Pages

Saturday, November 9, 2013

MAFANIKIO, CHANGAMOTO NA MIKAKATI YA TANROADS

IMG_9533_082a0.jpg
Mkuu wa Kitengo cha Habari wa Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) Bi. Aisha Aisha Malima akieleza kwa waandishi wa habari (hawapo pichani) kuhusu utekelezaji wa ukarabati na ujenzi wa barabara kenye mtandao wenye jumla ya kilometa 34,333 uliohusisha barabara kuu na barabara za Mikoa,wakati wa Mkutano uliofanyika ukumbi wa Idara ya Habari(MAELEZO) leo Jijini Dar es Salaam.Kushoto ni Mhandisai wa Mradi John Ngowi.
IMG_9537_61700.jpg
Mkuu wa Kitengo cha Mipango mkoa Dar es Salaam toka Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) Mhandisi Feya Malekela akieleza kwa waandishi wa habari (hawapo pichani) michakato mbalimbali inayopitiwa na wakala hao ikiwa kama barabara ipo chini ya kiwango ili kubaini chanzo cha tatizo.Kushoto ni Mkuu wa Kitengo cha Habari wa Wakala hao Bi. Aisha Malima
IMG_9545_f4204.jpg
Mhandisi wa Miradi toka Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) John Ngowi akieleza kwa waandishi wa habari (hawapo pichani) kuhusu mpango wa kutathimi barabara kwa kipindi cha miaka mitatu kabla ya kuipokea toka kwa mkandarasi ili kuhakikisha barabara zinazojengwa zinakidhi viwango.Kushoto ni Afisa Habari toka Idara ya Habari(MAELEZO) Georgina Misama.
Picha na Hassan Silayo-MAELEZO
TAARIFA KWA UMMA
MAFANIKIO, CHANGAMOTO NA MIKAKATI YA TANROADS
Moja ya mafanikio makubwa katika Sekta ya Barabara ni uanzishwaji wa Wakala wa Barabara nchini (Tanzania National Roads Agency – TANROADS). Wakala wa Barabara ulianzishwa chini ya Sheria Na. 30 ya mwaka 1997 (Executive Agencies Act No. 30/1997) na ulianza kazi mwezi wa Julai 2000.
Majukumu
Majukumu ya Wakala ni kuratibu na kusimamia matengenezo, ukarabati na ujenzi wa barabara kwenye mtandao wenye jumla ya kilometa 34,333 unaohusisha Barabara Kuu (km 12,204) na Barabara za Mikoa (km 22,126).
Wakala unajihusisha pia na usimamizi wa Karakana za Mitambo ya Barabara pamoja na Kitengo cha Maabara Kuu ya Vifaa na Maabara za Mikoa. Aidha, Wakala inajukumu la udhibiti wa uzito wa magari.
Mafanikio
Nchi yetu imepata mafanikio makubwa katika sekta ya barabara, sekta ambayo ina mchango muhimu katika kuinua uchumi wa Taifa kwa ujumla.
Mtandao wa barabara nchini umekuwa ukiboreshwa na kuongezeka kwa kuweka mkazo katika ujenzi na ukarabati wa Barabara Kuu na za Mikoa na Madaraja kwa lengo la kuleta uhakika na nafuu ya gharama za usafiri na usafirishaji nchini. Aidha, kipaumbele kimetolewa katika kutunza, kutengeneza na kukarabati barabara kupitia mipango na miradi mbalimbali iliyoandaliwa.
Mafanikio yaliyokwishapatikana tangu kuanzishwa kwa wakala hadi sasa ni pamoja na;
· Barabara zenye hali nzuri zimeongezeka kutoka 14% Machi 2003 hadi 39% Juni 2013.
· Barabara zenye hali ya wastani zimeongezeka kutoka 37% Machi 2003 hadi 47% Juni 2013
· Barabara zenye hali mbaya zimepungua kutoka 49% Machi 2013 hadi 14% Juni 2013.
Aidha mtandao wa Barabara za lami zilizo chini ya Wakala zimeongezeka kutoka kilometa 4,149 mwaka 2003 hadi kufikia kilometa 7,300 mwaka 2013. Hivi sasa zaidi ya kilometa 11,154 ziko katika hatua mbalimbali za ujenzi kwa kiwango cha lami.
Changamoto
TANROADS inakabiliwa na changamoto kadhaa katika utekelezaji wa majukumu yake.
· Moja ya changamoto kubwa ni kwamba barabara nyingi za nchi yetu bado za udongo au changarawe. Asilimia 21 % ya mtandao wa barabara wa nchi nzima ndiyo umewekewa lami, hivyo asilimia 79% bado ni barabara za udongo au changarawe. Hali hii inapelekea kuwa barabara zetu zinahitaji matengenezo ya mara kwa mara kuziweka katika hali nzuri, jambo linalogharimu Serikali yetu fedha nyingi.
· Uharibifu/wizi wa samani za barabara
· Uvamizi wa hifadhi ya barabara
· Magari kuzidisha uzito
· Uwezo mdogo wa wakandarasi kuweza kuhimili ushindani wa kimataifa
Mikakati
TANROADS imeweka mikakati madhubuti ili kufanikisha maendeleo katika sekta ya barabara.
(a) Wakala utaendelea kupunguza barabara za udongo au changarawe kwa kuzijenga kwa kiwango cha lami, zoezi ambalo linaendelea katika mikoa yote.
(b) Wakala kwa kushirikiana na wadau mbalimbali utaendelea kuwaelimisha wasafirishaji kuhusu umuhimu wa kutozidisha viwango vya uzito unaokubalika.
(c) Wakala kwa kushirikiana na taasisi nyingine utaeandelea kukuza uwezo wa Makandarasi na Wahandisi Washauri wa ndani kwa lengo la kuongeza mitaji, ujuzi na uzoefu ili waweze kuhimili ushindani wa kimataifa.
(d) Jitihadi zitaendelezwa kutoa elimu kwa wadau mbalimbali wa barabara ili kudhibiti uharibifu wa vifaa mbalimbali kama alama za barabarani, madaraja, barabara zenyewe pamoja uhifadhi wa miliki ya barabara.
TANROADS inawahakikishia Serikali, wadau wa maendeleo katika sekta ya barabara na wananchi kwa ujumla kuwa itaendelea kujenga na kutunza mtandao wa barabara zetu kwa gharama nafuu na katika namna endelevu ili kuendela kuchochea maendeleo ya kijamii na kiuchumi ya nchi yetu.
Barabara Bora kwa Maendeleo ya Taifa
Imetolewa na
Ofisi ya Habari
TANROADS
P.O. Box 11364
3rd Floor Airtel House
Makutano ya Barabara ya Ali Hassan Mwinyi/Kawawa
Dar es Salaam

No comments:

Post a Comment