Pages

Wednesday, February 26, 2014

MAPENDEKEZO ya POSHO za BUNGE YATUA KWA JK

pandu-ameir-kificho_d9f29.jpg
Mwenyekiti  wa Muda  wa Bunge Maalumu la Bunge la Katiba Punda Ameir Kificho 
KAMATI iliyoteuliwa kushughulikia nyongeza ya posho kwa wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba, imewasilisha mapendekezo kwa Rais Jakaya Kikwete, ikisubiri maelekezo ya kuongezwa au la.
Akitoa taarifa hiyo jana, Mwenyekiti wa Muda wa Bunge hilo, Pandu Ameir Kificho, alieleza hadidu za rejea zilizoongoza kupatikana kwa mapendekezo hayo ambayo hata hivyo hayajawekwa hadharani na kuomba subira kwa wajumbe kwa mrejesho kutoka Ikulu.

Hata hivyo, mapendekezo hayo yamepelekwa wakati wajumbe wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar, wakisubiri jibu kutoka Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ), kuhusu nyongeza ya posho ya kujikimu kutokana na kulipwa posho ndogo kinyume na utaratibu waliozoea.
Nyuma ya mapendekezo Kamati hiyo iliyoanza kazi Februari 19 na kuikamilisha juzi katika utekelezaji wa jukumu lake, iliongozwa na mambo manne likiwamo la uhalisia wa gharama za maisha mjini hapa.
Mengine ambayo Kificho alisema yamezingatiwa katika kutafakari kabla ya kuwasilisha mapendekezo kwa Rais, ni aina ya wajumbe walioteuliwa kwa kuainisha pato lao kabla ya kuwa wajumbe wa Bunge.
Pia sheria kuhusu taratibu za posho, uwazi wa posho zinavyotolewa na ulinganisho wa malipo ya kuzingatia aina za wajumbe. “Kama nilivyoeleza, suala la masharti ya mjumbe yako kwenye mamlaka ya aliyetoa (Rais).
Kamati baada ya kujiridhisha imewasilisha mapendekezo yake kwenye mamlaka hiyo, ili itafakari mapendekezo hayo na kutoa maelekezo.
“Hivyo waheshimiwa wabunge nawaomba sana muwe na subira wakati huu hadi tutakapopata maelekezo mengine juu ya jambo hili ambalo mmelitoa,” alisema Kificho.
Alitaka wajumbe waiachie Kamati hiyo ya uongozi kazi hiyo akisisitiza kwamba pia wao wanakamati, ni wadau wa suala hilo la kutaka kuongezwa posho.
Kamati hiyo inaundwa na Kificho, William Lukuvi, Freeman Mbowe, Paul Kimiti, Jenista Mhagama, Mohamed Aboud Mohamed na Asha Bakari Makame.
Msimamo wa Zanzibar
Mwishoni mwa wiki, Katibu wa Baraza la Wawakilishi, Yahya Khamis Hamad, alisema wajumbe wa Bunge la Katiba ambao ni wawakilishi bado wanadai nyongeza ya posho.
“Kweli walidai na wanaendelea kudai baada ya kuona posho ya kujikimu katika Bunge Maalumu ni Sh 80,000,” alisema Hamad.
Alifafanua, kwamba hoja ya wawakilishi hao 82 ya kuomba nyongeza ni kwamba, kiutaratibu, wanapokuwa kazini nje ya SMZ, posho wanayostahili kulipwa ni Sh 200,000.
Hivyo baada ya kufika kwenye Bunge Maalumu na kubaini posho ya kujikimu ni Sh 80,000, waliwasilisha maombi waongezwe kiasi kinachopungua, ambacho ni Sh 120,000 ili ifike Sh 200,000 kwa siku.
“Serikali haijajibu…lakini kwa mtazamo wangu, naona hizo fedha wanazoomba hakuna uwezekano, kwa sababu niliambiwa niangalie kwenye fungu langu, na mimi fungu langu haliwezekani kwa sababu nina matumizi mengine,” alisema Katibu wa Baraza.
