MCHAKATO wa kujadili na kuandika Katiba Mpya unaendelea
bungeni mjini Dodoma, licha ya kuwepo kwa mvutano na mgawanyiko wa makundi ya
wabunge wa bunge maalumu wanaojadili Rasimu ya
Pili iliyowasilishwa kwao.
Wakati hayo yakiendelea viongozi, wanaharakati na wadau wa watoto wanapendekeza
masuala ya haki za msingi za watoto yatambulike vizuri katika katiba ijayo.
Mwenyekiti wa Mtandao wa Mashirika yanayofanya kazi na
Watoto Tanzania ambaye pia ni Mratibu Miradi, Kituo cha Watoto wa Mtaani cha
Dogodogo Kigogo (Dogodogo Centre Street Children Trust), Sabas Masawe anashauri
ibara ya 43 ambayo inataja haki za msingi za watoto iendelee kuwepo mpaka
Katiba inakamilika na iboreshwe zaidi katika mchakato unaoendelea Bungeni.
Nasema haya maana tayari kuna baadhi ya watu wameanza kuhoji kwamba kwanini
hata watoto wanaingia kwenye katiba ilhali wao ni sehemu ya watu kama wazazi
wao.
Anasema pamoja na kuingizwa kipengele cha mtoto kwenye
rasimu ya pili ya katiba bado kuna mambo ambayo wao kama wadau wangependa
yaingizwe tena hivi sasa katika mchakato wa majadiliano unaoendelea. Anasema
baadhi ya mambo hayo ni kama umri wa mtoto mwenyewe kutaja wazi kwamba ni
kuanzia umri gani.
"...Unaweza ukaangalia hili ni suala la msingi sana
kutaja umri wa mtoto mwenyewe anayezungumziwa...kwa sisi wadau wa watoto
tunashangaa sana kwa maana nyingine tunaona suala hilo ni kama linaongeza
utata, kumuweka mtoto kwenye katiba ilhali umeshindwa kumtambua (kiumri) mtoto
ni yupi ni sawa na vichekesho...tunashauri mtoto huyu umri utajwe wazi kuondoa
utata...," anasema.
Mfano ukisema wazee wana haki ya kutibiwa bure lazima useme
huyu mzee anaanzia umri gani na kuishia wapi. Huwezi kusema wazee watibiwe bure
alafu unashindwa kuainisha vitu vya muhimu kama umri wao, bila hivyo utaleta
mkanganyiko wa tafsiri...ndiyo maana hata sasa mtoto anayetajwa tunataka tujue
anaanzia umri gani na kuishia umri gani. Sasa hili pekee linatushangaza watu
wasomi wanajadili bila kuliona
Mkuu wa Mkoa wa Tabora Fatma Mwasa akizungumza na mwandishi
wa makala haya.
Huyu mtoto akiingia kwenye mgongano katika sheria
anashughulikiwa namna gani kwasababu hili linaweza kuwa na mgongano kama pia
litashindwa kutajwa kwenye katiba chombo ambacho ni sheria mama ya nchi. Masawe
anasema mambo mengine ambayo yanatakiwa kuainishwa ni pamoja na kuelekeza namna
ya kuwawajibisha wazazi ambao wamekuwa wakikimbia majukumu yao ya kulea watoto
na kuwapeleka katika vituo vya yatima eti kwa madai wamewashinda.
"Hapa tunataka ijulikane pia hawa wazazi ambao wamekuwa
wakikwepa majukumu yao wanawajibishwa vipi...maana wengine tunawapelekea mtoto
wake anatamka wazi kwamba mimi huyu mtoto amenishinda kabisa, sasa kama
amekushinda nani wa kukulelea? Sasa watu kama hawa lazima ijulikane namna
wanavyowajibishwa kwenye katiba au kama ni jukumu la Serikali katiba ieleze
wazi ili iwe rahisi kumbana mtu kisheria," anasema Masawe.Katibu Mkuu wa
Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Watoto na Jinsia wa Tanzania, Anna Maembe,
anasema Serikali inawapenda watoto na ndiyo maana katika mchakato mzima wa
kukusanya maoni ilizingatia kupata maoni ya kutosha kutoka kwa watoto wenyewe
pamoja na wadau wengine wanaotetea haki za watoto.
