UCHAGUZI Mkuu wa tano wa Tanzania katika mfumo wa vyama
vingi vya siasa unatazamiwa kufanyika Oktoba mwaka huu. Ingawa haijafahamika
tarehe wala ni nani hasa atapewa nafasi hiyo ya kumrithi Jakaya Kikwete, angalau
majina kadhaa yanatajwa, kutoka kambi zote.
Wapo wanaotajwa kutoka CCM na kambi ya upinzani kwa ujumla
wao, ambao kwa jinsi tunavyoendelea, ni wazi kuwa watawakilishwa na mgombea
kutoka kundi la Ukawa. Kiuhalisia, hawa ndiyo wapinzani wakubwa wa chama
tawala, kwa sababu walio nje ya umoja huu, hawana nguvu.
Wote tunajua, kila mmoja anajipanga katika kundi analoamini
litashinda. Kuna rafiki yangu mmoja huwa ananipigia kelele kila siku,
akiniambia nisimame nihesabiwe, nisije sema sikuambiwa. Nabakia kucheka tu.
Mimi siyo mtu wa kusimama kinyonge na kuombea kudura za
kuhesabiwa. Ninaamini nina mchango mkubwa wa kuutoa kwa mtu atakayenipa kazi ya
kumnadi katika harakati zake za kuelekea magogoni, lakini sharti tukubaliane.
Siwezi kuwa kama wale wapiga mbinja wanaotegemea bahati
nasibu.
Kama nilivyosema mwanzo, wagombea watakaoshinda urais, kwa
maoni yangu, watatokea CCM au Ukawa, ingawa kwa uzoefu wa jinsi chaguzi zetu
zinavyoendeshwa, chama tawala kina nafasi kubwa ya kushinda katika nafasi hii.
Kwa maana hiyo, ajira hii ninaitafuta, kwanza kabisa kutoka CCM, lakini wakiona
sina vigezo, basi hata mgombea wa Ukawa nitamfanyia kazi.
Ili niwe katika kiwango huru cha kumnadi mgombea urais
atakayehitaji huduma yangu, ni lazima nimpe masharti ambayo anapaswa kukubaliana
nayo, vinginevyo, aniache kwa sababu nitamfanyia kampeni yeyote nitakayeona
anafaa wakati ukifika.
Sharti la kwanza kabisa analopaswa kukubaliana nalo ni
kunishawishi kwa hoja kuwa kweli yeye anafaa kuwa kiongozi wa taifa hili. Na
ushawishi huo, hautategemea kiasi gani cha fedha atanipatia, bali mbinu gani
atatumia ili kuwanusuru mamilioni ya Watanzania na maisha duni wanayoishi.
Nisipokubaliana na mbinu zake, aniache. Hii ni kwa sababu
nikiweka kigezo cha fedha atakazonilipa, sitakuwa nimetoa mchango kwa taifa
langu kwa sababu mimi sihitaji fedha zaidi ya hizi zinazoniwezesha kuishi hivi
ninavyoishi.
Ingawa wao mamilionea wananiona mimi hohehahe, lakini nina
uhakika mamilioni ya wananchi wanaishi duni kuliko mimi. Hao ndiyo ninaotaka na
wenyewe wainuke angalau wafikie hapa nilipo. Na hawa hawawezi kuinuliwa kwa
kuongopewa, watainuliwa kwa kuambiwa ukweli
wa mbinu za kubadili maisha yao, kwa sababu wakiziafiki, watashiriki
kujiinua!
Kwa hiyo hilo ndilo sharti langu la kwanza. Nipe hoja
nizikubali, kama unadhani nitafanya kazi hiyo kwa fedha, count me out!La pili,
ambalo pia ni muhimu sana, sitatumika kumchafua mgombea mwingine. Sioni faida
ya kufanya hivyo kwa sababu kama nitakuwa nimesharidhika na mikakati yake,
hakuna hata sababu ya kuhangaika na wapinzani wake, wa nini sasa wakati
tutawamaliza kwa hoja tu? Kwa hiyo akija mtu na kuniambia kazi yangu pia
itajumuisha na kumtukana, kumzushia, kumkejeli na kumdhalilisha mpinzani, mie
asinihesabie kabisa.
Ningeweza kutaja sifa zingine ambazo wanaonitaka niwe mpiga
debe wao walipaswa kuzijua, lakini hizi ndizo kubwa, kwa sababu zingine
zitakuwa zinaingia katika vifungu vidogo vidogo, kama vya uadilifu, uzalendo,
uucha Mungu na nyinginezo.
Kuhusu uwezo wangu kwa kazi hizo, wala wasiwe na hofu, kwa
sababu ninao ufahamu mkubwa mno wa matatizo ya wananchi, kwa vile hata mimi
nakumbana nayo. Kwa hiyo nitakapomwambia bosi wangu kuhusu tatizo la afya,
elimu, rushwa, matumizi mabaya ya madaraka na kero zingine za watu, ajue
ninazifahamu na nimeshaunguzwa nazo!Ninawakaribisha sana waheshimiwa wagombea,
hasa kutoka CCM!
No comments:
Post a Comment