Pages

Monday, May 26, 2014

BAJETI KUU HATI HATI

Kifuko kilichobeba Bajeti ya Serikali

Wakati Serikali ikiwa taabani kifedha, wabunge wengi, wakiwamo wajumbe wa Kamati ya Bunge ya Bajeti wanapanga kukwamisha Bajeti Kuu ya Serikali, inayofikia zaidi ya Sh19 trilioni.
Habari kutoka ndani ya vikao vya Kamati ya Bunge ya Bajeti, zinadai kuwa iwapo Serikali haitapunguza misamaha ya kodi hadi asilimia moja ya pato la taifa (GDP), wabunge hao watakwamisha bajeti hiyo.
Mbunge wa Mwibara, Kangi Lugola (CCM), alilithibitishia gazeti hili jana kuwa yeye ni miongoni mwa wabunge waliopanga kukwamisha bajeti hiyo na yuko tayari kufukuzwa ubunge kwa hilo.
Lugola alisema kuwa pamoja na kuwepo kanuni inayowakataza wabunge wa CCM kukwamisha bajeti na anayefanya hivyo hufukuzwa, yuko tayari afukuzwe ili ayaponye maisha ya Watanzania milioni 45.
 “Kila mwaka tunapiga kelele misamaha ya kodi, wanatumia mwanya huo vibaya na matokeo yake bajeti za Serikali mwaka hadi mwaka hazipati fedha kutoka Hazina,” alisema Lugola na kuongeza:
“Kama hakuna fedha, halafu tunatoa misamaha kiholela, basi ni afadhali bajeti ya mwaka huu tuzibe hiyo mianya, futa kabisa hiyo misamaha isiyo na tija.”
Lugola alisisitiza: “Hatuwezi kuendesha nchi kwa staili hiyo, lazima tufike mahali mambo ya kuwekeana kanuni kuwa tukikwamisha bajeti Bunge litavunjwa, acha livunjwe ili kuliponya taifa.”
Lugola alisema kama Serikali haitakuja na mwarobaini wa misamaha ya kodi, ukwepaji wa kodi, matumizi makubwa ya Serikali na kupambana na ufisadi na wizi, bungeni hapatatosha.
 
