MAAMBUKIZI ya ugonjwa wa ukimwi (VVU) katika Manispaa ya
Kinondoni yanaelezwa kuongezeka kutoka asilimia 5.6 na kufikia 6.8 kiwango
ambacho kimezidi kile cha kitaifa.
Hayo yalisemwa na Mratibu wa Kudhibiti Ukimwi wa Manispaa
hiyo, Mercy Ngekeno, wakati wa kufunga semina ya siku mbili iliyowahusisha watu
wanaoishi na VVU kutoka katika manispaa hiyo.
Ngekeno alizitaja sababu zilizochangia kuongezeka kwa
maambukizi hayo kuwa ni pamoja na
wingi wa madanguro, kaka poa na machangudoa
yanayopatikana ndani ya Manispaa ya Kinondoni.
Alisema sababu nyingine ni kuwepo kwa muingiliano mkubwa wa
watu kutoka maeneo mbalimbali wanaokuja kwa ajili ya utafutaji ajira na kufanya
shughuli nyingine kama ujenzi na miradi mbalimbali.
“Manispaa yetu ina mwingiliano mkubwa wa watu, lakini
madanguro, baa, klabu za usiku na machangudoa wamekuwa wengi sana, vitu
hatarishi ni vingi ndiyo maana maambukizi yako juu… tunachofanya sisi ni kutoa
elimu ya kujitambua ili kuepuka maambukizi mapya,” alisema Ngekeno.
Katika semina hiyo Naibu Meya wa Manispaa ya Kinondoni,
Songoro Mnyonge, ambaye ndiye Mwenyekiti wa Kamati ya Kudhibiti Ukimwi, alitoa
sh. milioni 27 kwa vikundi vitatu vya ujasiriamali vya watu wanaoishi na VVU
ili viweze kukopeshana na kupata mitaji ya kuanzisha biashara.
“Wapo wanaosema kwanini fedha zinapelekwa kwenye ukimwi na
zisielekezwe kwenye vipaumbele vingine, lakini bado eneo hili inahitaji
kukumbushana kwani binadamu ameumbwa kusahau, tukisema tunyamaze hali itakuwa
mbaya zaidi,” alisema Songoro.
No comments:
Post a Comment