Mbunge wa Same Mashariki, Anne Kilango Malecela akizozana na
dereva wa mkuu wa wilaya ya Mbozi (aliyekataa kutaja jina lake) baada ya
kukuta gari la mkuu huyo wa wilaya likipeperusha bendera katika jimbo la Same
Mashariki jambo ambalo ni kinyume cha taratibu.
Katika hali isiyo ya kawaida, Mkuu wa Wilaya ya Mbozi mkoani
Mbeya, Dk Michael Kadege limekutwa likipeperusha bendera katika eneo la Wilaya
ya Same mkoani Kilimanjaro na kuzua tafrani kati ya mkuu huyo na Mbunge wa Same
Mashariki, Anne Kilango Malecela.
Gari hilo likiwa na Bendera ya Taifa, lilionekana saa nne
asubuhi likiwa limeegeshwa katika eneo la Mamba Myamba katika Jimbo la Same Mashariki
huku Dk Kadege akiwa kwenye mgahawa.
Kitendo cha gari hilo kuonekana likipeperusha
bendera
kilimfanya Kilango kulifuata akidhani ni la Mkuu wa Wilaya ya Same, ndipo
akakuta ni la Mbozi.
“Hili gari siyo la Same na kawaida mkuu wa wilaya nyingine haruhusiwi
kupeperusha bendera kwenye eneo ambalo siyo lake, huyu amekuja kwenye mambo
yake ya siasa, anapeperusha bendera ili wananchi wamwone kuwa yuko juu na hii
ni hujuma kwenye jimbo langu,” alilalamika Kilango.
Alisema Dk Kadege ni miongoni mwa watu wanaotaka kugombea
ubunge Jimbo la Same Mashariki lakini ni vyema akasubiri muda ukifika ajitokeze
hadharani badala ya kujenga mpasuko kwa CCM katika jimbo hilo.
“Huyu amekuja kwa ajili ya vikao vya ndani, mwaka 2005
tuligombea wote kwenye kura za maoni nikamshinda nikiwa na kura 389 yeye 46
akawa mtu wa nne, mwaka 2010 mimi nilipata kura 7,900 na yeye alipata 2,200
sasa ameanza, sikatai lakini asubiri muda wake,” alisema Kilango.
Kwa upande wake, Dk Kadege alisema hakuwa na taarifa kuwa
gari lake linapeperusha bendera kwa kuwa yeye hahusiki kuweka bendera, akataka
dereva wake aeleze sababu za kupeperusha bendera kwenye eneo lisiloruhusiwa.
Dk Kadege alisema yeye yuko likizo na alikwenda nyumbani
kwao Same kupumzika na hafanyi shughuli zozote za kisiasa katika jimbo hilo
kama inavyodaiwa na Kilango.
Dereva wa mkuu huyo wa wilaya ambaye alikataa kutaja jina
lake, alipohojiwa sababu za kupeperusha bendera katika eneo lisiloruhusiwa
alisema alikuwa akifanya usafi wa gari na alipohojiwa zaidi alidai siyo msemaji
wa mkuu wa wilaya.
Mkuu wa Wilaya ya Same, Herman Kapufi alisema kutokana na
sheria, utaratibu na miongozo ya wakuu wa wilaya, kiongozi huyo wa wilaya
haruhusiwi kupeperusha bendera katika eneo ambalo siyo lake.
Alisema kwa mujibu wa Sheria ya Tawala za Mikoa namba 19 ya
Mwaka 1997 na Sheria ya Serikali za Mitaa namba Saba na Nane ya mwaka 1982,
mkuu wa wilaya ni msimamizi wa shughuli za kimaendeleo na mwenyekiti wa kamati
ya ulinzi na usalama katika wilaya yake tu.
Kapufi alisema atawasiliana na Dk Kadege kama anafahamu
utaratibu na miongozo waliyopewa wakati wa kuanza kazi ili ajue kama alikusudia
kufanya hivyo au kama alipitiwa.
Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Same, Agust Kessy alipoulizwa
kuhusu hali hiyo alisema mipaka ya wakuu wa wilaya inatambulika ni jambo la
kushangaza kama mkuu huyo alikuwa ndani ya gari na asiione bendera ikipepea.
Alisema CCM imeweka utaratibu na kanuni zinazotakiwa
kufuatwa na kila mwanachama na kuwataka wenye lengo la kugombea wasubiri muda
ufike ili kuepusha mgongano na mtafaruku ndani ya chama. “Tuache kutegeana,
tusubiri filimbi ipigwe,” alisema Kessy.
No comments:
Post a Comment