Wanaopinga
Wakati taarifa hiyo ikitolewa jana, kulikuwa na mpango wa baadhi ya wajumbe , wakiongozwa na Julius Mtatiro, kujiorodhesha majina na kusaini kwa lengo la kwenda kwa Rais kupinga ongezeko hilo.
Hata hivyo, Mtatiro aliyekuwa kwenye harakati hizo, alimwambia mwandishi wa habari hizi, kwamba amesitisha mpango huo baada ya kuhakikishiwa kwamba maombi hayo ya kuongezwa posho yamegonga mwamba kwa mamlaka husika.
“Tuna uhakika suala la nyongeza ya posho limegonga mwamba. Tumeona hakuna haja ya kuendelea kukusanya saini…tulitaka Kamati ikipeleka maombi ya posho kwa Rais, na sisi tungepeleka majina yetu kupinga isiongezwe,” alisema Mtatiro.
Licha ya Mtatiro, wabunge wengine waliopinga hadharani ongezeko hilo, ni Zitto Kabwe, aliyesema posho ikiongezwa hataipokea. Mwingine ni Mohamed Kessy aliyeita madai hayo ya nyongeza kuwa ni unyonyaji kwa wananchi.
Mchungaji Israel Natse alisema Katiba ni suala la kitaifa lenye maslahi kwa wananchi ambalo hata wangeambiwa kufanya kazi bila malipo, walipaswa kuifanya.
Wakati baadhi ya wabunge wakijitokeza hadharani kuzungumza na waandishi wa habari kupinga nyongeza hiyo kwa kutaka Rais Kikwete asiidhinishe, wapo ambao gazeti hili limebaini wanatumia mitandao ya kijamii kujiengua miongoni mwa wanaotaka nyongeza.
Gharama
Dodoma Wakati miongoni mwa mambo ambayo kamati imetafakari ni kuhusu gharama za maisha mjini Dodoma, wajumbe wasiokubaliana na nyongeza, walisema Sh 300,000 kwa siku zinatosha.
“Tumekuwa bungeni, nimekuwa mbunge, tunalipwa Sh 170,000 kwa siku. Kima cha chini ni Sh ngapi, walimu wanapata Sh ngapi kwa siku wanaishi na wana wake na watoto? Bunge hili tulikuwa tukilipwa Sh ngapi? Nyie hamwoni huruma kwa wananchi wenu?” Alihoji Kessy.
Kessy alisema ingekuwa vizuri kama bei ya hoteli, chakula, usafiri na matumizi mengine zingechanganuliwa, ili wajumbe wavune jasho lao kwa kulipwa wanachostahili kuliko kuumiza wananchi.
Zitto alisema; “Ni jukumu lenu waandishi wa habari kufanya uchunguzi (wa gharama halisi za matumizi Dodoma ). Kuna wabunge wanakaa kwenye hoteli mnazokaa, kuna wabunge wanakula sehemu mnazokula, nyie mnalipwa Sh ngapi?” Maisha yao Gazeti hili limebaini wajumbe walio wengi wanalala kwenye nyumba za wageni zinazotoza kati ya Sh 15,000 na 40,000 kwa siku.
Wapo wengine ambao mwandishi alibaini wamefikia kwa ndugu na jamaa zao. Kwa upande wa chakula, mbali na mgahawa wa bungeni na mingine ambayo bei za chakula zinaanzia Sh 4,000 kwa sahani, wajumbe wengine wamekuwa wakikutwa katika vibanda vya kawaida mitaani.
“Kama tutaongezwa, sawa. Lakini sisi ni watu wa kawaida, huko nyumbani tunaishi maisha ya kawaida. Labda hawa wenzetu wabunge (la kawaida) na mawaziri, hawawezi kujichanganya Uswahilini,” alisema mjumbe ambaye hakutaka jina lake liandikwe gazetini.