Bi. Maembe anasema Ibara ya 43 katika Rasimu ya Pili imeweka
wazi haki za watoto pamoja na kufafanua zaidi. "...Ibara ya 43(1) (a) na
kuendelea hadi (g) inaongelea kabisa na kufafanua kwa kina haki ya mtoto...hii
ni pamoja na kulindwa, kuelimishwa, kupatiwa huduma za afya na huduma zingine
zozote muhimu ambazo zitamfanya mtoto akuwe na kufikia utimilifu ambapo naye
awe mzalishaji na mwananchi mwema...," anasema Bi. Maembe akizungumza na
mwandishi wa makala haya.
Anasema katika mchakato wa kukusanya maoni wadau wamepewa
nafasi ya kutosha katika kutoa maoni kwa ushirikiano na wabunge, wadau wengine
wa watoto, pamoja na mabaraza ya watoto ambayo yapo kila wilaya kutoa sauti za
watoto. Anasema anaamini ibara iliyopo sasa inayozungumzia haki za watoto
itaboreshwa zaidi mara baada ya mchakato kufikia mwisho hivyo kutoka na
mwongozo mzuri zaidi wa kutetea haki za kundi hilo la watoto.
"...Binafsi mi bado naamini kuwa mchakato wa katiba, mi
naomba niseme hivi mchakato wa katiba ni nafasi nzuri sana ya kuweza kutetea
haki za watoto wa Tanzania, kwa kuwa mtoto wa leo ndiyo mbunge wa kesho, kwa
hiyo tusipoweka haki zake vizuri hata wabunge wetu wajao hawatakaa wakatimiza
wajibu wao vizuri...kwa kuwa sisi wote tulianzia utotoni hadi kufikia hapa, kwa
hiyo mchakato wa katiba ufanye mambo yote lakini haki za mtoto zionekane vizuri
ili sheria zote za nchi ziweze kupata mwongozo kutoka kwenye katiba yetu
inayokuja ambayo ni sheria mama kuweza kutoa haki kwa
Katibu Mkuu wa Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Watoto na
Jinsia wa Tanzania, Anna Maembe akizungumza na mwandishi wa makala haya.
Hata hivyo anasema mbali na haki za mtoto kuzingatiwa katika
Katiba inayokuja bado watoto wanapaswa kuzingatia kuwa haki inakwenda sawa na
wajibu, hivyo nao wanapaswa kutimiza wajibu yaani wasome kwa bidii, wakubali
kuelekezwa na sio wafanye mambo yao kinyume kwa kuwa wanajua haki zao
zimezingatiwa.
Mkuu wa Mkoa wa Tabora Fatma Mwasa anaipongeza Serikali kwa
kitendo cha kutoa msukumo wa kipekee kwa kuwaingiza watoto katika Katiba Mpya.
Anaongeza kuwa Serikali ina kila sababu ya kufanya hivyo maana imeridhia
mikataba ya kimataifa kulinda haki za msingi za watoto, ambapo katika mikataba
hiyo imeainisha mambo ya msingi ya kuzingatia.
Haki ya kuishi, haki ya kupata elimu, haki ya afya haki ya
kuudumiwa na kulindwa. Anasema kikubwa ambacho tukiweza kukifanya kikapitishwa
katika katiba mpya ambacho kitasaidia kuongeza hatua ambayo Serikali imefikia
ni kiongeza umri wa mtoto wa kike kuolewa. Akifafanua zaidi Mwasa anasema suala
hilo limekuwa na ajenda kwa muda mrefu hasa tunapopigania masuala ya kijinsia,
usawa na haki za watoto.
Anasema eneo hili la umri wa kuolewa limekuwa likizua
mkanganyiko kwa wengi kwa kile upande mmoja sheria kuruhusu mtoto wa chini ya
miaka 18 kuolewa, licha ya upande mwingine bado sheria nyingine inamtambua mtu
chini ya umri wa miaka 18 ni mtoto.
