MFANYABIASHARA mwanamama aliyetambulika kwa jina la Prisca
Paul Rugeiyamu au Mama Koku (34) ameuawa kwa kupigwa risasi na majambazi nje ya
geti la nyumba yake huku mwanaye Careen (12) akishuhudia.
Tukio hilo la kusikitisha lilitokea Januari 12, mwaka huu
saa mbili usiku maeneo ya Tabata Segerea jijini Dar ambapo kwa mujibu wa
chanzo, Prisca alikuwa akirejea nyumbani kwake ndani ya gari aina ya Vitz baada
ya kukusanya mapato yake ya siku kutoka kwenye biashara zake.
Mwili wa marehemu ukishushwa kaburini.
Akiwa nje ya geti la
nyumba yake akisubiri kufunguliwa, ndipo majambazi walitokea ghafla wakiwa
kwenye pikipiki na kulizunguka gari hilo na kutoa bastola wakitaka wapatiwe
fedha na laini za mitandao ya simu alizokuwa akizitumia katika biashara yake ya
huduma za kifedha kwa njia ya simu katika moja ya maduka yake.
Chanzo hicho kilisema kuwa, Prisca alibishana na majambazi
hao kwa muda ambapo walimpiga risasi ya mguuni na kumuongeza nyingine baada ya
kuendelea kugoma kutoa fedha.
Inaelezwa kuwa Careen
baada ya kuona hayo alikimbilia kwa bibi yake ambaye ni mama mzazi wa Prisca
anayeishi jirani na nyumba yao aliyefika eneo la tukio ambapo majambazi hao
waliokuwa wakijiandaa kutoweka walimpiga risasi ya mguu mama huyo na kuondoka
kwa kasi.
Mtoto wa marehemu akishika picha ya mama yake.
Akizungumza na waandishi wetu, ndugu wa familia hiyo
anayejulikana kwa jina la Geofrey Frank alisema kuwa baada ya kifo chake
walishangaa kuona wafanyabiashara wa madini wakija katika msiba na kudai kuwa
Prisca alikuwa mfanyabiashara mwenzao, na kuongeza kuwa marehemu hakuweka wazi
kazi yake hiyo.Amewaacha yatima watoto watatu, mkubwa ana miaka 12
huku wengine ni mapacha wana miaka saba. Mwili wa marehemu ulizikwa
Januari 15, mwaka huu katika Makaburi ya Segerea jijini Dar.
Imeandaliwa na Shani Ramadhani, Deogratius Mongela na Chande
Abdallah.
No comments:
Post a Comment