Arusha.
Kupitia
taarifa yake hiyo Mwigamba alisifia viongozi wa chama taifa kwa kusimamia
maslahi na matakwa ya Watanzania katika hoja au agenda mbalimbali pamoja na
kuendesha chama vizuri. Akamsifia Mbunge wa Arusha Mjini, kwa juhudi zake za
uenezi na uimarishaji wa chama.
Aidha baada ya kubainika kwa tuhuma hizo, pamoja na
uthibitisho uliokuwa chini ya waraka huo, uliotumika na wataalam wa kompyuta
kubainisha pasi na shaka kuwa waraka ule umetoka na umehifadhiwa kwenye
kompyuta yake, Mwigamba alipoulizwa alikana kabisa mbele ya kikao, akisema
hahusiki wala haijui ‘article’ ile ilitokea wapi, hadi alipolazimika kuandika
maelezo yake chini ya kiapo.
Jana mbele ya waandishi wa habari ameendelea
‘kugeuka-geuka’, akizungumza lugha tofauti tofauti kwenye suala moja.
Pili, kupitia taarifa hii kwa umma, Idara ya Habari ya
CHADEMA, inaweka hapa chini kumbukumbu sahihi juu ya kauli ya upotoshaji, uongo
na uchonganishi ya Mwigamba kuwa uongozi wa juu wa chama ‘umechakachua’ katiba
kwa kuondoa kipengele cha ukomo wa kushika madaraka ya uongozi ndani ya chama.
Kumbukumbu hii sahihi inatokana na ufafanuzi uliotolewa
katika mitandao ya kijamii (baada ya kuombwa na watu wengi) na Mkurugenzi wa
Habari na Uenezi, John Mnyika, ambaye alikuwa Katibu wa Kamati iliyohusika na
uandikaji upya wa Katiba ya CHADEMA ya mwaka 2006, ambayo ndiyo inatumika hadi
sasa.
Ufafanuzi wenyewe ni huu (una sehemu mbili, kwa nafasi yake,
pia maoni yake binafsi). Madai ya kwamba “Wakati tukifanya mabadiliko ya katiba
mwaka 2006 hatukugusa kipengele kinachomzuia kiongozi kuongoza kwenye nafasi
moja kwa zaidi ya vipindi viwili vya miaka mitanomitano. Lakini wakati katiba
inachapwa chini ya uongozi uliopo, kipengele hicho kiliondolewa kinyemela”;
hayana ukweli kwa kadiri ya ufahamu wangu.
Mosi, mwaka 2006 hatukufanya marekebisho ya katiba bali
tuliandika upya katiba ya chama kutoka ile ya mwaka 2004. Waraka uliandikwa
nchi nzima kwa wanachama kutoa maoni na kuwasilisha makao makuu kuanzia kwenye
ngazi zao za chini za kikatiba.
Baada ya kukusanya maoni kulikuwa na timu tatu, timu moja
ilihusu kuandika falsafa na itikadi ya chama ambayo Mwenyekiti wake alikuwa
Profesa Baregu na katibu wake nilikuwa mimi.
Sehemu hiyo ya katiba niliandika neno kwa neno mapendekezo
ya awali kwa kuzingatia mapendekezo yaliyotolewa, tulifanya mapitio pamoja na
Profesa Baregu na hatimaye ikaingia kwenye vikao vya kikatiba vya chama na
kupitishwa.
Sehemu ya falsafa kwa sehemu kubwa tulinukuu kwenye katiba
kama ilivyokuwa mwaka 2004, sehemu ya itikadi tuliandika upya kabisa haikuwepo
katika katiba ya CHADEMA ya zamani.
Sehemu zingine katika katiba kwa sehemu kubwa kazi ya kuunganisha
maoni mapya na kufanya pia rejea kwenye katiba ya zamani ilifanywa na timu ya
watu watatu tukiongozwa na muasisi wa chama Mzee Victor Kimesera pamoja na
Mkurugenzi Benson Kigaila na mimi.
Kulikuwa na timu nyingine ya kuandaa miongozo ya mabaraza ya
chama: Baraza la Wazee, BAVICHA na BAWACHA ambao nao walifanya kazi kwa upande
wao na nilishiriki katika kupendekeza mwelekeo na mapitio ya kulinganisha
rasimu ya miongozo yao na rasimu ya katiba ya chama.
Kwa ninavyokumbuka hicho kinachoitwa “kipengele kinachomzuia
kiongozi kuongoza kwenye nafasi moja kwa zaidi ya vipindi viwili vya miaka
mitano mitano” hakijawahi kuingizwa kwenye katiba mpya ya CHADEMA.
Baada ya timu zote kufanya kazi yake; rasimu ya katiba
ilipita katika vikao vyote vya kikatiba yaani sekretariati, kamati kuu, baraza
kuu na hatimaye mkutano mkuu. Katika vikao vyote hivyo, iwapo kipengele hicho
kingekuwa kimeondolewa ‘kinyemela’ kama inavyodaiwa, mwandishi wa tuhuma hiyo
angehoji toka Agosti 2006.