"...Kimsingi eneo hili limekuwa likizua utata kwa
baadhi ya makundi katika jamii...hasa baadhi ya viongozi wa dini wao wanasema
mtoto wa Tanzania anamaliza elimu ya msingi akiwa na miaka 14 na hapo kama
hakufanikiwa kuendelea na sekondari hubaki nyumbani bila kuwa na cha kufanya,
wanasema mtoto huyu anaweza kujiingiza katika mchezo mbaya kama atakaa tu
akisubiri umri wa kuolewa wao wanaona kama amepata wa kumuoa ni bora akaolewa
kuliko kujikuta akijiingiza katika mambo yasiofaa," anasema Mkuu wa Mkoa
huyo.
Anasema hata hivyo anaishukuru Serikali kuleta shule za kata
maana idadi kubwa ya watoto sasa wanapata nafasi za kuendelea na masomo na
kujikuta wakiepukana na hatari za ndoa za utotoni, lakini pamoja na hayo
anasema bado kuna haja ya kujenga mfumo mzuri wa kuhakikisha suala la ndoa za
utotoni linatoweka kabisa. Pamoja na hayo anabainisha kuwa kuna haja ya Katiba
kutamka wazi kuwa mtoto asiruhusiwe kuolewa chini ya umri wa miaka 18.
Akizungumzia haki kwa makundi maalum ya watoto wakiwemo
walemavu, anawashauri wazazi wenye imani potofu kubadilika na kumchukulia mtoto
mlemavu ana haki zote kama ilivyo kwa watoto wengine. Anasema baadhi ya wazazi
wamekuwa wakiwaficha watoto wenye ulemavu ili wasiweze kupata haki zao ya
msingi.
"...Kwenye hili changamoto kubwa ilikuwa wazazi wenyewe
kufikiri kuwa kuzaa mtoto mwenye ulemavu ni jambo ambalo linaleta fedheha, hii
imekuwa ikisumbua sana maana wakati mwingine tunabaini watoto wenye ulemavu
wakiwa wamewekwa ndani wakati mwingine kwa miaka kadhaa...sasa hili tunaamini
sio haki maana mtu yeyote anaweza kuwa mlemavu wakati wowote hata mimi sasa
kumbagua juu ya haki kwa kuwa yuko vile sio sawa hata kidogo," anasema
Mwasa.
Bi. Valerie Msoka ni Mkurugenzi Mtendaji wa Chama cha
Wanahabari Wanawake (TAMWA), anasema ili mabadiliko katika jamii yatokee vyombo
vya habari vinahitajika sana na kwa namna yingine vinatoa mchango mkubwa.
Anatolea mfano kuwa kwa sasa matukio ya ndoa za utotoni bado yanashamiri kwa
baadhi ya mikoa kwa kiasi kikubwa. Anasema pamoja na vitendo hivyo kuendelea
vyombo vya habari ndiyo nyenzo pekee ambayo inaweza kubadili mtazamo katika
jamii na matendo hayo kukoma kabisa.
Anasema mijadala inayoendelea kutoka kwa jamii na vyombo vya
habari kuendelea kuripo inasaidia wajumbe wa Bunge la Katiba kupata taarifa za
kina zaidi juu ya masuala mbalimbali wanayoyajadili hivi sasa hivyo kuendelea
kuboresha zaidi. "...Mfano masuala ya ndoa za utotoni yanayozungumzwa hivi
sasa, ukeketaji na masuala mengine ya unyanyasaji wanayofanyiwa watoto na
vyombo vya habari kuandika yanawasaidia wabunge kuwa naufahamu zaidi
wanapochangia katika kamati mbalimbali za Bunge la Katiba...kwa maana hiyo
mchango wa vyombo vya habari unaitajika sana," anasema Bi. Msoka.
Bi. Valerie Msoka kulia ni Mkurugenzi Mtendaji wa Chama cha
Wanahabari Wanawake (TAMWA).
Anasema ili kuondoa utata juu ya umri wa mtoto; Katiba ijayo
ingemsaidia mtoto kutamka wazi kuwa mtoto wa kike au wa kiume haruhusiwi kuoa
au kuolewa akiwa chini ya miaka 18. Anasema hii ikitamkwa wazi watu wataelewa
na hata utoaji elimu kwa jamii juu ya umri wa mtoto na haki zake hauta kuwa wa
mkanganyiko kama ilivyo sasa.
