TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) imesema
kuwa haikurupuki katika kuwashughulikia na kuwafikisha mahakamani viongozi
wanaotuhumiwa kujipatia fedha kutoka kwenye akaunti ya Tegeta Escrow na kwamba
ushahidi pekee ndiyo utakaofanya kuwafikisha mahakamani watuhumiwa.
Akizungumza mara baada ya kuzindua jengo la ofisi
ya mkoa la
taasisi hiyo mjini hapa juzi, Mkurugenzi Mkuu wa Takukuru, Dk Edward Hosea
alisema hakuna atakayeachwa katika sakata hilo, iwapo ushahidi utathibitisha
pasi na shaka kwamba alihusika.
Alisema uchunguzi dhidi ya viongozi na watu mbalimbali,
waliohusika na uchotaji wa fedha hizo, unaendelea na kwamba ushahidi
utakapokamilika, kila mmoja atapata kile anachostahili bila kumuonea.
“Hatutaki kukurupuka katika kushughulikia watuhumiwa wa
sakata la Escrow na muhimu ni ushahidi ambao utawatia hatiani watuhumiwa, ni
aibu kwangu kumfikisha mtuhumiwa mahakamani na mwisho wake siku ushahidi
hautoshi na mtuhumiwa kuachiwa huru,” alisema Dk Hosea.
Aliwataka wananchi kuwa na imani na chombo hicho katika
kushughulikia suala hilo na kwamba haki itatendeka kwa kuwashughulikia
watuhumiwa wote kwa haki.
Aliwataka wananchi waache kusikiliza kelele, zinazopigwa na
baadhi ya watu kwamba hawafanyi kitu au kuwashughulikia watuhumiwa wakubwa.
Tangu kuibuka kwa sakata la kuchotwa kwa fedha katika
Akaunti ya Tegeta Escrow, iliyokuwa imefunguliwa katika Benki Kuu ya Tanzania
(BoT) baada ya kuwepo kwa mgogoro wa kibiashara baina ya Shirika la Umeme
Nchini (TANESCO) na kampuni binafsi ya kufua umeme ya IPTL, hatua kadhaa
zimechukuliwa na Serikali.
Hatua hizo ni pamoja na kuvunjwa kwa Bodi ya Wakurugenzi wa
Tanesco na kutenguliwa kwa Uwaziri Profesa Anne Tibaijuka aliyekuwa Waziri wa
Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi.
Pia, Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Jaji Frederick Werema
alijiuzulu mwishoni mwa mwaka jana akidai kuwa ushauri wake katika suala hilo
haukueleweka, hivyo kuchafua hali ya hewa.
Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo pia
alijiuzulu mwezi uliopita na Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Eliakim Maswi
amesimamishwa kazi ili kupisha uchunguzi wa tuhuma dhidi yake juu ya ushiriki
wake katika sakata hilo.
Katika mkutano wake wa 16 na 17, Bunge lilitoa maazimio
manane, yakiwemo ya kuwawajibisha viongozi waliotajwa kuhusika kwa namna moja
ama nyingine na uchotwaji wa karibu Sh bilioni 300 katika akaunti ya Tegeta
Escrow.
Akaunti ya Tegeta Escrow ilifunguliwa BoT mwaka 2006 kwa
ajili ya kuhifadhi fedha za malipo ya tozo ya uwekezaji (capacity charges)
zilizokuwa zinalipwa na Tanesco, kabla hazijakabidhiwa kwa anayelipwa, ambaye
ni IPTL.
HABARI LEO
No comments:
Post a Comment