Usilolijua litakusumbua! Msichana aliyejitambulisha kwa jina
moja la Mary (23), mkazi wa Dar ambaye ni mwenyeji wa Nyegezi, Mwanza, ameangua
kilio na kusema; ‘nabebeshwa madawa ya kulevya (unga), nalipwa kiduchu hadi
nimechoka’.
Awali, gazeti hili lilitonywa na vyanzo vyake juu ya kuwepo
kwa ishu hiyo maeneo ya Manzese, Dar ambapo uchunguzi ulifanyika na kumnasa
binti huyo ambaye alifunguka kila kitu.
Akizungumza na wanahabari wetu kwa uoga mkubwa, Mary alidai
kwamba alichukuliwa kutoka kijijini kwao huko Nyegezi ambapo alipofikishwa Dar,
alijikuta akiunganishwa kwenye mtandao wa kuuza ‘unga’.
“Nililetwa Dar mwaka jana na mwanaume mmoja, aliniahidi
kunitafutia kazi, niliishi naye kama mtoto wake.“Zilipita kama wiki mbili tangu
aliponileta bila kuniambia nitafanya kazi gani, siku moja ndipo akanipeleka
Mitaa ya Magomeni (Dar) na kuniambia nitakuwa nafanya shughuli za kuuza unga
huku nikiishi nyumbani kwake na yeye ndiye bosi wangu.
“Nilishangaa sana kuona ile ndiyo kazi niliyoahidiwa kuja
kuifanya Dar. Nilianza kumlilia bosi wangu anirudishe kwetu Mwanza lakini
alinigomea, hata pale nilipotafuta kisingizio cha kumwambia nimemkumbuka mama
yangu, aliniambia nimtumie nauli aje Dar,” alisema binti huyo akilengwalengwa
na machozi.
Baadhi ya madawa ya kulevya yaliyowahi kunaswa.
Aliendelea kusimulia kwa majonzi kwamba, siku hadi siku
amekuwa akiiona dunia ikimuelemea kwa kuwa amechoka na hayupo radhi kufanya
shughuli hiyo, kwani mbali na hatari yake haoni manufaa anayopata.
Alisema, awali alikuwa akilipwa Sh. 3,000 kila siku kwa
kupakia kwenye paketi na alipobadilishiwa kitengo na kuanza kuhesabu kete na
kubebeshwa amekuwa akilipwa kiduchu, yaani Sh. 50,000 kwa mwezi.
“Hii kazi sitaki hata kuisikia, nimeshafanya kwa mwaka mmoja
sasa, sijapata faida yoyote kwani nalipwa kiduchu huku nikiishi kwa hofu muda
wote hivyo nimechoka.“Kuna kipindi mama yangu alikuja na kufikia kwake,
alimnyanyasa na kumnyima nauli ya kurudi Mwanza. Alikuwa ananiambia kama vipi
nikajiuze nipate nauli ya mama yangu.
Kamanda Godfrey Nzowa.
“Sikuwa tayari kufanya hivyo, mama yangu akasaidiwa na
jirani akasafirishwa kurudi kijijini Mwanza,” alisema na kuongeza:
“Kuna wakati ananitishia maisha endapo nitatoa siri popote,
jambo ambalo limenifanya nikose uhuru na amani ya maisha, ndiyo maana
nimeshukuru kukutana na magazeti ya Global Publishers nitue huu mzigo.”
Katika kile kinachozidi kumtia hofu ni pale alipoambiwa siku
chache zijazo ataanza kusafirisha unga nchi mbalimbali na kupata utajiri mnono
jambo ambalo hataki kulisikia, kwa kuwa anaogopa kuozea jela hivyo kikubwa
anachohitaji ni msaada wa nauli ya kurudi kwao Mwanza akamsaidie mama yake
ambaye ni mzee na ni mgonjwa.
Kwa yeyote aliyeguswa na habari ya mwanadada huyu na
anahitaji kumsaidia nauli ya kumrudisha Mwanza, awasiliane nasi kwa namba
0719595558.
No comments:
Post a Comment