Mjumbe wa Baraza la Wadhamini wa Chama cha
Demokrasia na Maendeleo (Chadema) na Mbunge wa Moshi Mjini, Philemon
Ndesamburo, amesema anaweza asigombee ubunge kwenye uchaguzi mkuu ujao.
Ndesamburo (80), ameliongoza jimbo hilo kwa vipindi vitatu, tangu mwaka 2000, 2005 na 2010.
“Nitatangaza wakati ukifika kama nitagombea au sitagombea. Naapa
mbele yenu kwamba, nitatumia malipo yangu yote yanayotokana na kiinua
mgongo cha Bunge la Jamhuri ya Muungano Tanzania; zaidi ya shilingi
milioni 200 kwa ajili ya kumuunga mkono, yeyote atakayechaguliwa na
chama changu, kupeperusha bendera ya Chadema,” alisema Ndesamburo.
Aliyasema hayo jana, wakati akifungua semina elekezi ya siku moja
kwa viongozi wa Serikali za Mitaa pamoja na viongozi wapya wa Baraza la
Wanawake wa chama hicho (Bawacha), Manispaa ya Moshi. Aliwataka wakazi
wa Moshi pamoja na wakereketwa wanaoamini na kutetea siasa za
mabadiliko, waendelee kuamini jimbo hilo, atalitetea kwa nguvu zake
zote, hata kama atang’atuka madarakani baada ya muda wa ubunge kukoma
kikatiba; kwa kuwa hata wapinzani wao CCM, wanazifahamu nguvu zake
katika siasa, na kubatizwa jina la ‘Ndesa Pesa’.
Hata hivyo, kumekuwapo na minong’ono ndani ya chama hicho, kwamba
miongoni mwa wanachama wa Chadema; wanaotajwa kumrithi Ndesamburo katika
kiti chake cha ubunge kuwa ni Meya wa sasa wa Manispaa ya Moshi,
Japhary Michael.
Ndesamburo aliwaasa wanawake hao kuvunja makundi waliyotoka nayo
katika uchaguzi uliofanyika ndani ya chama na kuungana ili kuisaidia
Chadema kutwaa viti vyote vya udiwani na ubunge Manispaa ya Moshi.
“Mkiendelea na makundi, mtawapa CCM nafasi ya kushinda lakini kama
mnataka tuendelee kuwatesa kwenye ubunge na udiwani; vunjeni makundi
yenu ili tuendelee kuongoza halmashauri tuliyonayo.
Hamshangai Rais, Jakaya Kikwete alikuja Moshi na kuisifia
Halmashauri inayoongozwa na Chadema…Ameikubali kazi ya Meya (Japhary
Michael) na madiwani wake, wakisaidiwa na mbunge,”alisisitiza.
Ndesambauro ambaye pia ni Mwenyekiti wa Chadema mkoa wa
Kilimanjaro, aliwasisitiza viongozi hao wa Bawacha, kujipanga vyema kwa
kujiwekea mikakati thabiti inayotekelezeka kuelekea uchaguzi mkuu wa
rais, wabunge na madiwani, unaotarajiwa kufanyika mwezi Oktoba, mwaka
huu.
Mbunge wa Viti Maalum (Chadema) na Mwenyekiti wa Bawacha Mkoa wa
Kilimanjaro, Grace Kihwelu, akimshukuru Ndesamburo kwa kuwaunga mkono
wanawake, alisema Baraza hilo limefanikiwa kuwaweka pamoja wanachama
wake na kuyavunja makundi ya chaguzi.
“Tunakuahidi mheshimiwa Mwenyekiti wa mkoa, kwamba tumejenga umoja
na kujiimarisha. Tayari tumeanza kuwaanda viongozi na wanachama wetu
kuwahamasisha wananchi kujiandikisha kwa wingi katika daftari la kudumu
la wapiga kura, wakati Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), itakapoanza
rasmi zoezi hilo mkoani hapa,”alisema Grace.
Awali, Katibu wa Bawacha Manispaa ya Moshi, Ovena Kowero,
akizungumza katika semina hiyo, alisema hadi kufikia sasa, baraza hilo
limefanikiwa kudahili wanachama wapya 1,300 kutoka katika viunga vya
mjini huo.
CHANZO:
NIPASHE
No comments:
Post a Comment