Mbunge wa Kasulu Mjini, Moses Machali (NCCR-Mageuzi), jana alisema kuwa angetamani kama Bajeti ya Serikali isipite mwaka huu ili wabunge watimize wajibu wao wa kikatiba wa kuisimamia Serikali.
“Nenda kwenye Ripoti za CAG, madudu ni yaleyale mwaka hadi mwaka, misamaha ya kodi ndiyo usiseme, matumizi ya anasa ndiyo balaa. Nchi inakwenda wapi?” alihoji Machali na kuongeza:
“Kama kweli wabunge wanaitakia mema nchi hii, tuungane, kama Serikali haiji na majibu ya madudu yote haya tusipitishe bajeti hii. Tuweke historia ambayo vizazi vijavyo vitatukumbuka.”
Wakati wabunge wengi wakipanga kukwamisha bajeti iwapo misamaha hiyo haitapunguzwa hadi asilimia 1 ya GDP, hadi kufikia Juni 30, 2013 misamaha hiyo ilikuwa Sh1.52 trilioni.
CAG
Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Ludovick Utouh alikaririwa akisema kuwa misamaha hiyo imepungua kwa asilimia 16 kutoka Sh1.81 trilioni mwaka 2011/2012 hadi Sh1.52 trilioni.
Mjumbe mmoja wa Kamati ya Bajeti, alisema wameapa kupambana ili misamaha hiyo ishuke hadi asilimia moja ya GDP na kwamba hakuna mantiki kwa nchi iliyo taabani kifedha kutoa misamaha ya kodi. “Tunataka hata hiyo asilimia moja ambayo tunataka ifikie, iwe ni misamaha yenye tija na tumesema wasipokuja na suala hilo hatutapitisha bajeti kwenye kamati na bungeni,”alidokeza.
Mkakati huo wa Kamati ya Bajeti na Bunge, umekuja katika kipindi ambacho harakati nzito za kukwamisha Muswada wa Sheria wa Kuondoa Misamaha ya Kodi kwenye VAT zikiendelea.
Zitto
Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC), Kabwe Zitto alisema baadhi ya wafanyabiashara wakubwa wanaonufaika na misamaha hiyo wanajipanga kukwamisha muswada huo.
Kwa mujibu wa Zitto, kama sheria hiyo ya VAT itafanyiwa marekebisho, ni dhahiri makundi hayo yanayonufaika na  misamaha ya kodi yataathirika na ndiyo maana yameungana kuikwamisha.
Mbali na kuwepo kwa sintofahamu hiyo, lakini wajumbe hao wameonyesha kutoridhishwa na utendaji kazi wa Waziri wa Fedha, Saada Mkuya anayedaiwa kuhudhuria kikao kimoja tu cha kamati.
“Nchi iko katika wakati mgumu kifedha, Waziri wa Fedha anakwenda Rwanda kuhudhuria kikao cha watu 3,000, badala ya kubaki Dodoma kutetea bajeti yake ya Sh19 trilioni,”alidai mjumbe mmoja.
Wajumbe wa kamati hiyo wanadai kuwa Mkuya amekuwa akiwatuma Naibu Mawaziri wake, Mwigulu Nchemba na Adam Malima ambao ni wageni wizarani kushiriki vikao vya Kamati ya Bajeti yeye akiwa safarini .
Mmoja wa wajumbe wa kamati hiyo aliyeomba jina lake lihifadhiwe, alidai hali ya kifedha ya Serikali ni mbaya na kwamba alitarajia Waziri wa Fedha angekuwapo Dodoma muda wote ili kuweka mikakati ya kuinusuru.
“Bajeti ya mwaka jana (2013/2014), ina deficit (upungufu) ya Sh1.8 trilioni, kwa maneno mengine kuna miradi ya maendeleo yenye thamani hiyo haikutekelezwa kabisa,” alidokeza mjumbe huyo.
Mjumbe mwingine alidai kuwa Serikali ina madeni makubwa ya mwaka jana, ambayo inataka kuyahamishia katika bajeti ya mwaka huu (2014/2015), ambayo itaathiri kwa kiasi kikubwa miradi ya maendeleo.
“Tunafahamu wabunge wanachachamaa, wanataka zile fedha tulizoidhinisha mwaka jana zitolewe kwanza ziende kwenye miradi, lakini tofauti na hivyo bungeni hapatatosha,”alidai mjumbe huyo.
Moja kati ya mambo ambayo Kamati ya Bajeti imeibana Serikali ni pamoja na kuitaka kubana matumizi makubwa na mengine ya anasa na kudhibiti mianya ya ukwepaji wa kodi. “Pale bandarini kuna mabilioni ya kodi yanakwepwa na tunaambiwa baadhi ya kampuni zina uhusiano na vigogo wa Serikali, wakitaka kukusanya kodi, vinakuja vimemo,”ilidokezwa.
Ukweli wa Serikali kuwa taabani kifedha unathibitishwa na namna wizara zilivyopokea fedha za maendeleo mwaka 2013/2014, ambapo baadhi zilipata kati ya asilimia 20 na 30.
Wizara ya Mifugo
Mathalan, Wizara ya Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi iliidhinishiwa Sh28.9 bilioni, lakini ilipokea Sh2.5 bilioni tu sawa na asilimia 13.4 wakati Wizara ya Katiba na Sheria ilipokea Sh9.9 sawa na asilimia 17.
Hali imeendelea kuwa hivyo katika Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi ambapo iliidhinishiwa Sh741.1 bilioni kwa ajili ya matumizi ya kawaida na miradi ya maendeleo, lakini imepokea asilimia 67 tu.
Katika mwaka unaomalizikia Juni 30, Bunge liliidhinisha Sh81 bilioni kwa ajili ya miradi ya maendeleo, lakini hadi kufikia Machi 31, mwaka huu ilikuwa imepokea Sh40.8 bilioni sawa na asilimia 50.38.
Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa (JKT), iliidhinishiwa Sh245.5 bilioni kwa ajili ya maendeleo, lakini hadi kufikia Machi 30 mwaka huu, ilikuwa imepokea Sh49.3 bilioni sawa na asilimia 20.1.
Mbali na wizara hiyo, Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto ilikuwa imeidhinishiwa Sh11.9 bilioni za miradi ya maendeleo, lakini hadi kufikia Machi ilipokea Sh2.9 bilioni pekee.
Kwa upande wake, Wizara ya Ujenzi iliidhinishiwa Sh845 bilioni kwa ajili ya miradi ya maendeleo, lakini hadi kufikia mwezi Machi, 2014 ilikuwa imepokea Sh604.4 bilioni sawa na asilimia 71.52.
Bajeti ya Wizara ya Maji na ile ya Nishati na Madini ilibidi zisogezwe mbele kama njia ya kusubiri hali ya hewa itulie baada ya wabunge wengi kujipanga kuzikwamisha.
Mbunge Keissy
.Mbunge wa Nkasi Kaskazini, Ally Keissy Mohamed (CCM), alisema suala hapa si kupunguzwa kwa misamaha ya kodi, bali ni kuifuta kabisa kwa kuwa hakuna mantiki kwa Serikali kudai haina pesa huku ikisamehe kodi.
“Mimi naunga mkono suala hili kwa kweli na mimi katika hili nitaibana Serikali tufute kabisa hii misamaha ya kodi na kwa kweli Serikali ibane matumizi… ina matumizi makubwa na sherehe kubwa,”alisema.
Mbunge wa Kinondoni, Idd Azzan (CCM), alisema kama ingewezekana, Serikali ingefuta misamaha ya kodi angalau kwa mwaka mmoja hasa katika kipindi hiki ambacho Serikali inapitia kipindi kigumu cha bajeti. Kwa upande wake, Mbunge wa Mkanyageni, Mohamed Habib Mnyaa (CUF), alisema hoja ya baadhi ya wabunge wa CCM kupanga kuikataa bajeti ni kiini macho tu, kwani hawana ubavu huo.
“Baadhi ya wabunge wa CCM wamewasaliti wapiga kura wao… badala ya kuisimamia Serikali kama Katiba inavyosema, wao wamegeuka watetezi wa Serikali… Nchi hii haiendi kwa sababu hiyo,”alisema Mnyaa.
Mnyaa alisema ijapokuwa wabunge wangeweka historia ya kuisimamia Serikali kwa kukwamisha bajeti, lakini wabunge wanaotokana na CCM hawawezi kufika huko, kwani wanahofu wakifanya hivyo Rais atalivunja Bunge na wao hawako tayari.
Chanzo:Mwananchi

No comments:

Post a Comment