BWENI la wanafunzi wa shule ya sekondari ya Idodi iliyoko
Jimbo la Isimani Wilaya ya Iringa
Vijijini Mkoani Iringa, limeteketea kwa
moto na kusababisha hasara ya mamilioni ya shilingi, ikiwa ni miaka sita
tu tangu bweni hilo liungue na kusababisha hasara kubwa na vifo vya wanafunzi
13.
Agosti 25, 2009 bweni la shule hiyo, liliwaka moto na
kusababisha vifo vya wanafunzi wa kike 13, ambao baadhi yao walizikwa shuleni
hapo baada ya miili yao kuharibika vibaya.
Katika tukio hilo, wanafunzi wengine 23 walijeruhiwa vibaya,
baada ya bweni hilo kushika moto uliosababishwa na mshumaa uliowashwa na
aliyekuwa mwanafunzi wa shule hiyo, Naomi Mnyali ambaye alisahau kuuzima baada
ya kumaliza kusoma.
Akizungumza kwa njia ya simu kutoka eneo la tukio, Kamanda
wa Jeshi la Zimamoto mkoani Iringa, Inspekta Kennedy Komba alisema kuwa bweni
hilo limeteketea lote na kuunguza baadhi ya mali, zikiwemo za wanafunzi
zilizokuwemo katika bweni hilo.
Alisema taarifa za awali zinaonesha chanzo cha moto huo,
kilitokana na hitilafu ya umeme na kwamba hakuna mwanafunzi yeyote
aliyejeruhiwa katika tukio hilo.
Komba alisema kuwa baada ya jeshi la zimamoto kupata taarifa
ya tukio hilo, lililotokea kati ya saa 3 na 4 jana asubuhi wakati wanafunzi wa
shule hiyo wakiwa darasani, iliwachukua dakika 45 kufika katika eneo la tukio.
Alisema baada ya kufika katika eneo la tukio kutoka Iringa
mjini ambako ni umbali wa kilometa 40, kazi ya kuuzima moto huo haikuwa kubwa,
kwani wananchi waliofika kutoa msaada, walifanikiwa kuzima moto huo kwa kiasi
kikubwa.
Aliwapongeza wananchi kwa moyo wa ushujaa wa kujitolea na
kuwataka kutoa taarifa mapema pindi majanga ya moto, yanapojitokeza katika
maeneo yanayowazunguka.
“Endapo tungepata taarifa mapema ninaamini tungeweza kuokoa
vitu vingi zaidi,” alisema Kamanda huyo na kuwataka wananchi wasitegemee
mtendaji au kiongozi apige simu kwa kikosi cha kuzima moto kwani kila mtu ana
fursa ya kupiga simu 111 katika kitengo cha mawasiliano cha jeshi hilo kuweza
kutoa taarifa ya majanga.
Aliongeza kuwa walitumia muda mdogo kufika eneo la tukio,
kutokana na ubora wa gari walilokuwa nalo na kuwashukuru wananchi kwa taarifa
na kuweza kuonyesha ushirikiano katika uzimaji wa moto huo usilete madhara
zaidi.
Akizungumzia hasara iliyosababishwa na moto huo, Komba
alisema tathmini kamili ya mali zilizoteketea, itafanywa kwa kushirikiana na
uongozi wa shule na taarifa yake kutangazwa.
No comments:
Post a Comment