Social Icons

IMETOSHA

IMETOSHA

Thursday, September 18, 2014

Mtuhumiwa Kesi ya Ugaidi Awalalamikia Polisi kwa Kumminya Sehemu zake za Siri na kumchomeka Mti sehemu za haja kubwa


 Mtuhumiwa katika kesi ya ugaidi, Abdallah Maginga, ameiomba Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha, kumruhusu kutohudhuria siku za kesi na abaki magereza, kutokana na maumivu makali anayodai anayapata sehemu za siri alikominywa na polisi na kuingiziwa mti kwenye haja kubwa.
“Mheshimiwa Hakimu naomba mahakama yako inipe ruhusa ya kutohudhuria siku ya kesi, sababu ninapopanda gari napata maumivu makali sana sehemu za siri kunauma kwa sababu polisi walinitesa kwa kuniingizia mti kwenye haja kubwa na kuminya sehemu zangu za siri,”alisema.
Alisema mbele ya Wakili wa Serikali, Rose Sulle kuwa mbali na 


maumivu ya sehemu za siri, pia mguu wake uliokatwa hospitalini, bado unamsumbua kutokana na maumivu.



Maginga pia aliomba iagize Magereza wamruhusu akatibiwe hospitalini, kwani alitakiwa kwenda kupata matibabu Septemba 5 mwaka huu, ila alizuiwa hadi sasa.
Akijibu hoja hizo, Hakimu aliyesikiliza kesi hiyo, Devotha Msofe, alisema  suala la kuja mahakamani ni lazima na mahakama haiwezi kumpa ruhusa hiyo.
Pia, alimshauri mshitakiwa huyo kuwa kama ana maelezo mengi, amweleze hakimu anayesikiliza kesi yake, Mustapher Siyani ambaye kwa siku hiyo hakuwepo.
“Sikiliza Maginga suala la kuja mahakamani ni lazima na sio hiyari wala majadiliano, ila kuhusu kwenda hospitalini liwasilishe Magereza ndio mtaona kwa pamoja mnafanyaje,” alisema.
Awali ilidaiwa mahakamani hapo kuwa washitakiwa  hao wameshitakiwa kwa makosa yaliyo chini ya Sheria ya Kuzuia ugaidi, ambapo Sheria Namba 22  ya Mwaka 2002 inasema upelelezi ukishakamilika, Mahakama Kuu ndiyo yenye mamlaka ya kuisikiliza na kutoa uamuzi.
Washitakiwa hao wanakabiliwa na mashitaka ya kuua, kujaribu kuua, kusajili na kusafirisha vijana kujiunga na Al-Shabaab.
Mbali na mashitaka hayo, pia wanahusishwa na  tukio la  mlipuko wa bomu lilitokea baa ya  Arusha Night Park jijini Arusha na kusababisha kifo cha mtu mmoja na kujeruhi wengine 16.
Watuhumiwa wengine wanaokabiliwa na mashitaka hayo ni Abdallah Athumani, Abdallah Thabiti, Ally Hamisi, Abdallah Wambura, Rajab Hemedi, Hassan Saidi, Ally Hamisi, Yassin Sanga, Shaaban Wawa, Swaleh Hamisi, Abdallah Yassin, Abdallah Maginga na Sudi Nassib Lusuma.
 Wengine walioongezwa katika shauri hilo ni Shaaban Mussa, Athuman Hussein, Mohammed Nuru, Jafari Lema, Abdul Mohammed na Said Michael Temba.

No comments:

Post a Comment