ASKARI wa Jeshi la Polisi amejeruhiwa na madereva wa
pikipiki maarufu kama bodaboda katika fujo zilizoibuka juzi jioni katika eneo
la Mzinga, Kongowe Mbagala nje kidogo ya Jiji la Dar es Salaam katika Manispaa
ya Temeke.
Akizungumza kwa njia ya simu kuhusiana na tukio hilo jana,
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Temeke, Kihenye Kihenya alisema askari walikuwa
kwenye doria kwa kutumia pikipiki maarufu kama Tigo na
walipofika eneo la
Mzinga walimkamata dereva mmoja aliyebainika kuwa na matatizo kadhaa kwenye
pikipiki yake.
“Polisi walimkamata mwendesha pikipiki mmoja na ikabainika
kwamba alikuwa na makosa kadhaa ambayo yalimpasa alipe faini. Lakini madereva
wenzake walipoona amekamatwa wakaanzisha fujo na kumjeruhi mmoja wa askari kwa
kumpiga chupa usoni,” alisema Kihenya.
Aliongeza kuwa “Tumekamata bodaboda kumi na tano na tayari
tunaendelea na uchunguzi ili kuweza kubaini wahusika wakuu na tuweze
kuwafikisha mahakamani kwa kosa la shambulio,” alieleza.
Mashuhuda wa tukio hilo walisema fujo hizo zilikuwa kubwa
kiasi kwamba polisi walilazimika kuwatawanya washambuliaji kwa kupiga risasi za
moto hewani.
“Mimi nilifunga duka nikakimbia maana kulikuwa hakukaliki
hapa, walipompiga yule askari, uso wote ulitapakaa damu ndipo wakarusha risasi
hewani. Kila mtu alikimbilia anakojua mwenyewe,” alisema moja wa mashuhuda
aliyeogopa kutajwa jina lake.
Kwa upande wake, Sanja Justin, alisema yeye alikuwa ana
safari ya kwenda Mbagala na alipokaribia kituoni cha basi, alisikia mlio wa
risasi na kuamua kukimbia na kurudi nyumbani.
“Nilitaka kwenda kupanda gari nielekee Mbagala lakini
nilipofika karibu na kituo nikasikia mlio wa risasi, nikarudi mbio na kila mtu
alikuwa kwenye harakati za kukimbia ili kujiokoa na matatizo,” alisema.
Eneo la Mziga limekuwa na matukio mengi ya kihalifu ambapo
mwishoni mwa mwaka jana kuliibuka kikundi cha kihalifu kilichojiita Black
Amerika na kusababisha ukosefu wa usalama katika eneo hilo.
Hata hivyo Jeshi la Polisi lilifanikiwa kulidhibiti kundi
hilo na kurejesha hali ya utulivu kwa wakazi wa eneo hilo.
No comments:
Post a Comment