Mwenyekiti wa Muda wa Bunge Maalumu la Bunge la Katiba Punda Ameir Kificho
KAMATI
iliyoteuliwa kushughulikia nyongeza ya posho kwa wajumbe wa Bunge
Maalumu la Katiba, imewasilisha mapendekezo kwa Rais Jakaya Kikwete,
ikisubiri maelekezo ya kuongezwa au la.
Akitoa
taarifa hiyo jana, Mwenyekiti wa Muda wa Bunge hilo, Pandu Ameir
Kificho, alieleza hadidu za rejea zilizoongoza kupatikana kwa
mapendekezo hayo ambayo hata hivyo hayajawekwa hadharani na kuomba
subira kwa wajumbe kwa mrejesho kutoka Ikulu.
Hata
hivyo, mapendekezo hayo yamepelekwa wakati wajumbe wa Baraza la
Wawakilishi Zanzibar, wakisubiri jibu kutoka Serikali ya Mapinduzi ya
Zanzibar (SMZ), kuhusu nyongeza ya posho ya kujikimu kutokana na kulipwa
posho ndogo kinyume na utaratibu waliozoea.
Nyuma ya
mapendekezo Kamati hiyo iliyoanza kazi Februari 19 na kuikamilisha juzi
katika utekelezaji wa jukumu lake, iliongozwa na mambo manne likiwamo la
uhalisia wa gharama za maisha mjini hapa.
Mengine
ambayo Kificho alisema yamezingatiwa katika kutafakari kabla ya
kuwasilisha mapendekezo kwa Rais, ni aina ya wajumbe walioteuliwa kwa
kuainisha pato lao kabla ya kuwa wajumbe wa Bunge.
Pia
sheria kuhusu taratibu za posho, uwazi wa posho zinavyotolewa na
ulinganisho wa malipo ya kuzingatia aina za wajumbe. “Kama nilivyoeleza,
suala la masharti ya mjumbe yako kwenye mamlaka ya aliyetoa (Rais).
Kamati
baada ya kujiridhisha imewasilisha mapendekezo yake kwenye mamlaka hiyo,
ili itafakari mapendekezo hayo na kutoa maelekezo.
“Hivyo
waheshimiwa wabunge nawaomba sana muwe na subira wakati huu hadi
tutakapopata maelekezo mengine juu ya jambo hili ambalo mmelitoa,”
alisema Kificho.
Alitaka
wajumbe waiachie Kamati hiyo ya uongozi kazi hiyo akisisitiza kwamba pia
wao wanakamati, ni wadau wa suala hilo la kutaka kuongezwa posho.
Kamati
hiyo inaundwa na Kificho, William Lukuvi, Freeman Mbowe, Paul Kimiti,
Jenista Mhagama, Mohamed Aboud Mohamed na Asha Bakari Makame.
Msimamo wa Zanzibar
Mwishoni
mwa wiki, Katibu wa Baraza la Wawakilishi, Yahya Khamis Hamad, alisema
wajumbe wa Bunge la Katiba ambao ni wawakilishi bado wanadai nyongeza ya
posho.
“Kweli walidai na wanaendelea kudai baada ya kuona posho ya kujikimu katika Bunge Maalumu ni Sh 80,000,” alisema Hamad.
Alifafanua,
kwamba hoja ya wawakilishi hao 82 ya kuomba nyongeza ni kwamba,
kiutaratibu, wanapokuwa kazini nje ya SMZ, posho wanayostahili kulipwa
ni Sh 200,000.
Hivyo
baada ya kufika kwenye Bunge Maalumu na kubaini posho ya kujikimu ni Sh
80,000, waliwasilisha maombi waongezwe kiasi kinachopungua, ambacho ni
Sh 120,000 ili ifike Sh 200,000 kwa siku.
“Serikali
haijajibu…lakini kwa mtazamo wangu, naona hizo fedha wanazoomba hakuna
uwezekano, kwa sababu niliambiwa niangalie kwenye fungu langu, na mimi
fungu langu haliwezekani kwa sababu nina matumizi mengine,” alisema
Katibu wa Baraza.
