SIKU chache baada ya Serikali kusema itazifutia usajili
shule zitakazokaidi agizo la kuweka viwango maalumu na tofauti vya ufaulu
kutoka kidato kimoja kwenda kingine, wadau wa elimu wamezungumza na kusema
agizo hilo linalenga kuua ubora wa taaluma nchini.
Akizungumza na HabariLeo, Katibu Mkuu wa Shirikisho la
Wamiliki na Mameneja wa Shule na Vyuo Visivyo vya Serikali (TAMONGSCO),
Benjamin Mkoya alisema viwango vinavyowekwa na shule
binafsi vinakubaliwa na
wazazi na kuwa kinyume chake shule hizo zitakufa kutokana na uwezekano wa
kufifia ubora wa kitaaluma.
“Viwango vinavyoweka huwa vinakubaliwa na wazazi, na lengo
la kufanya hivyo ni kutaka shule zifanye vizuri hivyo kuweza kujiendesha, kwani
mbali na kutoa huduma, tunafanya biashara,” alisema Mkoya.
Alisema suala la baadhi ya shule kupanga viwango vya ufaulu
limekuwa likifanyika muda mrefu na kuridhiwa na wizara husika ya elimu Julai
2013, baada ya agizo la kuifungia shule ya sekondari ya Mwilavya, Kasulu mkoani
Kigoma iliyopandisha viwango vya ufaulu hadi kufikia asilimia 45 kutokana na
matakwa ya wazazi.
Mkoya alisema suala hilo lilifika wizarani na uongozi wa
TAMONGSCO kukutana na Naibu Waziri (wakati huo akiwa ni Philipo Mulugo) ambaye
alisema kama wazazi wameridhia viwango hivyo, shule zinatakiwa kuendelea
kufuata viwango hivyo.
“Tulikutana na uongozi wa wizara, na hapa hatumuangalii mtu
aliyekuwepo ofisini bali taasisi,” na tulizungumza hilo, na hapo walisema kama
wazazi wanaridhia viwango hivyo basi hakuna sababu ya kugombana na wapiga kura
ambao wanataka viwango vya juu,” alisema na kuongeza kuwa kwa mwaka huu pekee
wameshafanya vikao na viongozi wa Wizara ya Elimu mara mbili kwa lengo la
kuboresha sera ya elimu na suala zima la Matokeo Makubwa Sasa (BRB).
Aidha, Mkoya alisema Serikali imekuwa ikitoa maagizo
mbalimbali yanaonekana kulenga kudhoofisha shule zisizo za serikali, na kutolea
mfano wa agizo lililotangulia lililotolewa na TAMISEMI likizitaka shule hizo
kutosajili wanafunzi mpaka hapo shule za serikali zitakapojaa.
“Serikali inatakiwa kutoona shule hizi kama ni ebola na
kuzipiga vita, badala yake wazione kama partner (mshirika) katika kuboresha
elimu hasa katika kufikia BRN. Mkoya alisema wakati umefika sasa, sekta ya
elimu kuwa na taasisi huru ambayo itasimamia elimu hapa nchini hivyo kuondoa
mgongano wa kimaslahi kutoka kwa serikali ambayo ni wamiliki wa shule na pia
ndio wanaosimamia elimu. “Tunataka mamlaka huru kama ilivyo SUMATRA, Wizara
ndio yenye shule na ndio inayosimamia elimu, hapa hapatakuwa na usawa,”
alisema.
Naye Mkurugenzi wa Huduma ya Elimu kwa Tume ya Kikristo ya
Huduma za Jamii (CSSC) ambayo ni Bodi ya muungano wa Baraza la Maaskofu
Katoliki Tanzania (TEC) na Jumuiya ya Kikristo (CCT), Petro Pamba alisema shule
zao hazitakwepa mfumo wa kupanga viwango vya ufaulu kwani unaandaa wanafunzi na
uwajibikaji kwa walimu.
Alisema taasisi yake yenye shule za sekondari 368 nchi zima
imekuwa ikiendesha shule kwa mifumo miwili ambayo ni shule za seminari ambayo
zinalenga kuwaandaa watumishi wa kanisa na ile ya kutoa huduma ya elimu kwa
jamii.
Alisema mfumo wa kupanga viwango vya ufaulu umekuwa
ukitumika muda mrefu na kujulikana na wizara na kwa sasa hawawezi kuukwepa
kwani umekuwa ukiwaandaa vizuri wanafunzi na uwajibikaji kwa walimu.
“Mfumo wa kuweka viwango vya ufaulu unawafanya walimu pia
wajitathmini, ukiwaacha walimu huru basi nao wanabweteka, hivyo sisi
tutaendelea na mfumo huo kwani umekuwa ukifanyika muda mrefu na mamlaka za
elimu zinaelewa,” alisema.
Alisema viwango vilivyopo sasa ni kati ya asilimia 40 hadi
49 na kuwa zaidi ya asilimia 50 kwa shule za seminari ambazo zinaandaa
watumishi wa kanisa.
“Huko kwenye seminari mchujo wetu ni mkali sana kwa sababu
ndio tunaowaandaa watumishi ambao watakuwa wakihudumia jamii hivyo kutakiwa
wawe vizuri kichwani,” alisema.
Hata hivyo, Pamba alisema taasisi yao inakamilisha mfumo
mbadala wa kuwasaidia wanafunzi wanaoelewa taratibu kwa kuwaandalia mafunzo
maalumu ili waweze kufanya vizuri mitihani ya mwisho na kuwa wale wenye alama
za chini watalazimika kurudia darasa.
Alisema pamoja na Wizara kutaka shule kufuata Sera ya Elimu
inayotaka viwango vya ufaulu kuwa ni asilimia 30, alisema sera hiyo inaelekeza
kwa wanafunzi wanapotakiwa kuvuka kutoka kidato cha pili kwenda cha tatu na si
katika madarasa mengine.
Alisema pia kiwango hicho cha ufaulu ni cha chini
ukilinganisha na mfumo mpya wa upangaji wa alama za ufaulu unaofanywa na Baraza
la Mitihani Tanzania (NECTA) ambayo ufaulu ni kati ya alama 40 hadi 49 (C),
huku alama 30 hadi 39 ni ufaulu hafifu ambao unatoa daraja D.
Alisema kutokana na alama hizo kupitwa na wakati, CSSC,
imepeleka pendekezo wizarani kutaka kubadilishwa kwa viwango vya ufaulu hadi
kufikia alama 40 kwa kidato cha pili kwenda cha tatu.
Alipoulizwa Katibu wa Elimu wa Baraza la Waislamu Tanzania
(BAKWATA) Mohammed Jongo alisema: ”Wizara ndio wasajili wa shule hapa nchini
hivyo tutatekeleza agizo lao.”
Kwa nyakati tofauti wakijibu maswali bungeni, Waziri wa
Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Dk Shukuru Kawambwa na Naibu wake Anne Kilango
Malecela walisema serikali itazifutia usajili shule zote za serikali au
binafsi, zitakazobainika kukaidi agizo la kuacha kuweka viwango maalumu na
tofauti za ufaulu kutoka kidato kimoja kwenda kingine.
Waraka wa Elimu Namba 6 wa mwaka 2011, umetoa maelekezo
kuhusu wastani wa ufaulu katika mtihani wa kidato cha pili ambapo kiwango cha
alama ya ufaulu ni asilimia 30 tu na si vinginevyo kwa shule za serikali na
binafsi.
No comments:
Post a Comment