Anasema kwa sasa zipo baadhi ya mila zinashindwa kumlinda
mtoto hasa wa kike hivyo kujikuta wanaozeshwa na kukosa haki zao za msingi ya
kupata elimu, ilhali sheria zinashindwa kuwasaidia kwa kile nayo kuwa wa utata
juu ya umri wa kuolewa kwa mtoto. Anasema katiba mpya ikitamka wazi masuala
hayo itakuwa rahisi kuwashughulikia wanaotumia udhaifu wa sheria na kumnyanyasa
mtoto.
Hata hivyo anafafanua kuwa pamoja na kuweka sheria ya kumlinda
mtoto katika hali zote za unyanyasaji bado jamii inatakiwa kupewa elimu ya
kutosha juu ya kuziacha mila na desturi zilizopitwa na wakati ambazo zimekuwa
zikimnyanyasa mtoto hasa wa kike. Mwanaharakati huyu ambaye pia ni Mjumbe wa
Bunge Maalum la Katiba anashauri elimu ya kuanzia msingi hadi kidato cha nne
itolewe bure na kwa watoto wote. Anasema mtoto atatakiwa kusoma hadi kidato cha
nne bure kama ilivyo darasa la saba sasa kisha kuchujwa kidato cha nne.
"...Nasema hivyo nikiwa na sababu kwamba ukiangalia
mtoto anayemaliza elimu ya msingi madarasa ambayo ni lazima kila mmoja apitie,
wanamaliza wakiwa wadogo sana, sasa kwa hali hii mi ninashauri kuanzia msingi
hadi kidato cha nne yangekuwa ni madarasa la lazima na bure ili watoto hawa
wapate elimu hadi kidato cha nne angalau hapa watakuwa wameongeza kitu kichwani
na miaka kusogea...," alisema.
Anasema mtoto anayemaliza katika kidato cha nne angalau
atakuwa amepata elimu kiasi, anajitambua na umri umeongezeka kidogo hivyo kama
wengine wataishia katika darasa hilo wanaweza kujitegemea na hata walioolewa
watajitambua hivyo kujenga familia ambazo zinajielewa kwa kiasi fulani tofauti
na ilivyo kwa sasa.
Kwa upande wake Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Watoto na
Jinsia wa Tanzania, Sophia Simba anasema takwimu zinaonesha kuwa Tanzania ni
kati ya nchi 20 Ulimwenguni ambazo zimekithiri kwa kuwa na ndoa za utotoni.
Aidha anabainisha kuwa takwimu pia zinaeleza katika kila watoto tano, wawili
kati yao wameolewa chini ya miaka 18. "...Hili ni tatizo kubwa sana,
fikiria kwa kila watoto watano wasichana wawili kati yao wameolewa chini ya
miaka 18, sasa ukiangalia utaona karibuni kila wakati kuna mtoto anaolewa Tanzania
akiwa chini ya miaka 18. Hili Serikali haiwezi kukaa kimya ndiyo maana kuna
programu mbalimbali zinafanywa kukabiliana na hali hii...leo tumezinduwa
kampeni za kukabiliana na hali hiyo Mara tutafanya hivi maeneo mengine pia
kupinga suala hili," anasema Bi. Simba.
Pili Muherisens (13) ni mwanafunzi wa darasa la tano katika
moja ya shule za msingi Wilayani Tarime. Binti huyu alilazimika kutoroka kwao
na kukimbilia eneo lingine akikwepa kukeketwa na wanaukoo kijijini kwao. Mtoto
huyu wala wazazi wake wote hakupenda kukeketwa baada ya kuhofia madhara ya
tendo hilo lakini ukoo ulishinikiza na ukatishia kama wazazi watazuia mtoto wao
kufanyiwa hivyo wangeliwatenga na mama yake kupigwa. Hapo ndipo binti alipoamua
kukimbia kijiji na kwenda kwenye vituo salama. Binti huyu anaomba Serikali
iwasaidie watoto kama hawa ambao hulazimishwa kukeketwa na hata kuozeshwa
mapema ikiwa ni vitendo vya unyanyasaji dhidi yao. Cha kujiuliza ni watoto
wangapi Tanzania ambao wanakumbana na unyanyasaji wa nguvu kama huu.
*Imeandaliwa na www.thehabari.com
No comments:
Post a Comment