Wanaopinga
Wakati
taarifa hiyo ikitolewa jana, kulikuwa na mpango wa baadhi ya wajumbe ,
wakiongozwa na Julius Mtatiro, kujiorodhesha majina na kusaini kwa lengo
la kwenda kwa Rais kupinga ongezeko hilo.
Hata
hivyo, Mtatiro aliyekuwa kwenye harakati hizo, alimwambia mwandishi wa
habari hizi, kwamba amesitisha mpango huo baada ya kuhakikishiwa kwamba
maombi hayo ya kuongezwa posho yamegonga mwamba kwa mamlaka husika.
“Tuna
uhakika suala la nyongeza ya posho limegonga mwamba. Tumeona hakuna haja
ya kuendelea kukusanya saini…tulitaka Kamati ikipeleka maombi ya posho
kwa Rais, na sisi tungepeleka majina yetu kupinga isiongezwe,” alisema
Mtatiro.
Licha ya
Mtatiro, wabunge wengine waliopinga hadharani ongezeko hilo, ni Zitto
Kabwe, aliyesema posho ikiongezwa hataipokea. Mwingine ni Mohamed Kessy
aliyeita madai hayo ya nyongeza kuwa ni unyonyaji kwa wananchi.
Mchungaji
Israel Natse alisema Katiba ni suala la kitaifa lenye maslahi kwa
wananchi ambalo hata wangeambiwa kufanya kazi bila malipo, walipaswa
kuifanya.
Wakati
baadhi ya wabunge wakijitokeza hadharani kuzungumza na waandishi wa
habari kupinga nyongeza hiyo kwa kutaka Rais Kikwete asiidhinishe, wapo
ambao gazeti hili limebaini wanatumia mitandao ya kijamii kujiengua
miongoni mwa wanaotaka nyongeza.
Gharama
Dodoma
Wakati miongoni mwa mambo ambayo kamati imetafakari ni kuhusu gharama za
maisha mjini Dodoma, wajumbe wasiokubaliana na nyongeza, walisema Sh
300,000 kwa siku zinatosha.
“Tumekuwa
bungeni, nimekuwa mbunge, tunalipwa Sh 170,000 kwa siku. Kima cha chini
ni Sh ngapi, walimu wanapata Sh ngapi kwa siku wanaishi na wana wake na
watoto? Bunge hili tulikuwa tukilipwa Sh ngapi? Nyie hamwoni huruma kwa
wananchi wenu?” Alihoji Kessy.
Kessy
alisema ingekuwa vizuri kama bei ya hoteli, chakula, usafiri na matumizi
mengine zingechanganuliwa, ili wajumbe wavune jasho lao kwa kulipwa
wanachostahili kuliko kuumiza wananchi.
Zitto
alisema; “Ni jukumu lenu waandishi wa habari kufanya uchunguzi (wa
gharama halisi za matumizi Dodoma ). Kuna wabunge wanakaa kwenye hoteli
mnazokaa, kuna wabunge wanakula sehemu mnazokula, nyie mnalipwa Sh
ngapi?” Maisha yao Gazeti hili limebaini wajumbe walio wengi wanalala
kwenye nyumba za wageni zinazotoza kati ya Sh 15,000 na 40,000 kwa siku.
Wapo
wengine ambao mwandishi alibaini wamefikia kwa ndugu na jamaa zao. Kwa
upande wa chakula, mbali na mgahawa wa bungeni na mingine ambayo bei za
chakula zinaanzia Sh 4,000 kwa sahani, wajumbe wengine wamekuwa
wakikutwa katika vibanda vya kawaida mitaani.
“Kama
tutaongezwa, sawa. Lakini sisi ni watu wa kawaida, huko nyumbani
tunaishi maisha ya kawaida. Labda hawa wenzetu wabunge (la kawaida) na
mawaziri, hawawezi kujichanganya Uswahilini,” alisema mjumbe ambaye
hakutaka jina lake liandikwe gazetini.
