Kifuko
kilichobeba Bajeti ya Serikali
Wakati
Serikali ikiwa taabani kifedha, wabunge wengi, wakiwamo wajumbe wa Kamati ya
Bunge ya Bajeti wanapanga kukwamisha Bajeti Kuu ya Serikali, inayofikia zaidi
ya Sh19 trilioni.
Habari
kutoka ndani ya vikao vya Kamati ya Bunge ya Bajeti, zinadai kuwa iwapo
Serikali haitapunguza misamaha ya kodi hadi asilimia moja ya pato la taifa
(GDP), wabunge hao watakwamisha bajeti hiyo.
Mbunge
wa Mwibara, Kangi Lugola (CCM), alilithibitishia gazeti hili jana kuwa yeye ni
miongoni mwa wabunge waliopanga kukwamisha bajeti hiyo na yuko tayari kufukuzwa
ubunge kwa hilo.
Lugola
alisema kuwa pamoja na kuwepo kanuni inayowakataza wabunge wa CCM kukwamisha
bajeti na anayefanya hivyo hufukuzwa, yuko tayari afukuzwe ili ayaponye maisha
ya Watanzania milioni 45.
“Kila mwaka tunapiga kelele misamaha ya kodi,
wanatumia mwanya huo vibaya na matokeo yake bajeti za Serikali mwaka hadi mwaka
hazipati fedha kutoka Hazina,” alisema Lugola na kuongeza:
“Kama
hakuna fedha, halafu tunatoa misamaha kiholela, basi ni afadhali bajeti ya
mwaka huu tuzibe hiyo mianya, futa kabisa hiyo misamaha isiyo na tija.”
Lugola
alisisitiza: “Hatuwezi kuendesha nchi kwa staili hiyo, lazima tufike mahali
mambo ya kuwekeana kanuni kuwa tukikwamisha bajeti Bunge litavunjwa, acha
livunjwe ili kuliponya taifa.”
Lugola
alisema kama Serikali haitakuja na mwarobaini wa misamaha ya kodi, ukwepaji wa
kodi, matumizi makubwa ya Serikali na kupambana na ufisadi na wizi, bungeni
hapatatosha.
Mbunge
wa Kasulu Mjini, Moses Machali (NCCR-Mageuzi), jana alisema kuwa angetamani
kama Bajeti ya Serikali isipite mwaka huu ili wabunge watimize wajibu wao wa
kikatiba wa kuisimamia Serikali.
“Nenda
kwenye Ripoti za CAG, madudu ni yaleyale mwaka hadi mwaka, misamaha ya kodi
ndiyo usiseme, matumizi ya anasa ndiyo balaa. Nchi inakwenda wapi?” alihoji
Machali na kuongeza:
“Kama
kweli wabunge wanaitakia mema nchi hii, tuungane, kama Serikali haiji na majibu
ya madudu yote haya tusipitishe bajeti hii. Tuweke historia ambayo vizazi
vijavyo vitatukumbuka.”
Wakati
wabunge wengi wakipanga kukwamisha bajeti iwapo misamaha hiyo haitapunguzwa
hadi asilimia 1 ya GDP, hadi kufikia Juni 30, 2013 misamaha hiyo ilikuwa Sh1.52
trilioni.
CAG
Mdhibiti
na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Ludovick Utouh alikaririwa akisema
kuwa misamaha hiyo imepungua kwa asilimia 16 kutoka Sh1.81 trilioni mwaka
2011/2012 hadi Sh1.52 trilioni.
Mjumbe
mmoja wa Kamati ya Bajeti, alisema wameapa kupambana ili misamaha hiyo ishuke
hadi asilimia moja ya GDP na kwamba hakuna mantiki kwa nchi iliyo taabani
kifedha kutoa misamaha ya kodi. “Tunataka hata hiyo asilimia moja ambayo
tunataka ifikie, iwe ni misamaha yenye tija na tumesema wasipokuja na suala
hilo hatutapitisha bajeti kwenye kamati na bungeni,”alidokeza.
Mkakati
huo wa Kamati ya Bajeti na Bunge, umekuja katika kipindi ambacho harakati nzito
za kukwamisha Muswada wa Sheria wa Kuondoa Misamaha ya Kodi kwenye VAT
zikiendelea.
Zitto
Mwenyekiti
wa Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC), Kabwe Zitto alisema baadhi ya
wafanyabiashara wakubwa wanaonufaika na misamaha hiyo wanajipanga kukwamisha
muswada huo.
Kwa
mujibu wa Zitto, kama sheria hiyo ya VAT itafanyiwa marekebisho, ni dhahiri
makundi hayo yanayonufaika na misamaha
ya kodi yataathirika na ndiyo maana yameungana kuikwamisha.
Mbali
na kuwepo kwa sintofahamu hiyo, lakini wajumbe hao wameonyesha kutoridhishwa na
utendaji kazi wa Waziri wa Fedha, Saada Mkuya anayedaiwa kuhudhuria kikao
kimoja tu cha kamati.
“Nchi
iko katika wakati mgumu kifedha, Waziri wa Fedha anakwenda Rwanda kuhudhuria
kikao cha watu 3,000, badala ya kubaki Dodoma kutetea bajeti yake ya Sh19
trilioni,”alidai mjumbe mmoja.
Wajumbe
wa kamati hiyo wanadai kuwa Mkuya amekuwa akiwatuma Naibu Mawaziri wake,
Mwigulu Nchemba na Adam Malima ambao ni wageni wizarani kushiriki vikao vya
Kamati ya Bajeti yeye akiwa safarini .