Vivyo hivyo, gharama za usafiri, kwa wanaotumia teksi, wastani wake ni Sh 7,000 kwa safari ya mbali, hivyo kwenda na kurudi ni Sh 14,000 wakati kwa safari za masafa mafupi ni Sh 3,000 na hivyo kwenda na kurudi ni Sh 6,000.
Pato la wajumbe
Kamati hiyo katika kujadili, pia ilizingatia aina ya wajumbe walioteuliwa kwa kuainisha pato lao kabla ya kuwa wajumbe wa Bunge.
Bunge hilo Maalumu linaundwa na watu wa kada tofauti wakiwamo wakulima, wafugaji, wafanyakazi, wabunge, wawakilishi, viongozi wa dini, watendaji katika mashirika yasiyo ya serikali (NGOs) na wafanyabiashara.
Katika mjadala unaoendelea kuhusu posho kupitia vyombo vya habari, mitandao ya kijamii na kwenye jamii, wananchi wanahoji kama kuna mfanyakazi anayelipwa mshahara wa Sh milioni tisa kwa mwezi.
Wengine wanahoji iwapo wajumbe hao wamelazimishwa kushiriki Bunge hilo na kama Sh 300,000 kwa siku ni ndogo kwa maana kwamba wanapata hasara kwa kuacha shughuli zao, waachie wanaoweza wafanye kazi hiyo.
Zitto alisema ingekuwa inawezekana, wangeteua eneo kama vile Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM) wakajifungia na kutengeneza Katiba.
Chimbuko la hoja
Siku ya pili ya kikao cha Bunge Maalumu, Richard Ndassa Mbunge wa Sumve, ndiye aliibua suala hilo la posho akisema Sh 300,000 kwa siku wanayolipwa wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba ni ndogo.
Pia alidai wajumbe wa Baraza la Wawakilishi wameongezwa posho na SMZ jambo ambalo linaleta tofauti bungeni.
Akiungwa mkono na Suleiman Nchambi, walihoji sababu za wao kupewa posho hiyo wakati wajumbe wa Tume ya Marekebisho ya Katiba walilipwa Sh 500,000 walipokuwa wakikusanya maoni.
Kwa mujibu wa wanaotaka nyongeza, mchanganuo wa matumizi yao ni kwamba hadhi ya hoteli wanayopaswa kulala ni ya kuanzia Sh 70,000. Pia wanahitaji mafuta ya gari, kulipa madereva na kutoa fedha kwa watu mbalimbali wanaowaomba msaada.
Mwigulu
Akizungumza jana wakati wa kuhitimisha semina ya viongozi na watendaji wa Jumuiya ya Wazazi Ngazi ya Taifa, mikoa na wilaya nchini, iliyofanyika kwenye ukumbi wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM mjini Dodoma, Naibu Waziri wa Fedha, Mwigulu Nchemba, alihoji huo ujasiri wa wajumbe kutaka posho umetoka wapi.
Alisema wajumbe hao si washauri wataalamu kutoka Kenya wala Uingereza mpaka wadai posho kubwa, wakati wanatoka kwa wakulima, wavuvi na watu wengine wa kawaida na walitarajiwa kuonesha uzalendo.
Aliendelea kushangaa madai ya nyongeza ya posho wakati walimu wana malimbikizo ya malipo yao ambayo hayajalipwa, wakulima wameuza mazao yao kwa Wakala wa Hifadhi ya Chakula (NFRA) nao pia hawajalipwa.
Mwigulu aliendelea kuhoji wajumbe hao wanapata wapi ujasiri huo, wakati kuna wananchi vijijini wanaamka na uji asubuhi na kusubiri cha jioni huku wengine wakifa hospitalini kwa kukosa dawa.
Alisema alitarajia baada ya kuteuliwa, wajumbe hao wangekuwa wameshiba tayari kwa kuwa hata mwanajeshi anapokwenda vitani, anajua kuna kifo lakini anakwenda kwa kuwa anatumikia Taifa.
CHANZO:HABARILEO

No comments:

Post a Comment