Simon Msuva wa Yanga akimtoka Juma Nyosso wa Coastal Union leo Mkwakwani na chini ni kikosi cha Yanga leo Mkwakwani
BAADA
ya sare ya bila kufungana na Coastal Union Uwanja wa Mkwakwani mjini
Tanga jioni ya leo, kocha Mkuu wa Yanga SC, Mholanzi Hans van der Pluijm
amesema kwamba upepo mkali kwenye Uwanja huo uliwafanya washindwe
kucheza vizuri kipindi cha pili. Akizungumza
na Waandishi wa Habari baada ya mechi hiyo, kocha huyo wa zamani wa
Berekum Chelsea ya Ghana alisema kwamba kipindi cha kwanza walicheza
vizuri, lakini wakashindwa kutumia nafasi walizotengeneza.
“Tulipoteza
mechi kipindi cha kwanza tuliposhindwa kupata bao licha ya kutengeneza
nafasi nyingi. Kipindi cha pili tulishindwa kucheza mpira mzuri kutokana
na upepo mkali,”alisema. Kwa
upande wake, kocha wa Coastal, Mkenya Yussuf Chippo amesema kwamba sare
hiyo ni jambo jema kwake, kwani amepata pointi moja na hajapoteza
mechi. “Tulichea
vizuri kipindi cha pili, lakini bado tuna upungufu wa kutumia nafasi
tunazotengeneza. Tutalifanyia kazi suala hilo,”alisema mwalimu huyo wa
zamani wa Bandari ya Mombasa, Kenya na timu ya taifa ya Kenya, Harambee
Stars. Yanga
SC wameshushwa kileleni mwa ligi hiyo leo kufuatia kulazimishwa sare ya
bila kufungana na Coastal Union Uwanja wa Mkwakwani, Tanga. Matokeo
hayo yanaifanya Yanga itimize pointi 32 baada ya kucheza mechi 15 na
kuipisha Azam FC kileleni, ambayo imetimiza pointi 33 baada ya kuifunga
Rhino Rangers bao 1-0 leo. Yanga SC ilitawala mchezo kipindi cha kwanza na Coastal walitawala kipindi cha pili. Huo unakuwa mchezo wa nne Yanga SC kucheza chini ya kocha wake mpya, Mholanzi Hans van der Pluijm ikishinda mechi mmoja tu. Awali
Mholanzi huyo aliyefukuzwa fukuzwa timu kibao Ghana na St George ya
Ethiopia kwa matokeo mabaya kabla ya kutua Jangwani, alitoa sare mbili
katika ziara ya Uturuki na akashinda dhidi ya Ashanti United kwa taabu
2-1 Jumamosi katika Ligi Kuu.
|
No comments:
Post a Comment