Wakati
sakata la kuokotwa kwa viungo vya binadamu likiendelea kutikisa nchi,
Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS), kimesema
kuwa hutumia maiti 25 kwa kuwafundishia wanafunzi kila mwaka.Pia
chuo hicho hakijawahi kuagiza maiti kutoka nje ya nchi na kwamba ni mtu
mmoja tu aliyewahi kutaka maiti ya mtoto wake itumike kufundishia.Kauli
hiyo ya MUHAS imekuja siku chache baada ya Serikali kuamua kuifungia
Hospitali ya Chuo Kikuu cha Kimataifa cha Tiba na Teknolojia (IMTU),
baada ya kubaini kasoro kadhaa katika utendaji wake.Juzi, Serikali
ilifanya ukaguzi wa kushtukiza IMTU, baada ya hospitali hiyo kukumbwa na
kashfa ya utupaji wa mabaki ya viungo vya binadamu katika Bonde la Mto
Mpiji, jijini Dar es Salaam mwanzoni mwa wiki iliyopita.Hata hivyo,
wakati Tume ya Watu 15 iliyoundwa na Serikali kuchunguza suala hilo
ikiendelea na kazi, Mkuu wa Kitengo cha Anatomy MUHAS, Profesa David
Ngassapa amebainisha kuwa chuo hicho hutumia maiti 25 kwa mwaka.
“Sheria
ya mwaka 1963 inatutaka baada ya matumizi tuondoe mwili kwa heshima
zote na miongoni mwa vitu ambavyo wanafunzi wanasisitizwa ni kuhakikisha
wanaiheshimu miili hadi hatua za mwisho,” alisema Ngassapa.
Alieleza
kuwa pamoja na sheria kutoa ruhusa ya kutumia maiti katika mafunzo,
bado imeweka vipengele vinavyowataka madaktari kuiheshimu miili ya watu,
hadi hatua ya mwisho.
Ngassapa
aliongeza: “Sheria inaruhusu kuhifadhi mabaki ya miili kwa njia mbili;
kuizika na kuichoma moto, pia hospitali inaweza kuhifadhi mabaki hayo
hata kwa miaka mitano.”
Hajawahi kuagiza miili kutoka nje
Akizungumzia
utaratibu wa nchi kubadilishana maiti kwa ajili ya mafunzo, Profesa
huyo alisema kuwa kwa zaidi ya miaka 30 aliyokuwa katika kitengo hicho,
hawajawahi kuagiza maiti kutoka nje ya nchi.
Alisema
maiti zilizopo nchini zinatosha kufundishia wanafunzi wote wa udaktari
kwa kuwa siyo Hospitali ya Taifa Muhimbili(MNH), pekee inayotegemewa
kutoa miili hiyo.
Alisema
kuwa siku za nyuma, Serikali ilikuwa ikiagiza mifupa kutoka nje ya nchi
kwa ajili ya mafunzo, lakini sasa kila kitu kinafanyika hapa nchini.
Ngassapa
alisema kuwa miili iliyoharibika kwa ajali au magonjwa haifai kutumiwa
kwa kuwa mwanafunzi anatakiwa kujifunza kwenye mwili uliokamilika.
Amkumbuka mtu aliyetoa maiti ya binti yake
Alisema
kuwa historia ya Tanzania inaonyesha kuwa ni mtu mmoja pekee ndiye
aliwahi kujitolea maiti ya binti yake ili itumike kufundishia
“Alijitolea
kwa kuwa binti yake huyo alianza kuugua akiwa na umri wa miaka miwili
hadi alipofikisha miaka 12, muda mwingi akiwa amelazwa hospitalini
hapa,” alisema.
“Alipofariki
dunia mzazi alisema mtoto huyo ni wa hospitali na anamtoa kwa ajili ya
matumizi ya hapa. Ibada ya mazishi ilifanyika eneo la chumba cha
kuhifadhia maiti,” alisema Ngassapa.
Alifafanua
kuwa hata baada ya kukabidhiwa maiti hiyo, waliendelea kumhifadhi kwa
miaka minne, hadi walipojiridhisha kuwa wazazi hawatabadilisha mawazo.
Sheria inayotumika
Mkuu
huyo wa kitengo kinachoshughulikia mwili na viungo vyake, alisema kuwa
sheria ya Serikali ya mwaka 1963, ndiyo inayoruhusu chuo chochote cha
afya kuchukua mwili kama umekaa katika chumba cha kuhifadhia maiti kwa
siku 14 bila ndugu kujitokeza.
Ngassapa
alifafanua kuwa licha ya sheria kuwataka kuchukua mwili uliokaa katika
kipindi hicho, chuo huuhifadhi mwili huo kwa siku 30, ili kujiridhisha
pasipo shaka kwamba hakuna ndugu anayejitokeza kuuchukua.
Alibainisha
kuwa baada ya hapo, huuweka dawa ili usiharibike, kisha huuacha kwa
wiki mbili au tatu zaidi wakisubiri kama ndugu wanaweza kujitokeza.
“Inapothibitika kuwa hakuna anayejitokeza, chuo huuchukua na kuutumia kwenye mafunzo,” alisema.
Alifafanua
kuwa sheria pia inakitaka Kitengo cha Anatomy kuandika barua kwa mkuu
wa chuo na Mahakama Kuu, kutaarifu kuwa wamechukua mwili kutoka katika
chumba cha kuhifadhia maiti.
Rais
wa Chama cha Madaktari Tanzania (MAT), Dk Primus Saidia juzi aliliambia
Mwananchi kuwa miili ni mali ya Serikali na kwamba chochote
kinachofanyika kwa binadamu lazima kifuate sheria zilizowekwa na
Serikali.
Pia
alisema kwamba sheria inaruhusu nchi kubadilishana maiti, lakini hana
uhakika kama jambo hilo limewahi kufanyika nchini, ingawa ana uhakika
kuwa haiwezekani hospitali zikakosa maiti za kufundishia.
Credit: Mwananchi
No comments:
Post a Comment