Vivyo
hivyo, gharama za usafiri, kwa wanaotumia teksi, wastani wake ni Sh
7,000 kwa safari ya mbali, hivyo kwenda na kurudi ni Sh 14,000 wakati
kwa safari za masafa mafupi ni Sh 3,000 na hivyo kwenda na kurudi ni Sh
6,000.
Pato la wajumbe
Kamati hiyo katika kujadili, pia ilizingatia aina ya wajumbe walioteuliwa kwa kuainisha pato lao kabla ya kuwa wajumbe wa Bunge.
Bunge
hilo Maalumu linaundwa na watu wa kada tofauti wakiwamo wakulima,
wafugaji, wafanyakazi, wabunge, wawakilishi, viongozi wa dini, watendaji
katika mashirika yasiyo ya serikali (NGOs) na wafanyabiashara.
Katika
mjadala unaoendelea kuhusu posho kupitia vyombo vya habari, mitandao ya
kijamii na kwenye jamii, wananchi wanahoji kama kuna mfanyakazi
anayelipwa mshahara wa Sh milioni tisa kwa mwezi.
Wengine
wanahoji iwapo wajumbe hao wamelazimishwa kushiriki Bunge hilo na kama
Sh 300,000 kwa siku ni ndogo kwa maana kwamba wanapata hasara kwa kuacha
shughuli zao, waachie wanaoweza wafanye kazi hiyo.
Zitto alisema ingekuwa inawezekana, wangeteua eneo kama vile Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM) wakajifungia na kutengeneza Katiba.
Chimbuko la hoja
Siku ya
pili ya kikao cha Bunge Maalumu, Richard Ndassa Mbunge wa Sumve, ndiye
aliibua suala hilo la posho akisema Sh 300,000 kwa siku wanayolipwa
wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba ni ndogo.
Pia alidai wajumbe wa Baraza la Wawakilishi wameongezwa posho na SMZ jambo ambalo linaleta tofauti bungeni.
Akiungwa
mkono na Suleiman Nchambi, walihoji sababu za wao kupewa posho hiyo
wakati wajumbe wa Tume ya Marekebisho ya Katiba walilipwa Sh 500,000
walipokuwa wakikusanya maoni.
Kwa
mujibu wa wanaotaka nyongeza, mchanganuo wa matumizi yao ni kwamba hadhi
ya hoteli wanayopaswa kulala ni ya kuanzia Sh 70,000. Pia wanahitaji
mafuta ya gari, kulipa madereva na kutoa fedha kwa watu mbalimbali
wanaowaomba msaada.
Mwigulu
Akizungumza
jana wakati wa kuhitimisha semina ya viongozi na watendaji wa Jumuiya
ya Wazazi Ngazi ya Taifa, mikoa na wilaya nchini, iliyofanyika kwenye
ukumbi wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM mjini Dodoma, Naibu Waziri wa
Fedha, Mwigulu Nchemba, alihoji huo ujasiri wa wajumbe kutaka posho
umetoka wapi.
Alisema
wajumbe hao si washauri wataalamu kutoka Kenya wala Uingereza mpaka
wadai posho kubwa, wakati wanatoka kwa wakulima, wavuvi na watu wengine
wa kawaida na walitarajiwa kuonesha uzalendo.
Aliendelea
kushangaa madai ya nyongeza ya posho wakati walimu wana malimbikizo ya
malipo yao ambayo hayajalipwa, wakulima wameuza mazao yao kwa Wakala wa
Hifadhi ya Chakula (NFRA) nao pia hawajalipwa.
Mwigulu
aliendelea kuhoji wajumbe hao wanapata wapi ujasiri huo, wakati kuna
wananchi vijijini wanaamka na uji asubuhi na kusubiri cha jioni huku
wengine wakifa hospitalini kwa kukosa dawa.
Alisema
alitarajia baada ya kuteuliwa, wajumbe hao wangekuwa wameshiba tayari
kwa kuwa hata mwanajeshi anapokwenda vitani, anajua kuna kifo lakini
anakwenda kwa kuwa anatumikia Taifa.
CHANZO:HABARILEO
No comments:
Post a Comment