Mmoja
wa wajumbe wa kamati hiyo aliyeomba jina lake lihifadhiwe, alidai hali ya
kifedha ya Serikali ni mbaya na kwamba alitarajia Waziri wa Fedha angekuwapo
Dodoma muda wote ili kuweka mikakati ya kuinusuru.
“Bajeti
ya mwaka jana (2013/2014), ina deficit (upungufu) ya Sh1.8 trilioni, kwa maneno
mengine kuna miradi ya maendeleo yenye thamani hiyo haikutekelezwa kabisa,”
alidokeza mjumbe huyo.
Mjumbe
mwingine alidai kuwa Serikali ina madeni makubwa ya mwaka jana, ambayo inataka
kuyahamishia katika bajeti ya mwaka huu (2014/2015), ambayo itaathiri kwa kiasi
kikubwa miradi ya maendeleo.
“Tunafahamu
wabunge wanachachamaa, wanataka zile fedha tulizoidhinisha mwaka jana zitolewe
kwanza ziende kwenye miradi, lakini tofauti na hivyo bungeni
hapatatosha,”alidai mjumbe huyo.
Moja
kati ya mambo ambayo Kamati ya Bajeti imeibana Serikali ni pamoja na kuitaka
kubana matumizi makubwa na mengine ya anasa na kudhibiti mianya ya ukwepaji wa
kodi. “Pale bandarini kuna mabilioni ya kodi yanakwepwa na tunaambiwa baadhi ya
kampuni zina uhusiano na vigogo wa Serikali, wakitaka kukusanya kodi, vinakuja
vimemo,”ilidokezwa.
Ukweli
wa Serikali kuwa taabani kifedha unathibitishwa na namna wizara zilivyopokea
fedha za maendeleo mwaka 2013/2014, ambapo baadhi zilipata kati ya asilimia 20
na 30.
Wizara
ya Mifugo
Mathalan,
Wizara ya Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi iliidhinishiwa Sh28.9 bilioni, lakini
ilipokea Sh2.5 bilioni tu sawa na asilimia 13.4 wakati Wizara ya Katiba na
Sheria ilipokea Sh9.9 sawa na asilimia 17.
Hali
imeendelea kuwa hivyo katika Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi ambapo
iliidhinishiwa Sh741.1 bilioni kwa ajili ya matumizi ya kawaida na miradi ya
maendeleo, lakini imepokea asilimia 67 tu.
Katika
mwaka unaomalizikia Juni 30, Bunge liliidhinisha Sh81 bilioni kwa ajili ya
miradi ya maendeleo, lakini hadi kufikia Machi 31, mwaka huu ilikuwa imepokea
Sh40.8 bilioni sawa na asilimia 50.38.
Wizara
ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa (JKT), iliidhinishiwa Sh245.5 bilioni kwa
ajili ya maendeleo, lakini hadi kufikia Machi 30 mwaka huu, ilikuwa imepokea
Sh49.3 bilioni sawa na asilimia 20.1.
Mbali
na wizara hiyo, Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto ilikuwa
imeidhinishiwa Sh11.9 bilioni za miradi ya maendeleo, lakini hadi kufikia Machi
ilipokea Sh2.9 bilioni pekee.
Kwa
upande wake, Wizara ya Ujenzi iliidhinishiwa Sh845 bilioni kwa ajili ya miradi
ya maendeleo, lakini hadi kufikia mwezi Machi, 2014 ilikuwa imepokea Sh604.4
bilioni sawa na asilimia 71.52.
Bajeti
ya Wizara ya Maji na ile ya Nishati na Madini ilibidi zisogezwe mbele kama njia
ya kusubiri hali ya hewa itulie baada ya wabunge wengi kujipanga kuzikwamisha.
Mbunge
Keissy
.Mbunge
wa Nkasi Kaskazini, Ally Keissy Mohamed (CCM), alisema suala hapa si kupunguzwa
kwa misamaha ya kodi, bali ni kuifuta kabisa kwa kuwa hakuna mantiki kwa
Serikali kudai haina pesa huku ikisamehe kodi.
“Mimi
naunga mkono suala hili kwa kweli na mimi katika hili nitaibana Serikali tufute
kabisa hii misamaha ya kodi na kwa kweli Serikali ibane matumizi… ina matumizi
makubwa na sherehe kubwa,”alisema.
Mbunge
wa Kinondoni, Idd Azzan (CCM), alisema kama ingewezekana, Serikali ingefuta
misamaha ya kodi angalau kwa mwaka mmoja hasa katika kipindi hiki ambacho
Serikali inapitia kipindi kigumu cha bajeti. Kwa upande wake, Mbunge wa
Mkanyageni, Mohamed Habib Mnyaa (CUF), alisema hoja ya baadhi ya wabunge wa CCM
kupanga kuikataa bajeti ni kiini macho tu, kwani hawana ubavu huo.
“Baadhi
ya wabunge wa CCM wamewasaliti wapiga kura wao… badala ya kuisimamia Serikali
kama Katiba inavyosema, wao wamegeuka watetezi wa Serikali… Nchi hii haiendi
kwa sababu hiyo,”alisema Mnyaa.
Mnyaa
alisema ijapokuwa wabunge wangeweka historia ya kuisimamia Serikali kwa
kukwamisha bajeti, lakini wabunge wanaotokana na CCM hawawezi kufika huko,
kwani wanahofu wakifanya hivyo Rais atalivunja Bunge na wao hawako tayari.
Chanzo:Mwananchi
No comments:
Post a Comment