Aidha, baada ya katiba kupitishwa na kuanza kutumika kifungu
hicho kingekuwa kimeondolewa kinyemela kati ya mwaka 2006 mpaka 2008 mtoa madai
au mtu mwingine yeyote ndani ya chama angekuwa amehoji wakati wa matumizi.
Kumekuwepo pia mchakato wa kufanya marejeo kwa ajili ya kushughulikia makosa ya
uchapaji (errata) kwa nyakati mbalimbali, suala hili si kati ya mambo
yaliyoibuliwa.
Mwaka 2009 CHADEMA kilifanya uchaguzi mkuu wakae mkuu nchi
nzima ambapo vifungu vya masuala ya uchaguzi wa ndani ya chama vilifanyiwa
rejea mara kwa mara. Mwandishi wa madai hayo alikuwepo wakati huo, suala hili
la kwamba kuna kifungu kimeondolewa kinyemela sikulisikia likilalamikiwa kwenye
vikao vyovyote vya kikatiba iwe ni sekretariati, kamati kuu, baraza kuu na
mkutano mkuu.
Kwa vyovyote vile kwa historia ya chama toka mwaka
kilipoanzishwa mpaka wakati huo wa uchaguzi wapo viongozi ambao walikuwa
wanagombea wakiwa na vipindi viwili wakati huo kwenye cheo kimoja cha ngazi
moja; kifungu hicho kingekuwepo toka 2006 kingetumika kuwawekea mapingamizi. Na
kama kingekuwa ‘kimeondolewa kinyemela’ kungekuwa na malalamiko mengi kiko wapi
kwa kuzingatia ‘joto’ la uchaguzi wa wakati huo.
2010 mpaka 2013 madai hayo hayajawahi kutolewa kwenye kikao
chochote cha kikatiba katika ngazi ya taifa kwa kuwa mimi ni mjumbe wa vikao
vyote vya kitaifa ambavyo yeye amesema kwamba ni mjumbe.
Madai kama hayo yangetolewa na asiye mwanachama au walau
mwanachama wa kawaida tungesema tu ni maoni ya kawaida yaheshimiwe na
aelimishwe. Lakini madai kama hayo yakitolewa na kiongozi wa chama mwenye
nafasi ya kuujua ukweli wote huo yanaacha maswali kuhusu dhamira yake. Naamini
mamlaka zinazohusika za chama zitatumika katiba, kanuni, maadili na itifaki
kuchunguza na kuchukua hatua kuanzia kwenye ngazi yao huko tukio lilipotokea.
Maoni binafsi ya John Mnyika katika suala hili
Hata hivyo, kwa maoni binafsi (yasichukuliwe kuwa ni kauli
ya nafasi ninazoshikilia kwenye chama), dhamira ya haya inajionyesha kwenye
andiko lenyewe la muhusika kuanzia aya ya kwaza “ Kufuatia malumbano
yanayoendelea kwenye vyombo vya habari namadhaifu mengi ambayo
tumeshayashuhudia kwenye chama kwa sasa, natoa wito kwawana CHADEMA wote nchini
kwamba wakati umefika tubadilishe uongozi wa juu wachama.
Mtoa madai anaendelea kuandika kwamba “ Ni muhimu
wanachadema mkafahamu kwamba kitendo cha kuondolewa kwa kipengele hicho ndicho
kinacholeta mpasuko leo kwenye chama unaotokana na Mbowe na Zitto kupigania
uenyekiti. Kama kingekuwepoleo Mbowe alikuwa anakatazwa na katiba kugombea
kipindi cha tatu na hivyo vita iliyopo kati yake na Zitto isingekuwepo na chama
kingekuwa imara zaidi. Ni dhahiri Mbowe aliondoa kipengele hicho kwa makusudi
ili aweze kuendelea kugombea bila mwisho na huu ni udikteta kama ule tu wa
akina Lyatonga Mrema, John Cheyo na wengineo, na wanachadema hatupaswi
kuuruhusu si kwa Mbowe tu balikwa yeyote atakayepata nafasi ya kuwa mwenyekiti
wa chama chetu.
Anaendelea kuandika madai mengine mengi ya upotoshaji lakini
mwishoni anamalizia kwa dhamira yake ile ile “Nitaendelea kuwadondolea ili
muonekwa nini napendekeza tuung'oe uongozi huu chini ya Mbowe.”. Kwa hiyo,
dhamira yake ni uchaguzi na mabadiliko ya uongozi; dhamira yeyote njema ifuate
mkondo wa katiba, kanuni, maadili na itifaki; kinyume chake ni ‘njama ovu’ na
‘utovu wa maadili”.
Nimekuwepo chaguzi mbili kuu za CHADEMA 2004 (nikiwa
mtazamaji sio mwanachama) na 2009 nikiwa katikati ya chaguzi hizo kama
kiongozi. Naamini uchaguzi huu wa chama ulioanza kuanzia mwaka huu 2013
utakamilika mwaka 2014 CHADEMA ikiendelea kusimamia dhima yake ya kuleta
uongozi bora, sera sahihi, mikakati makini na oganizesheni thabiti kwa
maendeleo endelevu ya nchi yetu.
JJ
Imetolewa leo Jumanne, Oktoba 29, 2013 na;
Tumaini Makene
Ofisa Mwandamizi wa Habari-CHADEMA
No comments:
Post a Comment