Mkurugenzi wa Huduma za Kisheria Wizara ya Ardhi, Nyumba na
Maendeleo ya Makazi, Rugonzibwa Theophil Mujunangoma akiwa chini ya ulinzi
wakati alipofikishwa mahakama.
Na Mwandishi Wetu
Vigogo wawili wa Serikali leo wamepandishwa kizimbani kwenye
Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es Salaam wakikabiliwa na kosa la
kupokea rushwa kutoka kwenye Akaunti ya Tegeta Esrcow.
Wakili wa serikali Bernad Son akishirikiana na Wakili Max
Ari, mbele ya Hakimu Mkazi Frank Moshi alidai kwamba, mnamo Februari 5, 2014
katika Benki ya Mkombozi wilaya ya Ilala jijini Dar es Salaam, Mujunangoma
alijipatia fedha kwa njia ya rushwa Sh.323, 400,000 kupitia namba ya Akaunti
yake ya benki 00120102602001 zikiwa ni sehemu ya Akaunti ya Tegeta Escrow.
Wakili Swai alieleza kwamba upelelezi wa shauri hilo
umekamilika, hivyo hakuna haja ya mshitakiwa kwenda kwa Mkurugenzi Mkuu wa
Mashitaka kuhusu pingamizi lolote.
"Naiomba Mahakama katika masharti ya dhamana itakayompa
mshitakiwa izingatie fedha alizochukua pamoja na kuzuia matumizi ya fedha hizo
kutokana na kuwepo kwa kesi mahakamani,"alieleza Swai.
Hata hivyo, Hakimu Moshi alimuuliza mshitakiwa kama
anakubaliana na kosa hilo, lakini mshitakiwa alikanusha kuhusika na kitendo
hicho.
Hakimu Moshi alimuachia mshitakiwa huyo kwa dhamana, baada
ya kukidhi masharti aliyopewa ikiwemo kuwa na wadhamini wawili ambao ni
watumishi wa umma, huku kila mmoja akitakiwa kutoa kiasi cha sh.25 milioni
keshi, na kuiahirisha kesai hiyo hadi Januari 29, mwaka huu.
"Mahakama hii..inazingatia haki, hivyo mshitakiwa
atakiwa kusafiri nje ya mkoa wa Dar es Salaam hadi apate ruhusa ya Mahakama
pamoja kutoruhusiwa kutoa fedha hizo hadi kesi itakapoisha,"alisema Moshi.
Kigogo wa pili anayekabiliwa na ufisadi huo ambaye ni Bwakea
alisomewa shitaka lake mbele ya Hakimu Mkazi Emmilius Mchauru, huku upande wa
Jamhuri ukiwakilishwa na Wakili Swai.
Akimsomea shitaka hilo, Wakili Swai alidai kwamba mnamo
Februari 12, mwaka jana katika Benki ya Mkombozi wilaya ya Ilala jijini Dar es
Salaam, Bwakea alijipatia rushwa ya Sh.161,700,00 kupitia Akaunti yake ya Benki
00410102643901 zikiwa ni sehemu ya Akaunti ya Tegeta Escrow, ambazo alizipokea
kutoka kwa Rugemalira.
Alieleza kwamba, mshitakiwa huyo alipokea rushwa hiyo akiwa
kama Mjumbe ambaye alihusika kuandaa sheria ya kuruhusu kuuzwa na kuzarisha
umeme katika Shirika la Tanesco, ikiwa kinyume na Kifungu cha 15 (1) cha sheria
ya kuzuia rushwa ya mwaka 2007.
Hakimu Mchauru alimuuliza mshitakiwa kama anakubaliana na
kosa hilo, lakini mshitakiwa alikanusha kuhusika na kitendo hicho. Pia alimtaka
mshitakiwa kutosafiri nje ya mkoa wa Dar es Salaam hadi apate ruhusa ya
Mahakama.
Baada ya kusoma shitaka hilo, Wakili Swai alidai kwamba upelelezi wa shauri hilo
umekamilika, hivyo hakuna haja ya mshitakiwa kwenda kwa Mkurugenzi Mkuu wa
Mashitaka kuhusu pingamizi lolote. Pia anaomba mahakama izingatie dhamana
kutokana na kiasi alichopokea mtuhumiwa.
Hakimu Mchauru alitaja masharti ya dhama kuwa mshitakiwa
anatakiwa adhaminiwe na watu wawili ambao ni watumishi wa umma pamoja na kulipa
fedha taslimu 10 Milioni kwa kila mmoja au hati inayofikia nusu ya fedha
alizochukua.
Katika kuzuia matumizi ya fedha hizo zilizochotwa, Hakimu
Mchauru aliutaka upande wa Serikali kuwasilisha maombi ya kutotumika kwa fedha
hizo hadi kesi itakapoisha.
No comments:
Post a Comment