UPANDE wa Mashikata kesi inayomkabili Kiongozi wa Jumuiya na
Taasisi za Kiislamu nchini, Shehe Ponda Issa Ponda umewasilisha ushahidi muhimu
wa mkanda wa video unaodaiwa kuonesha uhalisia wa tukio zima la kesi yake
inayomkabili ya kutoa maneno ya uchochezi.
Mkanda huo wa video uliletwa mahakamani hapo mbele ya Hakimu
Mkazi Mkoa wa Morogoro, Mary Moyo na kuoneshwa na shahidi wa tano wa kesi hiyo
ambaye ni askari kutoka makao makuu ya Jeshi la Polisi kitengo maalumu cha
uchunguzi wa picha,
Aristides alieleza vigezo alivyovitumia kuitambua uhalisia
wa video hiyo iliyochukuliwa Agosti 10 mwaka 2013.
Shahidi huyo akiongozwa na Wakili wa Serikali, Benard
Kongola alieleza mahakamani hapo kuwa video aliichunguza na kugundua kuwa
ilichukuliwa katika eneo la tukio kupitia kamera ndogo aina ya JVC na kwamba
baada ya kuichunguza aliandika hati na taarifa iliyoeleza vigezo alivyovitumia
katika uchunguzi huo na yale aliyoyaona na kuyasikia katika video hiyo ambayo
aliitoa mahakamani kama kielelezo.
Pamoja na ushahidi wake, lakini pia aliionesha video hiyo
mahakamani hapo ambapo ilionesha tukio zima pamoja na maneno aliyoyatoa Shehe
Ponda ambayo yanadaiwa kuwa yalikuwa ya uchochezi na yaliyoumiza imani ya dini
nyingine.
Shahidi huyo pia alitoa kamera, DVD, hati na taarifa ya
uchunguzi wa video hiyo kama kielelezo na kupokewa na mahakama hiyo.
Aliyekuwa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, Kamishna
msaidizi wa Polisi, Faustine Shilogile alikuwa shahidi wa nne katika kesi hiyo
ambaye alieleza kuwa baada ya kupata taarifa za kutafutwa kwa Shehe Ponda
kufuatia tuhuma mbalimbali zilizomkabili yeye kama kiongozi wa jeshi la polisi
mkoa aliandaa askari kwa ajili ya kumkamata baada ya kufika mkoani Morogoro.
Shahidi huyo alidai kuwa taarifa hizo za kiintelijensia
zilimhusisha Ponda na tuhuma za kumwagia tindikali wasichana wawili raia wa
Uingereza huko Zanzibar na tuhuma za kutoa maneno ya uchochezi jijini Dar es
Salaam na kwamba tuhuma hizo alizipata wakati akiwa kwenye adhabu ya kifungo
cha nje cha mwaka mmoja ambapo pia alitakiwa kutofanya kosa lolote katika
kipindi hicho cha mwaka mmoja.
Upande wa utetezi ukiongozwa na wakili Juma Nasoro
ulimuuliza maswali shahidi huyo, hata hivyo baadhi ya watu waliokuwepo
mahakamani hapo walishindwa kuzuia vicheko vyao kutokana na aina ya maswali
yaliyokuwa yakiulizwa pamoja na majibu yaliyokuwa yakitolewa.
Wakili wa utetezi: “Je wewe ulijuaje kama Shehe Ponda alitoa
maneno ya uchochezi?”
Shahidi: “Niliambiwa na OCD wangu kupitia radio call (simu
ya upepo) kwani alikuwepo eneo la tukio.”
Wakili: “Je, unayajua mashitaka yanayomkabili Shehe Ponda?”
Shahidi: ”Siyafahamu kwa kuwa mimi sio muandaaji wa hati ya
mashitaka.”
Wakili: “Ni askari wangapi uliwaandaa kumkamata Shehe
Ponda?”
Shahidi: “Sikumbuki”
Wakili: “Je, hukuandaa askari 25 hadi 30 kwa ajili ya
kumkamata Shehe Ponda? “
Shahidi: “Wewe ndio utakuwa umeeleza hiyo idadi”
Wakili: ”Je, askari wako walikuwa na silaha na kama walikuwa
nazo tunaweza kuamini kuwa wao ndio waliomjeruhi Shehe Ponda?”
Shahidi: “Ndiyo
baadhi ya askari wangu walikuwa na silaha lakini siwezi kufahamu Shehe Ponda
alijeruhiwa na nini.”
Wakili: “Je, unajua kama Msemaji wa Polisi, Advera Senso
alitoa taarifa kuwa kuna askari alisimamishwa kazi kupisha uchunguzi?”
Shahidi: “Sina taarifa na kama alitoa taarifa hizo basi ni
yeye na sio mimi.”
Wakili: “Je, kibali cha kufanya kongamano kilitolewa na nani
na je uliambiwa kama Shehe Ponda ni mzungumzaji katika kongamano hilo?”
Shahidi: “Kibali kilitolewa kwa OCD na sikuwa na taarifa
kama Shehe Ponda atakuwa mzungumzaji.”
Awali, upande wa mashtaka ulipanga kusikiliza mashahidi
watano hata hivyo mahakama ilishindwa kuendelea kusikiliza mashahidi wengine
watatu kutokana na muda kuwa umekwisha hivyo mashahidi hao watatu wataendelea
kusikilizwa leo Februari 10 katika mahakama hiyo.
Hata hivyo, kesi imeendelea kuvuta hisia za wakazi wengi wa
mkoa wa Morogoro na maeneo mengine huku hali ya ulinzi katika viwanja vya
mahakama hiyo ikiwa imaimarishwa na kufikia hatua ya kuweka vifaa maalumu vya
kuwakagua watu wanaoingia katika mahakama hiyo.
No comments:
Post a Comment